Asilimia 12 ya Watanzania wana maradhi ya pumu

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Pumu unakuwa ugonjwa wa pili kuwaathiri zaidi Watanzania baada ya shinikizo la juu la damu linaloathiri asilimia 26 ya watu wazima.

Dar es Salaam. Zaidi ya Watanzania 7,200,000, sawa na asilimia 12, wanaugua ugonjwa wa pumu unaoathiri mfumo wa upumuaji, huku wengi wao wakiwa ni watoto walio chini ya umri wa miaka 16, Wizara ya Afya imebainisha.

Pumu unakuwa ugonjwa wa pili kuwaathiri zaidi Watanzania baada ya shinikizo la juu la damu linaloathiri asilimia 26 ya watu wazima.

Akizungumza Februari mwaka huu, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema pumu ni miongoni mwa magonjwa ya mfumo wa upumuaji, ambayo kwa takwimu za mwaka 2013, maambukizi yaliongoza kuwaathiri Watanzania 4,901,844, sawa na asilimia 18.9.

Daktari bingwa wa mapafu na mfumo wa upumuaji kutoka Wizara ya Afya, Dk Mwanaada Kilima amesema mikakati na jitihada mbalimbali zinafanyika na watafiti, wakiwemo kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi Muhimbili (Muhas), watoa tiba, ikiwemo hospitali ya Taifa na wadau wengine kujua ukubwa wa tatizo.

“Haya ni magonjwa sugu, siyo ya kuambukiza, ni ngumu kusema watu wameongezeka au wamepungua, hivyo makadirio haya ni kwa ujumla ya waathirika nchini. Tofauti ni ndogo kwa mwaka jana na mwaka huu,” amebainisha.

Mtaalamu wa Magonjwa ya binadamu, Dk Mugisha Nkoronko amesema ugonjwa huo hauambukizi, bali mtu anarithi vinasaba vinavyochochea uzalishaji wa kemikali mwilini na hatimaye kusababisha mishipa kusinyaa.

Ameshauri kuwa  mtu anayeishi na ugonjwa huo anapaswa kuwa msafi, kuepuka marashi, kutembea na dawa itakayomsaidia kupumua akibanwa na kifua.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mfumo wa upumuaji, Elisha Osati amesema kuna uwezekano wa mtu kupata pumu ukubwani, japokuwa mtu anapata zaidi ugonjwa huo akiwa mtoto.

Amesema kwenye familia baba au mama wakiwa na pumu, mtoto anaweza kupata mara tatu hadi sita, hivyo familia inasababisha zaidi. “Mtoto na mtu mzima mwenye uzito kupindukia wanahusianishwa na pumu, uvutaji wa sigara, shisha pia ni visababishi kwa hivi sasa,” amebainisha.

Amesema namna ya kukinga ni kujizuia kutumia vitu hivyo na kupunguza uzito, kutunza mazingira, ikiwemo ya kufanyia kazi, kusafisha nyumba, mazulia na kwenda hospitali kupata dawa na ushauri wa daktari.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu mwamko wa uelewa wa Watanzania juu ya ugonjwa huo, Dk Kilima amesema, “uelewa wa wananchi unaongezeka kutokana na utandawazi, pamoja na elimu tunayoendelea kuitoa, hususan kitengo cha elimu cha Wizara ya Afya pamoja na madaktari na watoa huduma.

“Ndiyo maana sasa hivi ugonjwa huu unaonekana wa kawaida na wananchi wanajitokeza kupata huduma tofauti na awali. Elimu bado inahitajika, japokuwa mwamko upo ukilinganisha na miaka ya nyuma,” amesema Dk Kilima.

Katika kukabiliana na ugonjwa huo, amesema moja ya hatua inayochukuliwa na Wizara ya Afya ni kuanzisha jarida rasmi la pumu, ambalo litakuwepo katika ngazi zote za utoaji huduma, kuanzia zahanati hadi Hospitali za Taifa.

Dk Kilima amesema jarida hilo, litawezesha kupata takwimu na kukusanya taarifa za ugonjwa huo ambao kwa kawaida ni wa kurithi.

Kuhusu pumu

Pumu ni ugonjwa sugu wa mapafu unaoathiri watu wa rika zote. Dalili zinaweza kujumuisha kukohoa, kupumua kwa shida, upungufu wa pumzi na kubana kwa kifua.

Ingawa pumu mara nyingi huanza utotoni, inaweza kuendelea katika umri wowote. Watu wengine ambao hawakuwa na shida za kupumua hapo awali, wanaweza kupata dalili za pumu kupitia vichochezi kama vile mizio, maambukizi au sababu za mazingira.

Kuhusu utambuzi wa pumu, Daktari Ezekiel Mugini amesema ugonjwa huo unatambulika mtoto anapofikisha miaka miwili, ni ngumu kuthibitisha ikiwa yupo chini ya umri huo.

Dk Mugini amesema dawa za pumu zinasaidia kutanua njia za hewa, ili mgonjwa aweze kupumua vizuri ambazo zinategemeana na kiwango cha ubanwaji wake.