Angalizo latolewa matumizi ya dijitali kutatua changamoto za jamii

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Utafiti waonyesha asilimia 90 ya kazi zote zinahitaji kuwa na maarifa kuhusu masuala ya teknolojia.

Dar es Salaam. Wanawake hususani vijana wametakiwa kutumia fursa za ukuaji wa teknolojia na matumizi ya kidijitali kutatua changamoto zinazoikabili jamii.

Hilo likifanyika, imeelezwa ushiriki wa wanawake utaongezeka katika masuala ya teknolojia, hivyo kukuza usawa wa kijinsia.

Hayo yameelezwa leo Mei 23, 2024 wakati wa mdahalo kuhusu ujuzi wa kidijitali kwa maendeleo ya rasilimali watu katika wiki ya ubunifu kwa mwaka 2024, yenye kaulimbiu ‘ubunifu kwa uchumi shindani.’

Wiki ya ubunifu imeandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na Mradi wa Ubunifu wa Funguo chini ya Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Mtaalamu wa kuwawezesha wanawake kiuchumi kutoka UN-Women, Lilian Mwamdanga amesema japo kuna mambo mbalimbali yamekuwa yakifanyika kuhakikisha teknolojia inakua, jitihada zaidi zinahitajika ili kuhakikisha inawanufaisha wanawake na wanaume kwa usawa.

Mwamdanga amesema jitihada hizo ni muhimu kufanyika ili kutowaacha wanawake nyuma kwani utafiti wa hivi karibuni unaonyesha asilimia 90 ya kazi zote zinahitaji kuwa na maarifa kuhusu masuala ya teknolojia.

"Hapa nchini takwimu zinaonyesha katika wataalamu watano wa masuala ya sayansi na uhandisi mmoja ni mwanamke, jitihada kubwa zinahitajika kuziba pengo hilo ikiwemo kuhakikisha wanawake wanapata zana na mafunzo kuwawezesha kupata maarifa ya dijitali," amesema.

Mchambuzi wa miradi kutoka UN-Women, Michael Jerry amesema ili kufikia usawa wa kijinsia katika masuala ya teknolojia, wameanzisha programu mbalimbali ikiwemo ya ‘Binti dijitali’ ambayo imelenga kuwawezesha mabinti wenye umri kati ya miaka 17 hadi 25 kwa kuwapatia mafunzo yatakayowawezesha kufanya ubunifu katika masuala ya teknolojia.

Amesema kwa mwaka 2023 programu hiyo iliwafikia mabinti zaidi ya 100 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

"Baadhi yao baada ya kupata mafunzo wamejiajiri, kuajiriwa na hata kuja na bunifu wa aina mbalimbali," amesema.

Mkufunzi wa masuala ya dijitali, Suna Salum amesema ili kufikia usawa huo katika teknolojia Serikali na wadau wanatakiwa kushirikiana ili kuwafikia walengwa kwa urahisi.

Anna Kweka, mshiriki wa mdahalo huo amesema hilo litafanikiwa iwapo Serikali itawekeza katika miundombinu na vifaa vya kutosha kujifunza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na wakufunzi wa kutosha katika shule za mijini na vijijini nchini.

"Kama hakuna walimu wa kutosha vifaa kama vile kompyuta na intaneti yenye uhakika hatuwezi kufanikiwa katika hili," amesema.