Askofu Kasala awataka wahudumu wa afya kubadili fikra

Muktasari:

  • Wahudumu wa afya na wanafunzi wanaosomea kada hiyo wametakiwa kubadili mtazamo na kuwekeza zaidi kwenye utafiti utakaowezesha kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Sengerema. Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Geita, Flavian Kasala amesema kuna hatari ya wahudumu wa afya kubaki nje ya mfumo kama hawatabadili mtazamo na kuwekeza zaidi kwenye utafiti utakaowezesha kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Akizungumza na wanafunzi wa taasisi ya mafunzo ya afya Sengerema leo Januari 24, Askofu Kasala amesema dunia imebadilika na mambo mengi yanafanywa kwa misingi ya Sayansi na teknolojia, hivyo kama Taifa halina budi kuendana na mabadiliko hayo.

“Kwa sasa tunahitaji watu wenye ujuzi mkubwa hospitali zetu zinavifaa vya kisasa lakini wahudumu ni walewale kama hawataongeza ujuzi walionao wanaweza kubaki nje ya mfumo,” amesema Askofu Kasala.
Askofu Kasala amesema wanafunzi hawapaswi kusubiri na kutegemea kile wanachofundishwa darasani pekee, badala yake wanapaswa kujiongeza kwa kuingia kwenye mitandao kusoma vitabu na kufanya utafiti.
Akizungumzia ujenzi wa jengo jipya la la maabara, ofisi na madarasa lililojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh955milioni, Askofu Kasala amesema jengo hilo litaongeza idadi ya kozi na kuwezesha wanafunzi kupata mazingira mazuri ya kujifunzia.
“Eleweni majengo pekee hayatoi elimu jifunzeni kwenda nyakati simu zenu badala ya kuzitumia kuchati tumieni kuperuzi jinsi dunia inavyobalikia kuendana na sayansi na teknolojia nanyi muongeze ujuzi kwa tafiti hii itawasaidia Zaidi,” amesema Askofu Kasala.
Awali mkuu wa taasisi hiyo, Dk Gerald Yubaha amesema jengo hilo lenye ghorofa tatu lilipangwa kujengwa kwa Sh 1.2bilioni lakini hadi kukamilika imegharimu Sh955.2milioni kutokana na kujenga kwa kutumia force account.
Amesema taasisi hiyo iliyoanza mwaka 1971 majengo yake mengi yamelemewa kutokana na ongezeko la wanafunzi na kuwa moja ya mikakati ni kuangalia namna ya kuongeza vyumba vya madarasa sanjari na kuongeza hadhi ya chuo kw akuwa na wataalamu wabobezi.