Matukio udhalilishaji yaongezeka asilimia 26 Zanzibar
Muktasari:
- Katika matukio hayo, watoto wameonekana kuwa waathirika zaidi kwa asilimia 78.9 wakifuatiwa na wanawake kwa asilimia 16.1 na wanaume asilimia 5.0.
Unguja. Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar imesema kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia visiwani Zanzibar, ambapo matukio 199 yameripotiwa kwa Oktoba 2023 sawa na ongezeko la asilimia 26.8 ikilinganishwa na Septemba.
Katika matukio hayo, watoto wameonekana kuwa waathirika zaidi kwa asilimia 78.9 wakifuatiwa na wanawake kwa asilimia 16.1 na wanaume asilimia 5.0.
Akitoa takwimu hizo leo Novemba 21 mjini Unguja, Mtakwimu kutoka Divisheni ya Jinsia na ajira katika Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Ramla Hassana Pandu amesema idadi ya matukio hayo 199 ni ongezeka la asilimia 26.8 kutoka matukio 157 yaliyoripotiwa Septemba, 2023.
Akitoa mlinganisho wa makosa hayo kwa wa Septemba na Oktoba 2023, Ramla alisema matukio ya kubaka kwa Septemba yalikua 59 na Oktoba yamefikia 89 sawa na ongezeka la makosa 30.
“Makosa ya kulawiti na kunajisi Septemba yalikua 15, Oktoba ni 22, makosa ya kuingiliwa kinyume na maumbile, Septemba yalikua sita na Oktoba ni 13, kutorosha Septemba yalikuwa makosa 11 na Oktoba ni makosa 10,” amesema Ramla.
Ametaja pia makosa ya shambulio la aibu au kukashifu akisema kwa Septemba yalikua 24 Oktoba makosa 22, huku upande wa makosa ya shambulio kwa Septemba yalikua 42 na Oktoba yameongezeka kufikia 43.
“Idadi hiyo ya matukio ya Oktoba mwaka huu, yameongezeka kwa asilimia 21.3 kutoka matukio 164 yaliyoripotiwa Oktoba mwaka 2022,” amesema.
Akitaja hatua zilizochukuliwa, Ramla amesema kati ya matukio yote 199, matukio 139 yapo chini ya upelelezi wa Jeshi la Polisi sawa na asilimia 69.9, matukio 57 sawa asilimia 28.6 yapo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na matukio matatu sawa na asilimia 1.5 yapo Mahakamani.
Amezitaja Wilaya za Mjini na Magharibi B kwamba ndizo vinara kwa matukio ya udhalilishaji na ukatili ikilinganishwa na wilaya zingine kwa matukio 52 sawa na asilimia 26.1 kwa kila wilaya, ikifuatiwa na Wilaya ya Magharibi A yenye matukio 37 sawa na asilimia 18.6.
Ametaja pia Wilaya za Micheweni na Mkoani zilizoripotiwa kuwa na idadi ndogo ya matukio ya udhalilishaji kwa kuwa na matukio matatu kila moja sawa na asilimia 1. 5.
“Wilaya ya Mjini imeripotiwa kuwa na idadi kubwa ya matukio ya kubaka ikilinganishwa na wilaya nyingine kwa matukio 22 sawa na asilimia 24.7 kati ya matukioa yote ya kubaka yaliyoripotiwa, ikifuatiwa na Wilaya ya Magharibi B kwa matukio ya ubakaji 19 sawa na asilimia 21.3,’ amesema.
Amesema miongoni mwa matukio 89 ya ubakaji yaliyoripotiwa kwa Oktoba 2023, matukio 15 sawa na asilimia 16.9 yameripotiwa kwa wanawake na matukio 74 yameripotiwa kwa wasichana sawa na asilimia 83.1
Akizungumzia ongezeko hilo, mwanaharakati wa haki za binadamu visiwabi humo, Jasmin Khamis ametaja changamoto ya hatua zinazochukuliwa, akisema hazina ufanisi.
“Kuna sheria ya udhalilishaji ilianzishwa lakini sheria hii inaangalia upande mmoja, ila wapo wengine hawaoni shida maana wanajua hata wakikutwa sheria haiwagusi,” amesema mwanaharakati