Anna Abdallah: Nilipoteuliwa walishangaa, lakini sasa hawashangai tena 

Muktasari:

  • Wanawake wako kwenye kilele cha shangwe cha kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani na mwanasiasa mkongwe, Ana Abdallah anasimulia mambo yaliyozungumzwa wakati akiteuliwa kuwa mkuu wa wilaya wa kwanza Mwanamke mwaka 1973.

Dar es Salaam. Jina la Anna Abdallah si geni masikioni mwa wengi. Katika medani za siasa, atakumbukwa kushika nyadhifa mbalimbali hasa ule wa kuwa mkuu wa mkoa wa kwanza mwanamke. 

Anna Abdallah, kadhalika amewahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri wa Ujenzi na nyadhifa zingine kubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake. 

Leo Ijumaa Machi 8, 2024 wakati dunia inaadhimisha Siku ya Wanawake, Ana Abdalah, anatukumbusha historia yake katika siasa na uongozi na anakumbuka siku alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa. 

“Wakati ule tulikuwa na uongozi wa kofia mbili, niliteuliwa mkuu wa mkoa na mwenyekiti wa chama wa mkoa, jina langu lilipotajwa tu, kiongozi mmoja wa chama akasema, yaani mnamteua huyu mnataka mkoa wetu uwe wa majaribio?,” anasimulia mama huyu shupavu.

Anasema uteuzi wake ulisababisha mshtuko mkubwa kwa watu wengi lakini, alipopata nafasi ya kusimama anasema aliwaambia: “Nataka niwaeleze kuwa nitaifanya kazi hii vizuri na nitawaonyesha kuwa sikukosea na mimi niliendelea kupanda hadi kuwa waziri.” 

Anna anasema wakati ule watu wengi walishangaa juu ya uteuzi wake. Lakini, hali hiyo ya kushangaa inamkumbusha pia hata Samia Suluhu Hassan alipoteuliwa kuwa Makamu wa Rais na hatimaye Rais wa nchi, wapo walioshangaa kidogo lakini hivi sasa wameacha kushangaa.  

“Rais Samia amefuta ile dhana ya kwamba, wanawake wakiwezeshwa wanaweza na sasa imekuja dhana kuwa wanawake wanaweza wakipata nafasi,” anasema Anna.

Anasema akiwa mtangulizi katika ulingo wa siasa, alijifunza kutumia nafasi yake kuwajenga wanawake wengine, jambo ambalo anasema hata Rais Samia analitekeleza kwa vitendo.  

Anasema katika kipindi kifupi cha Rais Samia madarakani, wanawake wengi zaidi wameteuliwa katika ngazi za kichama, kisiasa na za uchumi.  

“Nawaomba wanawake wasimkatishe tamaa Rais Samia, waonyeshe kwamba uteuzi wao haukuwa wa bahati mbaya au wa upendeleo bali wana sifa za kuwa hapo walipo,” anasema mama Anna.  

Anasema kuna mtazamo wa kidhanifu kuwa wanawake hawapendani na yeye anaukataa akisema aliwashika mkono wanawake wengine hasa katika ngazi ya chama alipokuwa Mwenyekiti wa UWT wakati ule. 

“Wakati ule, kwanza tulihakikisha, ndani ya chama wanawake wanakuwepo katika maeneo mengi. Katika teuzi za wagombea, nilisimama imara kuhakikisha mwanamke hakatwi kugombea bila sababu,” anasema. 
Anasema aliweka msingi kwamba iwapo kuna sababu ya mwanamke mgombea kukatwa, basi isitofautiane na ya mwanaume, vigezo na sifa za kumkata mgombea mwanaume viwe vilevile kwa mwanamke. 

“Kama kuna sababu basi iwe ya msingi na kama mwanamke anakatwa basi sifa na vigezo vilevile vitumike kumkata mwanaume. Nilisimama bila aibu, kama ni sifa mfano mzururaji, mwanamke asiwe mzururaji na mwanaume asiwe mzururaji,” anaongeza. 

Hata katika kampeni, anasema alihakikisha wanawake wanaweka nguvu kubwa kwa kwenda katika kampeni na kuchagua viongozi hasa wanawake wenzao.  

“Tusiendekeze haya maneno kwamba wanawake wenyewe hawapendani, tuachane na hayo maneno ya kupandikiza,”anaonya mwanasiasa huyu ambaye kwa sasa amepumzika kwenye majukwaa. 
 
Changamoto za wanawake katika siasa na uongozi 
Akizungumzia changamoto za siasa na uongozi kwa wanawake, Anna anasema zipo, lakini anasisitiza kuna masuala wanawake wanajitakia wenyewe. 

Anasema suala la rushwa ya ngono kwa wanasiasa wanawake ni muhimu kupima na kuwa na nguvu ya kuyashinda majaribu hasa ya wanaume. 

Anna anasema wakati mwingine mwanamke mwanasiasa anaweza kuwa yupo na marafiki zake wanakunywa mvinyo, lakini watamshutumu kuwa ni mlevi, lakini wakati huo huo mwanasiasa mwanaume anakunywa glasi tano za mvinyo na kila mtu anaona, huyu ataonekana kufanya vile yuko sahihi. 

“Haya mambo yapo, ni kweli wanawake wanadhalilishwa, mengine tunayaendekeza inabidi tuyakatae,” anasema na kuongeza:  

“Nashukuru katika hizi sheria za hivi karibuni, kumdhalilisha mgombea ni kosa la uchaguzi, zamani ilikuwa kosa la jinai. Hii ni nguvu kubwa,” anasema mama huyu. 

Kwa mara kwanza Anna alichaguliwa kuwa mbunge wa Viti Maalum mwaka 1975, katika Bunge ambalo lilikuwa na wanawake watano tu. 

Kihistoria, Anna ana taaluma ya uuguzi na hilo lilimpa hadhi na nafasi nzuri baadaye ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Afya, kuanzia mwaka 2000 hadi 2005.  

Anakumbuka historia yake katika uongozi na kusema:  
“Tungekosea sisi wakati ule, basi ingekuwa hadithi, mimi na watangulizi wenzangu tulionyesha uwezo na kuonyesha mwanamke ana uwezo sawa na wanaume ndiyo maana tukaendelea kuaminiwa,” anasema. 

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake mwaka huu, yamebebwa na kauli mbiu isemayo, ‘Wekeza kwa Wanawake ili kuharakisha maendeleo.’

Maadhimisho haya yamekuja wakati tunaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu na uchaguzi mkuu hapo baadaye mwaka 2025. 

Rais Samia Suluhu tayari ameonyesha dhamira ya wazi ya kugombea nafasi hiyo kubwa kitaifa na hiki ndicho anachosema, Anna: “Ninachojua ni kuwa Rais Samia atagombea, na tunataka agombee, linganisha aliyoyafanya katika miaka mitatu na miaka 60 ya Uhuru, je akikaa miaka mingine mitano, itakuwaje?” 

Anasema Rais Samia amekaa madarakani katika kipindi kifupi na kuonyesha kuwa Rais mwanamke, ana nguvu. Pamoja na hayo, Anna, anaasa wanawake kuwa wasiyumbishwe na dhana ya kuwa ‘wanawake hawapendani.’  

“Wanawake tupendane, tusaidiane, tuaminiane, hili ni jambo kubwa sana na yapo mambo yamepandikizwa katika mioyo ya wanawake, kuwa hawapendani. Hatuwezi kwenda wote tukapata vyeo, wote tukawe mawaziri, lazima waende wachache watakaosimama kwa niaba yetu,” anasema Anna.