Mama, mwanaye wauawa kwa kukatwa vichwa

Miili ya mama na mtoto wake waliouwawa kwa kukatwa vichwa na kutengamishwa na viwiliwili vyao ikitolewa  nje ya nyumba tayari kwenda kuzikwa. Lilian Lucas.

Muktasari:

  • Mauaji hayo yanadaiwa kutokea Jana Ijumaa Novemba 24, 2023 saa 12 asubuhi katika Kitongoji cha Ilangali, kijijini hapo, katika familia ya Juma Maita.

Morogoro. Wakati siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zikiadhimishwa duniani, mkoani Morogogo, kumetokea tukio la kusikitisha ambapo mama na mtoto wake ambao ni wakazi wa Kijiji cha Mavimba wilayani Ulanga, wameuwawa kwa kutenganishwa vichwa na viwiliwili vyao.

Mauaji hayo yanadaiwa kutokea Jana Ijumaa Novemba 24, 2023 saa 12 asubuhi katika Kitongoji cha Ilangali, kijijini hapo.

Mwananchi Digital imemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama kuzungumzia tukio, hata hivyo  simu yake imeita mara kadhaa bila kupokelewa.

Akizungumza na Mwananchi Mwenyekiti wa Kijiji cha Mavimba, Salehe Ndopi amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo huku akiwataja marehemu hao kuwa ni Mwanaisha Matele (37) na mtoto wake Baraka Maita (7), ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili shule ya Msingi Mavimba.

Amesema mtuhumiwa wa mauaji hayo ni kijana aliyeletwa na rafiki wa mume wa marehemu, na baada ya kutekeleza mauaji hayo alitokomea kusikojulikana na vichwa vya marehemu hao.

Aidha Ndopi amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa kitongoji hicho, alifika eneo la tukio na kukuta miili ya mama na mtoto wake ikiwa imetapakaa damu, na ndipo alipotoa taarifa kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Lupilo na ofisi ya Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD).

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mlola, wilayani Ulanga, Masudi Kilalangongono ameeleza kuwa kijiji hicho kina utaratibu ya kuwatambua wageni wanaoingia, japo familia hiyo haikufuata utaratibu huo na kuishi na kijana huyo kwa wiki mbili.

“Hili la kutofuata utaratibu na kumuamini kijana huyo, lilimpa urahisi mtuhumiwa  kutekeleza mauaji hayo, wakati mume wa marehemu akiwa safarini mkoani Dodoma,” amesema diwani huyo.

Naye mkazi wa Kijiji cha Mvimba, Lukia Ngaomana amesema wamepokea taarifa za tukio hilo kwa masikitiko makubwa na kitendo hicho siyo cha kuvumilika, huku akioa wito kwa mamlaka husika kumkamata mtuhumiwa  na kumfikisha katika vyombo vya sheria.

Kijana huyo ambaye jina lake halikupatikana anatafutwa huku mwenyekiti wa kijiji Ndopi akieleza kuwa mtu aliyemleta akishikiliwa na polisi.