Walinzi watatu wauawa wakiwa lindo Geita

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Ally Kitumbu

Muktasari:

  • Walinzi hao watatu ambao walikuwa lindo wameuawa usiku wa kuamukia Desemba 22, 2022 kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na watu wasiojulikana.

Geita. Watu wasiojulikana wamewaua kwa kuwapiga na kitu kizito kichwani walinzi watatu wa kampuni binafsi ya ulinzi wakati wakiwa lindo eneo la mtaa wa Shilabela mjini Geita mkoani Geita


Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Ally Kitumbu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mauaji hayo yametokea usiku wa kuamukia jana Alhamisi Desemba 22, 2022.


Kitumbu amesema kuwa uchunguzi wa awali wa jeshi la polisi umebaini walinzi hao walivamiwa wakiwa wamelala na kushambuiliwa kwa ubao mzito na mtu asiyejulikana.

Kamanda Kitumbu amesema kuwa waliouawa ni Jumanne Shaban (35), Hendry Celestine (36) na Charles Shija (45)

Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo amelaani kitendo hicho na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kuimaruisha ulinzi na usalama ndani ya wilaya kuelekea kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.


Wakizungumuzia tukio hilo, wakazi wa mtaa wa Shilabela wameeleza kushtushwa na mauaji hayo na kuliomba jeshi la polisi kufanya ufuatiliaji ili watuhumiwa wakamatwe.


Joseph Shija ambaye ni mlinzi binafsi alisema mauaji ya walinzi mjini Geita yamekuwepo sana na kilichotokea jana ni matokeo ya kukosekana kwa mwarobaini wa kudumu wa kumaliza tatizo.