Wataalamu kujifungia Arusha kutafuta mwarobaini wa ukatili
Muktasari:
- Zaidi ya Wataalamu wa maendeleo ya jamii 1,500 nchini wanatarajia kukutana jijini Arusha kujadili chanzo na kusaka suluhu ya mmomonyoko wa maadili unaopelekea matukio ya ukatili hasa mauaji, ubakaji, ulawiti, na vipigo.
Arusha. Zaidi ya Wataalamu wa maendeleo ya jamii 1,500 nchini wanatarajia kukutana jijini Arusha kujadili chanzo na kusaka suluhu ya mmomonyoko wa maadili unaopelekea matukio ya ukatili hasa mauaji, ubakaji, ulawiti, na vipigo.
Kongamano hilo la tano kwa kila mwaka, litafanyika kwa siku tatu kuanza kesho Novemba 20 hadi 22, 2023 mkoani Arusha na kuwakutanisha wataalamu hao wa maendeleo ya jamii kutoka taasisi na mashirika ya umma na binafsi kote nchini.
Wataalamu hao watakutana kwa malengo matatu ikiwemo la kujadili usalama wa jamii dhidi ya matukio ya ukatili na kuweka mipango ya kukabiliana nayo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 19, 2023 jijini Arusha, Rais wa Chama cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania, (Codepata), Angela Mvaa alisema kuwa mbali na kujadili usalama wa jamii pia wanatarajia kujadiliana changamoto za utekelezaji wa majukumu yao katika kuifanikisha jamii kuwa salama
"Moja ya changamoto kubwa katika jamii yetu kwa sasa ni mmomonyoko mkubwa wa maadili unaopelekea vitendo vya ukatili hivyo kupitia kongamano hili tunatarajia pia kuweka mipango sahihi ambayo tutahakikisha tunaipeleka kwa jamii na kila mmoja wetu atatekeleza kulingana na jamii yake,"amesema.
Amesema katika mpango huo watakaoujadili na kuupitisha utawaingiza katika kibarua cha kuelimisha jamii upya jinsi ya kupambana na matukio hayo, kufahamu viasharia na jinsi ya kumtetea anaekumbana na ukatili na jinsi ya kumsaidia kisaikolojia kurudi katika hali yake dhidi ya kisasi au msongo wa mawazo kwa kushirikiana na taasisi mbali mbali.
Kwa upande wake katibu wa Codepata , Daniel Wambura amesema kongamano hilo litaenda sambamba na maadhimisha ya miaka 60 ya taasisi ya maendeleo ya jamii Tengeru 'TICD' pia watajadili namna bora ya kutetea taaluma yao kwa manufaa ya jamii na nchi kwa ujumla.