Aweso ahoji gharama kuunganishiwa maji nchi nzima

Tuesday July 13 2021
By Janeth Joseph
By Florah Temba

Moshi. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo, Anthony Sanga kuwasiliana na  wakurugenzi wote wa mamlaka za maji  nchini ili kujua gharama halisi ya kumuunganishia mwananchi maji.

Amesema kuna watu wanaunganishiwa maji katika mtaa mmoja lakini kwa gharama tofauti jambo alilodai kuwa halikubaliki.

Ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi wa kata ya njia panda mjini mdogo wa Himo wilayani Moshi wakati akisikiliza kero mbalimbali za wananchi.

"Ipo changamoto hii kwenye mamlaka zetu za maji juu ya gharama za uunganishwaji wa maji kwa wananchi, leo mtu anataka kuunganishiwa maji mita mbili na mnaweza mkawa wote kwenye mtaa mmoja lakini kila mmoja anapewa gharama hiyo hiyo hii haiwezekani."

"Namwelekeza katibu mkuu wizara ya maji apitie wakurugenzi wote wa mamlaka za maji ili kujua gharama halisi ya kumuunganishia mwananchi maji, hili ni lazima tulizingatie hatuwezi kukubali kama wizara ," amesema Aweso.

"Tunataka gharama za uunganishwaji majumbani ziangaliwe upya ili mwisho wa siku mwananchi apunguziwe mzigo waweze kupata maji safi na salama," amesema Aweso.

Advertisement

Pamoja na mambo mengine amewataka wataalamu wa miradi kuhakikisha miradi yote iliyotolewa maelekezo inaanza mara moja ili Watanzania waweze kupata huduma ya maji safi na salama na kwamba katika kata ya njia panda Serikali imetenga Sh1.3 bilioni  kukamilisha mradi wa maji uliopo katika kata hiyo.

Mbunge wa Vunjo (CCM),Dk.Charles Kimei ameishukuru Serikali kwa jitihada inayofanya kuhakikisha wananchi wake wanaondokana na kero mbalimbali za maji.

"Naishukuru Serikali kwa kututengea bajeti nzuri ya maji ili kuhakikisha wananchi wa Vunjo wanaondokana na kero mbalimbali za maji , tunashukuru kwa kutuhakikishia kwamba kwa miezi minne wananchi wangu wanaenda kuyaona maji maana hapa njia panda changamoto na gharama za maji ni kubwa," amesema  Dk Kimei.

Advertisement