Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bwana harusi mtarajiwa amlilia mchumba wake aliyefia ajalini

Muktasari:

  • Bibi harusi mtarajiwa, Rehema Chao alifariki dunia Novemba 28, 2023 pamoja na mama yake mzazi, Agness Chao na mfanyakazi wa ndani wa mdogo wake, Irene Shija wilayani Mwanga, baada ya gari alilokuwa akiendesha akitokea mkoani Morogoro kwenye ‘send-off’ yake kugongana na lori lililokuwa likitokea Arusha.

Moshi. "Msiba huu tumeupokea tofauti na zaidi ya maumivu kama ambavyo hakuna mtu anayeweza kupokea msiba na kuukubali, sasa hivi tuko kwenye maandalizi ya msiba hatuwezi kuzungumza chochote kwa sasa."

Ni maneno aliyozungumza aliyekuwa bwana harusi mtarajiwa wa Rehema Chao (37), Amani Mollel, mkazi wa Oldonyosambu, mkoani Arusha, huku akilengwa na machozi. Mollel ameyasema hayo leo Novemba 30, akiwa nyumbani kwa familia ya aliyekuwa  aliyekuwa mke mtarajiwa (Rehema) ambaye alifariki dunia Novemba 28, 2023 wilayani Mwanga baada ya gari alilokuwa akiendesha akitokea mkoani Morogoro kwenye ‘send-off’ yake kugongana na lori lililokuwa likitokea Arusha.

Bibi harusi huyo pamoja na mama yake watazikwa Jumamosi, Desemba 2, 2023 ambayo ilikuwa ndiyo siku yao ya harusi, nyumbani kwao Kijiji cha Nganyeni, kata ya Mwika Kaskazini, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.

Katika ajali hiyo Rehema (marehemu) alifariki dunia pamoja mama yake mzazi, Agness Chao (75) na mfanyakazi wa ndani wa mdogo wake, Irene Shija (15) baada ya gari walilokuwa wanasafaria aina ya Toyota Raum kugongana na lori wakati wakijaribu kukwepa shimo katika eneo la Kichwa cha Ng'ombe, wilayani humo.

Akizungumza kaka wa bwana harusi mtarajiwa, Edward Mollel amesema harusi ilikuwa ifungwe katika usharika wa Oldonyosambo mkoani Arusha Desemba 2, 2023 na walikuwa wameshafanya maandalizi yote ya harusi.

"Tayari maandalizi yote yalishakamilika, ikiwemo kulipia ukumbi pamoja na vyakula, kifupi ni kwamba maandalizi yote yalishakamilika na kilichokuwa kikisubiriwa ni shughuli yenyewe,”amesema.

Amesema harusi hiyo ilikuwa igharimu zaidi ya Sh10 milioni na msiba huo umewaumiza sana kama familia na sasa kinachoendelea ni maandalizi ya mazishi.

Given Chao ambaye ni pacha wa marehemu (Rehema) amesema kwa sasa maandalizi ya mazishi yanaendelea nyumbani ambako yatafanyika na tayari makaburi yameanza kujengewa kwa ajili ya kuwapunzisha mama na pacha wake Desemba 2, 2023.

"Maandalizi ya msiba yanaendelea kama mnavyoona hapa na kesho ijumaa saa saba tutaenda Mwanga katika kituo cha Afya Kisangara kwa ajili ya kuichukua miili na  kuileta hapa nyumbani kwa maandalizi ya mazishi ambayo yatafanyika Desemba 2, 2023," amesema.

Bibi harusi huyo ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Sua, mkoani Morogoro alifanyiwa ‘send-off’ ‘ katika ukumbi wa Glonency na baada ya sherehe hizo alianza safari kuelekea nyumbani kwao Marangu Moshi akiwa ameambatana na familia yake, kwa ajili ya maandalizi ya harusi yake ambayo ingefanyika, Desemba 2 mkoani Arusha.

Jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba wanamshikilia dereva wa lori, Joachim Meela (37) kwa mahojiano zaidi.

Akizungumzia ajali hiyo jana, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Abdallah Mwaipaya aliwataja majeruhi kuwa ni Veronika Chao (35) mdogo wake na bibi harusi ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Nguzo Mbili Geita na mwanaye, Jayden Erasto (2).

"Jana kulitokea ajali mbaya katika wilaya yetu ya Mwanga, ambapo ilisababishwa na magari mawili, lori aina ya Scania, iliyokuwa ikiendeshwa na mkazi wa Moshi ikitokea Arusha kwenda Dar es salam na iligongana na gari aina ya Toyota Raum ikitokea Morogoro kwenda Marangu, ambayo ilikuwa ikiendeshwa na bibi harusi huyo.

"Chanzo cha ajali ni dereva aliyekuwa anaendesha gari aina ya Raum (ambaye ni bibi harusi) akitokea Morogoro kuja Marangu, ambapo wakati anakwepa shimo alikuwa mwendokasi na aliingia kwenye gari kubwa (lori) ambalo lilikuwa linatokea Arusha," amesema.

Akizungumzia hali za majeruhi wa ajali hiyo, Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya KCMC, Gabriel Chisseo alisema jana majeruhi hao walipofikishwa hosplitalini hapo wakitokea kituo cha afya Kisangara, walifanyiwa matibabu na baada ya hali zao kuimarika waliruhusiwa kwenda nyumbani.

"Majeruhi hawa walifikishwa jana hapa KCMC wakitokea Kisangara na walipofika hapa walifanyiwa matibabu na afya zao zilionekana kuimarika na waliruhusiwa jana," amesema Chisseo