Arejeshewa pete ya uchumba baada ya maziko

Muktasari:

  • Bibi harusi huyo, ambaye alikuwa ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Sua, mkoani  Morogoro, alivalishwa pete ya uchumba na mchumba wake huyo,  Septemba 2, 2023 na Novemba 24, mwaka huu alifanyiwa  send off, katika ukumbi wa Glonency, mkoani humo.

Moshi. Tukio la kukabidhiwa pete ya uchumba, aliyekuwa bwana harusi mtarajiwa, Aman Mollel  aliyokuwa amemvisha mchumba wake Rehema Chao (39), aliyefariki kwa ajali ya gari akitokea kwenye send-off, limeibua kilio upya kwa mchumba wake huyo pamoja na waombolezaji wengine waliokuwepo kwenye maziko.

Bibi harusi huyo, ambaye alikuwa ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Sua, mkoani  Morogoro, alivalishwa pete ya uchumba na mchumba wake huyo,  Septemba 2, 2023 na Novemba 24, mwaka huu alifanyiwa  send off, katika ukumbi wa Glonency, mkoani humo.

Leo, Desemba 2, 2023 ndiyo ilikuwa ifungwe ndoa yao katika Usharika wa Oldonyosambu, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), mkoani Arusha, lakini wakati akiwa njiani kurudi Kilimanjaro kwa ajili ya maandalizi ya harusi hiyo, ndipo alipopata ajali.

Ajali hiyo ilitokea Novemba 28, baada ya gari alilokuwa akiendesha kugongana na lori wakati akijaribu kukwepa shimo, eneo la Kichwa cha Ng'ombe wilayani Mwanga na kusababisha vifo vya watu watatu akiwemo yeye, mama yake mzazi na mfanyakazi wa nyumbani, huku mdogo wake na mwanaye wakijeruhiwa katika ajali hiyo.

Baada ya shughuli za maziko kumalizika nyumbani kwao katika Kijiji cha Nganyeni, Wilaya ya Moshi, Mchungaji aliyekuwa akiongoza ibada hiyo, Calvin Koola akiwa na wachungaji wengine alimuita Mollel na kumkabidhi pete hiyo.

Hata hivyo, baada ya kupokea pete hiyo huku akishindwa kujizuia kulia, wachungaji walimtaka akae kwenye kiti na wote kwa pamoja wakamzunguka na kumuombea.

Akizungumza baada ya kukabidhi pete hiyo, Mchungaji Koola ambaye ni Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki, Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, amesema wameamua kumkabidhi Mollel pete hiyo kwa kuwa ndiye aliyemvisha, hivyo hakuna mwingine wa kuichukua.

"Pete ile mwanaume ndiye alimvisha, na sasa mwenzake hayupo kwa hiyo familia walikuwa na ile pete wakauliza sasa wanaipeleka wapi na yeye hayupo, ndipo nikamkabidhi aliyekuwa bwana harusi mtarajiwa, lakini wangeweza kumuacha aende nayo," amesema Mchungaji Koola na kuongeza kuwa

"Hakuna kitu cha kiibada pale, ni kwamba ile pete alivikwa bibi harusi lakini walimvua wakati wa kumuandaa sasa wakaniuliza inakwenda wapi na mimi nikawaambia kwa kuwa aliyekuwa bwana harusi yeye ndiye aliyenunua na kumvika, basi akabidhiwe; maana walishamvua na hakuna mwingine anayeweza kuachiwa pete hiyo."

Mchungaji amesema licha ya kwamba kwa bwana harusi pete hiyo inawezakuwa inamtonesha na kumkumbusha mtu ambaye alimpenda na kutarajia kumuoa, lakini hakuna mtu mwengine ambaye angeweza kupewa.

"Ni kitu ambacho hakiwezi kufutika, hata kama akijakuoa mwingine, hawezi kumsahau mpendwa wake na mke wake mtarajiwa kwa kuwa alishamposa na kufanya maandalizi yote lakini jambo lile halikuweza kufikiwa mwisho ule ambao walilolitamani," amesema Mchungaji Koola.

Aidha Koola amesema: "Kwa hiyo alama ambayo bwana harusi huyu anaweza kubakia nayo ni zile picha za Send-Off na hiyo pete, ambayo kiukweli sijui ataipeleka wapi kwa sababu hata akimchumbia mtu mwingine sidhani kama anaweza kumvisha pete hiyo."

Alipoulizwa kama pete hiyo anaweza kumvika mwanamke mwingine, Mchungaji Koola amesema hapana kwa kuwa agano alilokuwa ameweka na Rehema (marehemu) haliwezi kuwa agano atakaloweka na mwingine.

"Ile pete ilikuwa ni ya mtu mwingine, sidhani kama anaweza kumvusha mtu mwingine na angeuliza kama anaweza kumvisha mtu mwingine, sisi tungemwambia hapana kwa sababu agano alilokuwa ameweka na Rehema haliwezi kuwa agano la mwingine atakayetokea," ameelekeza Mchungaji Koola.

Rehema na mama yake mzazi wamezekwa leo nyumbani kwao ambapo mamia ya waombolezaji, kutoka maeneo mbalimbali nchini walishiriki.