Askari mbaroni akidaiwa kumjeruhi mfanyakazi wa ndani

Muktasari:

  • Inadaiwa kuwa binti huyo siyo mara ya kwanza kushambuliwa na bosi wake huyo., Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njomba hivyo ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za unyanyasaji wanaowafanyiwa watumishi wa ndani bila kujali hadhi ya mtu.

Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamshikilia Bandeke Lukambingu (33) askari wa kikosi cha 514 KJ kwa tuhuma za kumpiga na kumsababishia majeraha mfanyakazi wake wa ndani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Aprili 8, 2024 na kusema mtuhumiwa huyo amekamatwa na polisi akiwa mkoani hapa.

Amesema mtuhumiwa anadaiwa kumshambulia msichana huyo (13), mkazi wa mtaa wa Kikula Halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe kwa kumpiga ngumi na buti na kumsababishia maumivu mwilini.

Sababu kubwa ya binti huyo kushambuliwa inadaiwa alishindwa kufanya kazi za nyumbani.

"Kumekuwa na dhana mtaani kwamba kwa sababu huyu ni mtumishi wa Serikali hawezi kukamatwa, mtu huyu tayari tumemkamata yupo mbaroni na taratibu za kimashtaka zinaendelea,” amesema Banga.

Amesema inadaiwa kuwa binti huyo si mara ya kwanza kushambuliwa na bosi wake huyo, hivyo ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za unyanyasaji wanaowafanyiwa watumishi wa ndani bila kujali hadhi ya mtu.

Pia, Kamanda Banga amewatoa hofu wakazi wa mtaa wa Kikula juu ya tukio hilo na kwamba jeshi hilo lipo makini na kama kuna jambo lolote linaendelea wapate ushirikiano.

Amesema anaendelea kukemea waajiri wanaowatesa wafanyakazi wa nyumbani na kuahidi kuendelea kuwachukulia hatua.

Akisimulia tukio hilo, binti huyo amedai alikuwa akiwasha moto, ndipo mtuhumiwa akachukua rungu na kumpiga nalo.

"Alikuwa ananikataza nisiseme kwa watu, lakini nilikuwa nakwenda dukani nawaambia majirani wao wakaniambia nirudi nyumbani,” ameeleza binti huyo.

Amesema hana mawasiliano ya watu wa nyumbani kwao na hawana taarifa kama kajeruhiwa na mwajiri wake.

“Nyumbani hawajui, namba za simu sina na hatuwasiliani nao,” amesema.