Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wenza wa viongozi wa dini wahamasishwa kuwania uongozi

Maaskofu wakiaga mwili wa marehemu, Askofu Mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk Erasto Kweka katika ibada iliyofanyika katika Kanisa Kuu la KKKT Dayosisi ya mashariki na Pwani (DMP) Azania Front jijiji Dar es Salaam Novemba 29, 2023. Picha Sunday George.

Muktasari:

  • Dk Erasto Kweka alikuwa kiongozi wa Dayosisi ya Kaskazini mwaka 1976 hadi 2004 alipostaafu.

Hai. Mbunge wa Viti Maalumu, Shally Raymond, amewashauri wenza wa maaskofu na wachungaji kuchukua fomu kuwania uongozi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka 2024.

Shally ametoa  rai hiyo leo Desemba 6, 2023 alipopewa nafasi ya kutoa salamu wakati wa ibada ya mazishi ya Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Erasto Kweka.

Ibada hiyo imefanyika katika usharika wa Uswaa na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji, wakiwamo viongozi wa dini, kisiasa na Serikali.

Shally amesema wenza wa maaskofu na wachungaji wana uwezo wa uongozi, hivyo wakipata nafasi wanaweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii na Taifa kwa ujumla.

"Mwakani kuna uchaguzi wa Serikali za mitaa, niwaombe baba zangu maaskofu na wachungaji, mimi nafahamu wenza wenu wana uwezo mkubwa wa uongozi na hakuna mahali pameandikwa ukiwa mwenza wa askofu, mchungaji au kiongozi wa dini usichukue fomu ya kugombea uchaguzi wa Serikali za mitaa au nafasi nyingine za kisiasa," amesema.

Shally amesema, "Niwaombe uchaguzi unaokuja ni muhimu sana, kinamama tuchukue nafasi. Mama akiwa kiongozi anaweza kuleta mabadiliko na haitoshi tu kuwa kiongozi kwenye kanisa, anaweza pia kuwa kiongozi serikalini na hata kuwa  mbunge.

Amesema Dk Kweka enzi za uhai wake alipenda wanawake na aliamini wanaweza, akisisitiza wapatiwe elimu.

"Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya Dk Kweka ambaye alitujali na kutupenda wengi, baba alitupenda wanawake na alitaka watoto wa kike wasome.  Alituona tunaweza.

“Kwa mabinti wote waliopo hapa wazingatie masomo na tukumbuke baba alisema kitabu hakipendani na kinywaji na ameondoka bila kuvunja msimamo, hakupenda watu kunywa pombe hovyo,”amesema Shally.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amesema Kanisa na Taifa limepoteza nguvu kubwa ya mshauri na shujaa.

"Nitapoteza muda kueleza sifa za mzee huyu ila tutambue tulikuwa na shujaa na tuna sababu ya kumshukuru Mungu kwa maisha ya baba yetu, kwani alikuwa wa baraka na kila jambo jema la kuigwa, ni mtu mwema,” amesema Mbowe.

Dk Kweka alikuwa kiongozi wa Dayosisi ya Kaskazini mwaka 1976 hadi 2004 alipostaafu.

Amefariki dunia, Novemba 25, 2023, akipatiwa matibabu katika taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Maziko yanafanyika leo Desemba 6, 2023 katika Usharika wa Uswaa wilayani  Hai, mkoani Kilimanjaro.

Inaelezwa Askofu Kweka alikuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu kwa muda mrefu. Ametibiwa katika hospitali mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Novemba 7, 2023 akiwa nyumbani kwake hali ilibadilika ghafla, akapelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kabla ya kupewa rufaa ya kwenda JKCI. Alifariki dunia Novemba 25,2023 saa nne asubuhi.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria maziko ni Waziri wa Ardhi, Jerry Silaa anayeiwakilisha Serikali.

Wengine ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi.