Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Magunia 133, ekari 68 za bangi zateketezwa Tabora

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo, akitoa taarifa kuhusu operesheni ya kukabiliana na dawa za kulevya mkoani Tabora.

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, inakadiriwa zaidi ya vijana 500,000 nchini wapo katika vituo vya tiba na urejeshaji (SOBA House) kutokana na athari za dawa za kulevya.

Tabora. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imeendesha operesheni ya siku saba katika misitu ya hifadhi ya Mto Igombe wilayani Uyui na Nyahua wilayani Sikonge mkoani Tabora, ambapo magunia 133 ya bangi pamoja na ekari 68 za mashamba ya bangi vimeteketezwa.

Akizungumza leo Aprili 30, 2026, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema operesheni hiyo ililenga kubaini na kuondoa mitandao ya kilimo cha bangi na mirungi katika maeneo ya hifadhi za misitu.

“Tumeendesha operesheni katika misitu hiyo na kubaini mashamba ya bangi na mirungi. Vimekamatwa na kuteketezwa,” alisema Lyimo.

Alisema operesheni hiyo imefanyika kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kanda ya Magharibi pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Tabora, akibainisha kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu.

Kwa mujibu wa Lyimo, katika operesheni hiyo ilibainika kuwepo kwa nyumba iliyojengwa katikati ya msitu, uharibifu mkubwa wa miti pamoja na shughuli za kilimo cha bangi na ufugaji ndani ya hifadhi.

“Kuanzia sasa, tutaendelea na operesheni endelevu kukomesha kabisa kilimo cha dawa za kulevya ambacho kimekuwa kikiathiri afya za vijana, uchumi na kusababisha changamoto za kijamii,” alisisitiza.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, aliagiza TFS kuongeza doria za mara kwa mara akisema haiwezekani uharibifu mkubwa kufanyika ndani ya misitu bila kugundulika mapema.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha

“Ni lazima doria ziimarishwe na hatua kali zichukuliwe kwa wote watakaobainika. Hatuwezi kuvumilia uharibifu huu unaowaangamiza vijana wetu,” alisema Chacha.

Alisema vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo vimeimarika na kuahidi kuwa hali ya usalama itaendelea kuboreshwa.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, inakadiriwa zaidi ya vijana 500,000 nchini wapo katika vituo vya tiba na urejeshaji (SOBA House) kutokana na athari za dawa za kulevya.