Andiko lililowasilishwa TCAA kuifuta au kuinusuru Fastjet

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya  Usafiri wa Anga (TCAA) Hamza Johari akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mkurugenzi Mtendaji wa Sekta Binaf-si Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye anasema ni muhimu kwa wafanyabi-ashara kufuata sheria za nchi pindi wanapofanya uwekezaji, lakini hata mamlaka za usimamizi kama zina nafasi ya kusaidia ustawi wa uweke-zaji huo tofauti na sheria zisaidie.

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku 17 kufikia mwisho wa notisi ya kusudio la kufutwa kwa leseni ya shirika la ndege la Fastjet Tanzania, hatima yake itaamuliwa na andiko lao la mpango wa biashara na fedha ambalo wameliwasilishwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).

Desemba 17, TCAA ilitoa notisi ya siku 28 ya kusudio la kufuta leseni ya shirika hilo kwa kile walichodai kuwa ni mwenendo usioridhisha, kutokuwa na ndege wala meneja mwajibikaji ambaye anapaswa kuwa ni mtaalamu wa operesheni na matengenezo ya ndege.

Pia, shirika hilo lilikuwa halijawasilisha mpango wake wa biashara na fedha tangu kujiondoa kwa Fastjet PLC, lililokuwa shirika mama.

Katika mahojiano na Mwananchi juzi, Mwenyekiti Mtendaji wa Fastjet Tanzania, Lawrence Masha alisema kwa asilimia kubwa ametekeleza matakwa ya notisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwa na meneja mwajibikaji, kuwasilisha mpango wa biashara na fedha na kuagiza ndege, lakini TCAA imezuia isiingie nchini. “TCAA inasema ili niweze kuingiza ndege hiyo nimalize kwanza madeni yote, baadhi ya madeni tayari yamelipwa na Fastjet Plc, mengine Fastjet Tanzania tunaendelea kulipa ikiwa ni pamoja na tiketi za abiria, lakini fedha imeisha,” alisema Masha.

“Kwa kuwa tayari fedha nyingine tulizitumia kutimiza matakwa yao, sasa wangeniruhusu nifanye kazi ili nipate fedha ya kulipa yaliyobaki. Hata hivyo kipaumbele changu ni kusafirisha abiria wangu, siyo kuwarudishia tiketi.”

Jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alisema tangu mamlaka hiyo itoe notisi, Fastjet Tanzania wamejibu Desemba 24 wakiwasilisha mipango yao ya biashara na fedha kama walivyotakiwa, uteuzi wa meneja mwajibikaji na maombi ya kuingiza ndege.

“Kuna mambo ya msingi ambayo lazima yafanyike, ametuletea andiko la kitaalamu kuhusu mambo yote tuliyoyahitaji, wataalamu wetu wanalipitia (andiko hilo), lina mambo mengi wanalifanyia kazi, angetuletea andiko hili mapema tusingefika hapa tulipo sasa, lakini hakufanya hivyo,” alisema Johari.

Pia, alisema mwenyekiti wa Fastjet Tanzania siku hiyohiyo aliiandikia TCAA kuwa amemteua Lawrence Masha kuwa meneja mwajibikaji, jambo ambalo bado linafanyiwa kazi kuona kama anakidhi vigezo.

“Miongoni mwa mambo ya msingi ni uwezo wa kifedha katika shirika, kwenye usafiri wa anga hakuna ujanjaujanja. Kama hatakidhi matakwa ya sheria na masharti yote, leseni yake itafutwa, tukisema tuhurumiane ni hatari, tutaua watu, usafiri wa anga usiposimamiwa vizuri ni hatari ndiyo maana ajali zake ni chache, kuna umakini mkubwa.”

Kuhusu kuzuiwa ndege, alisema hawakuizuia Fastjet kuingiza ndege zake mbili aina ya Boeing 737-500 Desemba 22 kama alivyoeleza Masha, bali maombi ya uingizaji yaliwasilishwa TCAA Desemba 24.

“Ndege zao aina ya Embraer190 ambazo zina usajili wa Tanzania hazitaruhusiwa kurudi kwa aliyewakodisha hadi madeni yote yatakapolipwa, mamlaka ina wajibu wa kuhakikisha watoa huduma kwa shirika wote wanalipwa,” alisema.

“Madeni ya Fastjet yalikuwa zaidi ya Sh6 bilioni wanazodaiwa na watu tofauti, tayari wamelipa baadhi ya fedha wanazodaiwa na TCAA japo si zote. Watoa huduma wengine bado wanadai.”

Alisema wanatoa ushirikiano mkubwa kwa mashirika yote ya ndege na si kwamba wanaipendelea ATCL, bali Fastjet ina matatizo yake yenyewe na wao wanajisikia vibaya wanapoona shirika linashindwa kuendelea na biashara.

“Tungeweza kulifuta shirika moja kwa moja kwa kuwa halijakidhi matakwa ya kisheria, lakini tumeendelea kuwa na mjadala nao, hii ni support tosha. Hata Masha kabla ya kununua shirika hilo tulimshauri kwanza alielewe na aelewe sekta kwa ujumla,” alisema Johari.

Mkurugenzi wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisema, “Sidhani kama Serikali imekusudia ibakie na ATCL pekee nchini, maana haitoshi, yanahitajika mashirika mengine zaidi yenye ustawi mzuri ili kukuza sekta hiyo, ndiyo maana Presicion Air bado ipo.”