Askari wakumbushwa uadilifu katika kuwatumikia wananchi

Mkuu wa Mkoa Lindi, Zainabu Tareck akihutubia wananchi kwenye kikao cha ufunguzi wa jengo  la ofisi ya Uhamiaji  mkoani hapo.

Lindi. Askari wa Jeshi la Uhamiaji na vyombo  vingine  vya ulinzi nchini vimetakiwa kuwa waadilifu, waaminifu, wazalendo na watiifu kwenye watekelezaji wa majukumu yao.

 Wito huo umetolewa na mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainabu Tareck baada ya ufunguzi wa jengo la ofisi Mkoa wa Lindi jana.

"Niwaombe na kuwasihi sana askari kuwa waaminifu, waadilifu na wazalendo wa Taifa hili. Mfanye kazi kwa kuzingatia misingi ya haki na sheria, tumieni weledi wenu kuchunguza na kufuatilia kwa umakini taarifa na madai zitakazowasilishwa kwenu kwa namna mbalimbali. Kimsingi, tunatarajia kuona kuna mabadiliko makubwa katika utendaji kazi na uwajibikaji," amesema Tareck.

Amesema serikali haitarajii kusikia tuhuma inaelekezwa kwa vyombo vya ulinzi kwa kushindwa kuchukua hatua stahiki kwa wakati, kwani havitafumbiwa macho vitendo vyovyote vitakavyokosesha wananchi furaha kutokana na maamuzi yasiyo sahihi.

Tareck pia amewaomba  wananchi mkoani Lindi kutoa ushirikiano kwa vyombo  vya ulinzi na usalama ili nchi iendelee kuwa amani na utulivu.

Akimwakilisha Kamishna Mkuu wa Jeshi Uhamiaji, Dk Anna Makakala, Kamishna msaidizi Novaita Edmund Mrosso  amesema jengo hilo lilianza kujengwa katika Mwaka wa Fedha 2012/2013   kwa Gharama ya  Sh2 bilioni.

Mrosso amesema katika kuhakikisha kuwa nchi  inaendelea kuwa na Amani, Jeshi la Uhamiaji ufanya   doria, misako na oparesheni mbalimbali dhidi ya wahamiaji haramu ambapo kuanzia Machi 2021 hadi Februari 2023 jumla ya wahamiaji haramu 52,415 walikamatwa na kuchukuliwa  hatua mbalimbali za kisheria ikiwemo kufukuzwa nchini.

Amesema pamoja na mafanikio hayo, Idara inakabiliwa na changanoto mbalimbali zikiwemo za baadhi ya mikoa  na wilaya kutokuwa na Majengo ya ofisi, upungufu wa askari, uhaba na uchakavu wa vyombo vya usafiri.

Mrosso amesema  kuwa Jeshi la Uhamiaji litaendelea kufanya kazi ya kuwahudumia raia na wageni kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali.

"Nawaomba  Wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa Idara ya Uhamiaji katika mapambano dhidi ya Uhamiaji haramu." amesema Kamishina Msaidizi, Novaita Edmud Mrosso.