Asilimia 79 ya wanawake wanasiasa wamedhalilishwa mitandaoni

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Dk Rose Reuben (kulia) akisoma tamko la chama hicho mbele ya waandishi wa habari.

Muktasari:

  • Udhalilishaji huo ni pamoja na ukiukwaji wa faragha za mtu, kuchafua sifa ya mtu, vitisho na vurugu za moja kwa moja, maneno na lugha ya kuudhi.

Dar es Salaam. Utafiti umebaini asilimia 79 ya wanasiasa wanawake wanaotumia mitandao ya kijamii nchini Tanzania walidhalilishwa kwa kufanyiwa ukatili wa kijinsia wa aina mbalimbali kupitia mitandao yao ya kijamii.

Udhalilishaji huo ni pamoja na ukiukwaji wa faragha za mtu, kuchafua sifa ya mtu, vitisho na vurugu za moja kwa moja, maneno na lugha ya kuudhi.

Kutokana na hilo, asilimia zaidi ya 70 waliacha kabisa kuitumia mitandao hiyo.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Aprili 25, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Dk Rose Reuben, katika mkutano wa siku mbili wa chama hicho ulioanza leo jijini Dar es Saalam.

Katika mkutano huo pamoja na mambo mengine, Tamwa imejadili hali na mwenendo wa watumiaji wa mitandao ya kijamii na nafasi ya mwanamke.

Dk Rose amesema utafiti huo waliufanya kwa kushirikiana na Taasisi ya Tech & Media Convergency kupitia programu ya Women at Web.

 “Hivi karibuni Bunge lilipitisha Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ambayo inakwenda kusimamia ulinzi wa taarifa binafsi, hivyo tunatarajia sheria hii itatatua baadhi ya udhalilishaji na ukatili dhidi ya wanawake kwani kusainiwa kwake hakukuja kwa bahati nasibu bali ni maamuzi yaliyoanzia ngazi ya kikanda kwa maana nchi wanachama wa Kusini mwa Afrika ziliadhimia kwa pamoja wanachama wake, kupitisha sheria hii,” amesema.

“Wanachama wa Tamwa, tunaamini kuwa kushughulikia unyanyasaji mtandaoni kunahitaji mikakati ya pamoja kati ya jamii na Serikali inayoweka mifumo ya usalama, kampuni za mawasiliano, mashirika ya kiraia na vyombo vya habari,” amesema Dk Rose.

Akieleza kuhusu madhara ya vitendo hivyo, amesema unyanyasaji mitandaoni si tu unakiuka haki za kimsingi za binadamu na kuharibu utu na usalama wao, lakini pia unazuia juhudi za wanawake kushiriki kikamilifu katika mazungumzo ya umma, kitaaluma, na mwingiliano wa kijamii.

“Udhalilishaji kwa njia ya mtandao unawajengea wanawake mazingira ya woga na kuamua kunyamaza, kuwazuia wanawake kujieleza kwa uhuru na kushindwa kutekeleza kile wanachokitamani kutokana na woga, wakihofia kudhalilika zaidi,” amesema.

Kutokana na vitendo hivyo, Tamwa kimeitaka Serikali kusimamia sheria za ulinzi na usalama mitandaoni ili kuwa na Taifa linaloheshimu utu, utamaduni na nidhamu ya mtu mmoja mmoja.

Kwa upande wa kampuni za teknolojia, amesema zina wajibu wa kufuatilia na kupunguza matukio ya udhalilishaji na unyanyasaji mtandaoni kwa kutumia mifumo yao kwa umakini ikiwemo kuendana na mifumo na misingi ya utamaduni wa Mtanzania.

Suzan Lymo, mwanasiasa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amewataka wanawake wasikate tamaa kwa yanayoendelea kwenye mitandao juu yao.

Kwa upande wake Mariam Mtemvu, diwani wa Viti Maalumu amekiri kuwepo kwa uzalilishaji huo, akishauri wanawake wanasiasa au wanaotaka kuingia kwenye siasa kuishi katika maadili kwa kuwa wameshakuwa kioo cha jamii.