Askofu: Wazazi msiwafiche watoto wenye changamoto za ukuaji

Mtaalamu wa mbolea kutoka Kampuni ya Agrami, Ndebemeye Rwikima (mwenye flana ya kijani) akionyesha bustani tiba na  namna anavyotumia mbolea ya kisasa kupandia mazao. Bustani hiyo ipo katika kituo cha kulea watoto cha Huduma ya Utengamani cha Antonia Verna kilichopo Kawe. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:


  • Askofu Msaidizi Henry Mchamungu wa Jimbo Kuu la Katoliki Dar es Salaam amewahimiza wazazi kuwapeleka shuleni au katika vituo vya kulelea watoto watoto wenye changamoto za ukuaji.

 Dar es Salaam. Wazazi wenye watoto wenye changamoto ya ukuaji wa kiakili na kimwili wametakiwa kutowaficha ndani watoto hao na badala yake kuwapeleka shule, ili wapate elimu au katika vituo vya kulelea watoto.

 Kauli hiyo imetolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Katoliki Dar es Saam, Henry Mchamungu  wakati wa  uzinduzi wa bustani tiba katika kituo cha kulea watoto cha Huduma ya Utengamano cha Antonia Verna, kilichopo Kawe.

Amesema watoto wana utajiri mkubwa, hivyo jamii ina wajibu wa kuwasaidia na kuwalea vyema.

“Jamii imekuwa ikiwaficha wasionekani, lakini kumbe ndani wana utajiri mkubwa, wakitoka nje na kufundishwa na kushirikiana na wengine wataleta furaha ambayo ulimwengu unaitafuta katika fedha na mambo mengine.

"Nimefurahia bustani tiba, mtoto atafundishwa namna ya kulima mbogamboga ambayo itamfanya viungo vyake kugusana na udongo na mimea, hivyo kuchangamsha hisia na kupunguza shinikizo la damu," amesema Askofu Mchamungu.

Awali, Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma ya Utengamano cha Antonia Verna, kilichopo chini ya shirika la Invrea Congregation Kawe, Angela Jeremiah amesema  mpaka sasa kituo hicho kinahudumia  watoto 768 wenye ulemavu kutoka maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Amesema watoto hao hupelekwa kituoni hapo kwa ajili ya kufanyiwa mazoezi ya viungo, watu wanaowahudumia kupewa elimu namna ya kuandaa lishe kwa ajili ya watoto hao.

"Familia nyingi hazina kipato kizuri, hali inayochangia watoto hawa kukosa huduma muhimu ikiwemo matibabu, ulaji unaofaa kwa watoto wenye ulemavu" amesema sista Jeremiah.


Pia amesema moja ya changamoto inayowakabili ni kushindwa kujiendedha kutokana na asilimia kubwa ya wazazi kushindwa kuchangia huduma za chakula na matibabu ya mazoezi ya viungo.

Kwa upande wake,  Ofisa Lishe wa Manispaa ya Kinondoni, Janet Mnzava, amewashauri wazazi wenye watoto wenye changamoto ya ulemavu kuwapatia vyakula vyenye virutubisho vyote ikiwemo wanga, protini, vitamini madini  na mafuta, vihusike katika mlo wa kila siku.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni  ya Mwana wa Afrika, Rhoda Magoinga, amesema kupitia bustani hiyo, wanasafisha mazingira na kupunguza hewa ya ukaa huku wakisisitiza kuwa na kilimo mjini kwa kutumia mbolea za asili.

"Bustani kwa watot wetu katika kituo hiki itawasaidia kujfunza namna ya kulima, lakini na sisi ambao ni wasambazaji wa mbolea, tutakuwa bega kwa bega katika kuwasaidia wanawake ambao wanalea watoto wao wenye changaamoto ya ukuaji, kwa sababu tunaona wanawake wakipewa nafasi wanatenda haki," amesema Magoinga.