Askari anusurika kifo akishambuliwa na Simba

Muktasari:

  • Askari wa wanyamapori mkoani Iringa wamefanikiwa kumthibiti simba anayedaiwa kutoroka Hifadhi ya Taifa Ruaha na kuingia katika Kijiji cha Ilamba.

Iringa. Askari Muhifadhi daraja la tatu, Charles Mafuru amenusurika kifo baada ya kushambuliwa na simba dume anayedaiwa kutoroka katika Hifadhi ya Taifa Ruaha.

 Askari huyo amejeruhiwa katika Kijiji cha Ilamba wilayani Kilolo katika mapambano ya kuudhibiti simba huyo anayetajwa kula mifugo.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Kamishna Uhifadhi Msaidizi Mwandamizi wa Mamlaka ya Wanyamapori (Tawa), Joas Makwati amesema tukio hilo limetokea baada ya kundi la askari na madaktari wa wanyamapori kuona eneo la karibu yao nyasi zikitikiswa na baada ya kuangalia kwa makini waligundua simba yupo pale.

Makwati amesema waligundua kuwa simba yupo eneo hilo na ili kumdhibiti walimpiga risasi za moto jambo ambalo lilimchochea mnyama huyo na kumkimbilia Mafuru kwa kasi na kumjeruhi usoni na mkononi.

"Kutokana na ujasiri wa askari Muhifadhi daraja la tatu, Nkolo Dologo aliweza kutumia umahiri wake kwa kumpiga risasi simba huyo akiwa juu ya mwili wa askari alikuwa tayari kajeruhiwa," amesema.

Pia madaktari wa wanyama pori daraja la tatu ambao wameshiriakiana na askari kumdhibiti mnyama huyo ni Emmanuel (TAWILE), Mwakyusa, Daniel Isangya na Paul Masatu (TAWA).

Kwa upando wao Wananchi wa Kijiji cha Ilamba Wilayani Kilolo wamesema wanashukuru kwa jitihada zilizofanyika kwa ushirikiano wa askari wa wanyamapori na viongozi wa serikali kuhakikisha simba hao korofi wanapatikana ili kunusuru mali zao.

Lakini pia wameeleza hali halisi inayoendelea sasa ni

hofu kutokana na simba waliokuwa wanavamia na kula  mifugo bado hawajadhibitiwa wote.

"Sasa leo baada ya kumuona huyu simba ndio nimeamini kama kuna Simba kijijini kwetu nilikua siamini kabisa hapa tuwe makini," amesema Jofrey Ngole.

Hata hivyo Diwani wa Kata ya Dabaga Amin Tengelakwi kusema kuwa kabla ya simba kuuwawa tayari alikuwa ameua nguruwe, mbuzi na ng'ombe katika kata hiyo.

"Tunaishukuru serikali na askari wa Wanyamapori kwa juhudi zilizoonekana kwani hofu ya wananchi ilikua ni kubwa," amesema Tengelakwi.

Kamishna Makwati ametoa elimu kwamba simba aliyeuawa kuna namna tofautitofauti ambazo wanaweza kumtumia ikiwa ni pamoja na kumuweka katika sehemu sahihi zinazotambulika ikiwa ni pamoja na bustani ya Tabora, bustani ya Songea na sehemu nyinginezo.

Lakini pia Simba huyo anaweza akatumika kwa maonyeshi katika shughuli mbalimbali zinazofanyika nchini.

Makwati amewaomba wananchi kuwa watulivu na kuchukua tahadhari kwani idadi iliyokuwa ikikisiwa ni simba wawili na mpaka sasa aliyepatikana ni mmoja tu.