Ataka kutapeli kupitia mawasiliano na Rais Samia
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha akitoa taarifa ya mtu aliyetaka kutapeli kanisa Tabora akidai kawasiliana na Rais Samia.
Muktasari:
- Amejifanya kuwa amefanya mawasiliano na Rais Samia ili kusaidia kanisa Tabora.
Tabora. Jeshi la Polisi mkoani Tabora linamshikilia mtu mmoja anayedaiwa kuwa raia wa Burundi kwa tuhuma za kujaribu kulitapeli kanisa moja mjini hapa kwa kujifanya amewasiliana na Rais Samia Suluhu Hassan ili kulipatia msaada.
Akizungumza leo Mei 5, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amesema kanisa hilo lilikuwa limewahi kuandika barua kwa Rais kuomba msaada wa kukamilisha ujenzi wake.
Hata hivyo, mtuhumiwa alitumia mwanya huo kudai kuwa tayari amewasiliana na Rais kuhusu msaada huo.
“Huyu bwana ameliambia hili kanisa kwamba amewasiliana na Rais na tayari ili kuwasaidia kumalizia kanisa lao jambo ambalo siyo kweli na sidhani kama hata anajulikana wapi,” amesema.
Amesema mtuhumiwa huyo, ambaye anaishi Nairobi nchini Kenya, aliitaka kanisa hilo kutoa Sh15 milioni akidai ni sehemu ya maandalizi ya kupokea msaada mkubwa kutoka kwa Rais.
Baada ya kanisa hilo kutoa taarifa kwa vyombo vya dola, makachero wa Polisi mkoani Tabora walianza ufuatiliaji na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo katika mpaka wa Namanga alipokuwa akijaribu kuvuka kuelekea Kenya.
"Nilishasema hapa Tabora tuna Itelijensia kali sana na hakuna muhalifu atayeweza kufurukuta hapa na hata aende wapi tutamkamata tu, hatuna mzaha na vibaka au matapeli tapeli hapa ni lazima watu waishi kwa amani na utulivu," amesema.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu ili hatua zichukuliwe kwa haraka.
Aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao na kuwataka kuendelea kutoa taarifa pindi wanapobaini viashiria vya uhalifu.
Naye mchungaji wa kanisa hilo (jina limehifadhiwa), amesema walishawahi kuomba msaada kwa Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo walivutiwa na taarifa ya mtuhumiwa kabla ya kubaini kuwa ni njama za utapeli.
“Awali tulifurahi tukidhani ombi letu limejibiwa, lakini tukaanza kutilia shaka baada ya kuona mawasiliano hayakupitia kwa Mkuu wa Mkoa. Ndipo tukatoa taarifa,” amesema.
Ameongeza kuwa mwaka 2024 walishawahi kutapeliwa Sh4 milioni, jambo lililowafanya kuwa waangalifu zaidi safari hii.
Amelishukuru Jeshi la Polisi kwa hatua za haraka zilizochukuliwa na kuonya wananchi kuwa makini dhidi ya matapeli.