Askofu Mwagala alivyosimikwa, Biteko ataka uchaguzi usiwagawe wananchi

Dk Biteko ameyasema hayo leo Jumanne Machi 19, 2024 katika Misa Takatifu ya kuwekwa Wakfu na Kusimikwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mafinga, Mhashamu Vincent Mwagala.
Pia, amesisitiza Watanzania waepuke kuchaguana kwa misingi ya ukabila, dini au mahali walikotoka bali wazingatie misingi ya kuleta matokeo.
“Tujue kinachotuunganisha ni Utanzania wetu, tuchaguane kwa amani tuweze kuleta maendeleo kwenye nchi yetu,”amesema Dk Biteko.
Naibu Waziri Mkuu huyo aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo akimuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ya dini kuwaletea Watanzania maendeleo.
“Watanzania wanataka maendeleo, wanahitaji shule nzuri, zahanati, vituo vya afya, barabara, umeme, tena sio tu umeme, ila umeme wa uhakika, wanahitaji kuona mtoto anayezaliwa anasoma katika mazingira rahisi na kupata elimu bora,” amesema Dk Biteko.
Pia, amesema Rais amemuagiza amwambie Askofu Mwagala kwamba, Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa Katoliki na madhehebu mengine kuiletea nchi maendeleo ya uhakika.
Katika hotuba yake, Dk Biteko aliyegusia msemo wa Kiswahili wa, ‘mwanzo mgumu’ amemwambia Askofu Mwagala kuwa ameanza kuongoza jimbo hilo jipya, atakutana na milima na mabonde wakati wa kulijenga.
“Watatokea wa kukuvunja moyo usiwasikilize, wengine watasema wanajua kuliko wewe wasikilize, kwa sababu hata saa mbovu kuna wakati inakuwa nzima, wape sikio lako, lakini kamwe wasikuondoe kwenye uchungaji wako,” amesema Dk Biteko.
Amesema tukio la kusimikiwa kwa askofu huyo lina baraka za Mungu huku akifafanua kwamba hata kanisani huwa kuna waumini waliogawanyika kwenye makundi.
“Wapo wanaopenda mahubiri, yakimalizika wanatamani kutoka, wapo wachache wanapenda kipindi cha sadaka kikiisha wanatoka japo hawa huwa ni wachache, ila wapo wale wanaosubiri Askofu aseme nendeni na amani, lakini leo (jana) hata hawa wa nendeni na amani naona bado wapo, wamevumilia hii ni ishara kwamba tukio hili lina baraka za Mwenyezi Mungu,” amesema Dk Biteko.
Akizungumzia suala la mazingira, Dk Biteko amesema Mafinga ipo kwenye eneo zuri kijiografia na ina mandhari nzuri maana yake mazingira yanatunzwa.
“Haya mazingira tunayoishi tunayatawala kwa sababu Mungu ametupa akili ya kuyatawala, hivyo tuyatunze, tuyahifadhi ili yaweze kutulinda na sisi.
“Mmeona hivi karibuni tulipata mtikisiko kutokana na mgao wa umeme, kwa sababu vyanzo vya maji vilikauka, tuna mradi wa Bwawa la Nyerere urefu wake ni kilomita 100 na upana ni kilomita 25, lile sio bwawa ni ziwa, maji yaliyopo pale yanategemea utunzaji wa mazingira,” amesema Dk Biteko.
Akizungumzia miaka mitatu ya Rais Samia madarakani, Dk Biteko amesema Rais aliipokea nchi ikiwa katikati ya majonzi makubwa, ikiwa imempoteza Rais wake wa Dk John Magufuli.
“Nchi ilikuwa katika shaka ni nani anaweza kutupeleka mbele, miradi yote iliyoanzishwa wengine walikuwa na shaka, alipoingia ofisini kauli mbiu yake ilikuwa ni Kazi iendelee; na kweli ameendelea kutekeleza miradi ile na mingine mipya kwa kasi kubwa akisimama katika kauli yake,” amesema Dk Biteko.
Hivyo, amewaomba viongozi wa dini na Watanzania kuendelea kuiombea nchi na Rais huku akiwaasa waumini wa Mafinga kupendana, kuvumiliana na kustahimiliana huku akiwasisitiza changamoto watakazokutana nazo watafute suluhu badala ya kumtafuta mtu.
Katika Misa Takatifu hiyo, iliyoongozwa na Kardinali Protase Rugambwa na Askofu Mkuu, Angelo Accattino ambaye ni Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania, Askofu Mwagala amewaomba waumini wote kumuombea huku wakitambua kuwa mtoto mchanga anahitaji uangalizi wa pekee.
“Naombeni mniombee kwa namna ya pekee mimi mtumishi wenu, wanasema kobe ukimkuta juu ya mti ni lazima amepandishwa, mimi kama kobe nimepandishwa, ili niendelee kubaki lazima mnishikilie,” amesema Mwagala.
Naye Askofu Mkuu, Angelo Accattino amewashukuru watu wa Mafinga huku akiwasisitiza kutunza mazingira kwa sababu Mungu amewapa ardhi nzuri wanayopaswa kuitunza vema kwa maendeleo yao na Taifa.
Mchakato wa kumpata askofu
Januari 25 kwenye hafla ya kusimikwa kwa Askofu wa Jimbo la Bukoba, Jovitus Mwijage, Monsiyori David Mubirigi alielezea mchakato wa namna ya kumpata Askofu, akisema huanza kwa askofu wa jimbo.
Alisema kila baada ya miaka mitatu huwa anatuma orodha ya majina ya mapadri watatu anaoona wanastahili kuwa maaskofu.
Mubirigi alisema hiyo orodha inaweza kubadilishwa kulingana na hali za mapadri waliochaguliwa.
“Huenda kuna padri akawa mgonjwa, amechoka au amezeeka kwa sababu hiyo orodha inaweza kubadilishwa,”alisema Mubirigi.
“Inapofika wakati askofu anahitajika, inaangaliwa orodha ya mapadri waliotumwa kama wanafaa, Roma haina haraka, kanisa halina haraka ndiyo maana majimbo mengine wanamaliza miaka hadi mitano bila kuwa na askofu.”
Alisema orodha ya majimbo ambayo yako wazi hayana maaskofu huwa inapelekwa Roma, wanafanya mchakato wa kina na si lazima ateuliwe padri kutoka jimbo husika, bali huangaliwa pia hata wa jimbo lingine akateuliwa kwenda kuongoza jimbo linalotakiwa kuwa na askofu kwa muda huo.
“Katika mchakato wa kumpata askofu wanahojiwa maaskofu, mapadri na hata waumini kisha ripoti inarudi kwa Monsiyori anayeituma Roma,” alisema.
Pia, alisema katika ripoti hiyo, kunakuwa na majina matatu yanayowasilishwa kwa Baba Mtakatifu ambaye huyaweka kwenye maombi kwa siku nzima, hapo ndipo anapoangaziwa Roho Mtakatifu anayemuonyesha mmoja kati ya watatu walio kwenye orodha.
Sifa za askofu ni pamoja na imani thabiti, maadili, bidii, busara, fadhila, vipaji, umri kuanzia miaka 35 na kisomo katika chuo kikuu.