Atupwa jela maisha kwa kumnajisi mwanafunzi wa la kwanza
Muktasari:
Kaliyango Maganga (55) anadaiwa kutenda kosa hilo na kushtakiwa Julai 30 mwaka huu, kisha kufunguliwa kesi ya jinai namba 240/2023.
Shinyanga. Mahakama ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imemuhukumu kifungo cha maisha jela mkazi wa Kijiji cha Chapulwa Kata ya Mwendakulima, Kaliyango Maganga (55) kwa kosa la kumnajisi mtoto wa darasa la kwanza (8).
Maganga anadaiwa kutenda kosa hilo na kushtakiwa Julai 30 mwaka huu, kisha kufunguliwa kesi ya jinai namba 240/2023.
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Christina Chovenye ametoa hukumu hiyo Septemba 22, 2023 ambapo amesema mshtakiwa aliyekuwa akifanya kazi ya umwagiliaji bustani ya maua nyumba ya jirani na mtoto huyo, alikuwa akimvizia wakati akienda shule na muda walezi wake wakimuacha peke yake kwenda kwenye shughuli za uchimbaji madini katika mgodi wa Mwime.
“Mtoto huyo alikuwa akiishi na walezi wake ambao ni babu na bibi walikuwa wakiondoka nakumuacha ndipo mtuhumiwa alikuwa akimchukua na kumnajisi huku akimueleza asimwambie mtu akisema atamuua,”amesema Chovenye
Hakimu Chovenye amesema licha ya vipimo vya daktari kuthibitisha, mtoto huyo pia alisikilizwa na kutoa maelezo ya kunajisiwa na mtuhumiwa mara kwa mara akidai Mahakama haikuwa na shaka lolote juu ya utoaji wa hukumu hiyo.
Hakimu Chovenye amesema walimu wa shule anayosoma mtoto huyo walitoa maelezo ya kugundua mtoto huyo kunajisiwa nakueleza kila siku amekuwa akichelewa shule na akifika anakuwa amechoka na kuwa na maumivu makali.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Evodia Baimo amesema kesi hiyo imesikilizwa mara nne tangu kufunguliwa kwa shauri hilo akidai adhabu hiyo kwa mshtakiwa iko sahihi ili iwe fundisho kwa wengine.
Akijitetea baada ya hukumu hiyo, Maganga aliomba kupunguziwa adhabu hiyo kwa madai ni mzee na anategemewa na familia.