Athari vita vya Israel, Palestina zanukia

Dar es Salaam. Mapigano yanayoendelea kati ya Israel na kundi la Wanamgambo la Hamas kwa siku nane sasa, yanaweza kuiathiri Tanzania kiuchumi, hivyo wadau wameshauri Taifa kuchukua hatua za tahadhari.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa wanasema kuna uwezekano wa bei ya mafuta kupaa kwenye soko la dunia na kukosekana misaada ya maendeleo kutokana na kuhamishiwa kwa waathirika wa vita hivyo.

Kutokana na uwezekano wa hayo kutokea, walishauri Tanzania kuungana na mataifa mengine duniani kusaka suluhu ya mgogoro huo na kuimarisha usimamizi wa rasilimali fedha za ndani ili ikitokea misaada ikasitishwa, athari zisiwe kubwa zaidi nchini.

Tayari Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imetoa tamko kuhimiza pande zinazohasimiana katika vita hiyo kukaa kwenye meza ya mazungumzo kutafuta suluhu ya mgogoro kwa njia ya amani.

Kuhusu bei ya mafuta katika soko la dunia, Serikali imesema inaangalia njia za muda mfupi na mrefu kukabiliana na changamoto yoyote ya upatikanaji wa nishati hiyo.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Kamishna wa Mafuta na Gesi Asilia, Michael Mjinja alisema si tu kutokana na mgogoro wa Palestina na Israel, lakini kwa mwenendo wa siasa duniani, wanaangalia njia ambazo Tanzania itakuwa salama kwenye upatikanaji wa mafuta.

Alisema nchi zinazopigana sasa si wazalishaji wakubwa wa mafuta, lakini hofu iliyopo ni kwa nyingine zinazozalisha nishati hiyo kuingilia vita, hivyo kusababisha mtikisiko wa upatikanaji wake.

“Athari si kwenye bei pekee, bali hata kwenye upatikanaji, kwa hiyo tunaangalia njia zitakazosaidia kupata mafuta,” alisema, bila kueleza kwa undani mikakati iliyopo.

Kwa sasa bei ya petroli kwa Dar es Salaam imeongezeka kutoka Sh3,213 iliyokuwapo Septemba hadi kufikia Sh3,281 Oktoba, dizeli ilikuwa Sh3,259 Septemba na ikapanda hadi Sh3,448 Oktoba.


Maoni ya wachambuzi

Mchambuzi wa siasa za nje, Ibrahim Rabi alisema athari za mgogoro huo kwa nchi za Afrika ni kubwa ikilinganishwa na zilizotokana na ule wa Russia na Ukraine, ulioathiri nchi chache zilizotegemea ngano, mbolea na chakula kutoka mataifa hayo.

“Kadiri mgogoro unapotanuka kuwa wa kikanda na mataifa mengine kuhusika kama Syria na Lebanon, athari zitakuwa kubwa kwa sababu asilimia 80 ya mafuta tunayotumia yanapita kwenye mfereji wa Homs uliopo chini ya Iran.

“Iran imeongeza meli za ulinzi za kivita, sasa kumekuwa na hofu ya kuingia na kutoka kwa meli za mafuta, hivyo athari itakuwa kubwa endapo vita itakuwa ya kikanda,” alisema.

Rabi alisema nchi za Afrika zinapaswa kujikita kutafuta suluhu ya mgogoro huo na si kuegemea upande mmoja.

“Baadhi ya nchi za Afrika zimekuwa kama kasuku zinafuata mkumbo; nyingine zimeshatoka kwenye misingi zilizojiwekea. Zipo nchi hujiwekea misimamo baadaye hugeuka. Tukija kuleta siasa kwenye jambo hili tutakaoumia ni sisi,” alisema.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa za kimataifa, Said Msonga alisema mgogoro baina ya Israel na Hamas unavutia mataifa makubwa kushiriki, hivyo mchango wa kiuchumi ambao mataifa yaliyoendelea yalikuwa yakitoa kwa mataifa yanayoendelea, unaweza kupunguzwa na kuelekezwa kwenye mgogoro.

Ili kutokwama kwenye miradi, Msonga alisema upo umuhimu wa watu wanaopewa dhamana ya kusimamia na kuajiriwa kwenye sekta za umma, kuwa waadilifu kuwezesha fedha zinazopatikana kupitia makusanyo ya ndani, zielekezwe kufanya miradi iliyokusudiwa, ili hata athari zinapotokea, kusiwe na matatizo maklubwa yanayoweza kutokea na kuaathiri nchi.

Alisisitiza Serikali iwaongoze wananchi kuhakikisha wote waliopewa dhamana wanatekeleza majukumu yao ipasavyo ili malengo yaliyowekwa na nchi yafikiwe.

Naye Godwin Gonde, mtaalamu wa masuala ya diplomasia alisema:

“Nchi zinazochochea mgogoro huu zina masilahi, kwa hiyo Afrika ikiwamo Tanzania kuonyesha kuwaunga mkono Israel au Palestina, tutaonyesha tunakinzana na mataifa hayo au tunayaunga mkono, hii inaweza kuwekewa vikwazo.”

Gonde alisema Tanzania imeonyesha kutofungamana na upande wowote, lakini alihoji ni kwa kiasi gani itaweza kuyashawishi mataifa mengine kufuata msimamo huo.