Askofu Kweka azikwa Uswaa alikozaliwa

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (wa pili kushoto) akiwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu (wa tatu kushoto), wakiaga  mwili wa marehemu Askofu mstaafu Dk Erasto Kweka, katika ibada iliyofanyika Usharika wa Uswa Machame, Kilimanjaro leo Jumatano Desemba 6, 2023. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

  • Dk Kweka ambaye alifariki Novemba 25, 2023, katika taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu, amezikwa leo, Desemba 6, 2023, mbele ya lango kuu la kuingia kanisa la Uswaa, ambapo ni kanisa la kijijini kwao alikozaliwa.

Hai. Hatimaye Mwili wa Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Erasto Kweka (89) umezikwa katika Usharika wa Uswaa, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Dk Kweka ambaye alifariki Novemba 25, 2023, katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu, amezikwa leo, Desemba 6, 2023, mbele ya lango kuu la kuingia katika usharika huo ambapo kuna kanisa la kijiji alichozaliwa.

Ibada hiyo ya maziko imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini kutoka ndani na nje ya nchi, vongozi wa kisiasa na Serikali.

Akizungumza katika ibada hiyo ya maziko, Askofu wa Dayosisi ya Maskariki na Pwani ambaye pia ni Mkuu wa KKKT mteule, Dk Alex Malasusa amesema enzi za uhai wake, Dk Kweka amefanya mambo mengi na kwamba kaacha historia ambayo haitafutika katika kanisa hilo.

"Tunaendelea kumshukuru Mungu kwa ajili ya mambo mengi mema ambayo amefanya baba yetu, hakuwa na upendeleo, alijua ametumwa na huyu Yesu kuja kufundisha watu, hakujali gharama, hakika tutaendelea kuyaenzi," amesema Malasusa.

Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amesema Dk Kweka atakumbukwa kwa mambo mengi aliyoyafanya katika kanisa na Taifa ikiwemo uchapaji kazi na misimamo yake katika kupigania maendeleo.

"Tumejifunza Dk Kweka alikuwa mchapakazi na kwenye kazi hakuwa na visingizio, tumeambiwa suala la wachungaji wanawake lilikuwa ni moja ya mambo aliyoyaasisi, hivyo alishaona nguvu ya wanawake katika uongozi," amesema Silaa.

"Leo Taifa letu linapoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, naamini ni moja kati ya maono na vitu vinavyoishi ambavyo Dk Kweka aliviasisi, niombe kanisa kuendelea kumuombea Rais katika kazi anayofanya ya kuongoza Taifa letu na kuendelea kuliombea Taifa liendelee kuimarika kiuchumi na kijamii ili liendelee kustawi". Amesema

Dk Kweka amekuwa kiongozi wa Dayosisi ya Kaskazini tangu mwaka 1976 mpaka 2004 alipostaafu na kwa mujibu wa historia,  alikuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu kwa muda mrefu na ametibiwa katika hospitali mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Novemba 7, 2023 akiwa nyumbani kwake hali yake ilibadilika ghafla, akapelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambapo baada ya matibabu ya kina alipewa rufaa ya kwenda JKCI na Novemba 25 saa 4:00 asubuhi alifariki dunia.