Baba adaiwa kuwanywesha sumu wanaye watatu, kisa ugomvi na mkewe

Dar es Salaam. Watoto wawili wamefariki dunia na mmoja kulazwa hospitali baada ya baba yao mkazi wa Chanika, Karim Shaaban kutuhumiwa kuwanywesha sumu kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kutokana na mgogoro wake na mkewe.

Kwa mujibu wa taarifa iliyoripotiwa na kituo cha televisheni ya Azam, mwanaume huyo aliwachukua watoto wake siku ya Sikukuu ya Idd El-Fitr na kwenda nao kwake ambako aliwapa juisi ambayo inadaiwa kuwa na sumu.

Akisimulia mkasa huo, mjomba wa mtuhumiwa, Juma Mohamed amesema mwanaume huyo alitengana na mke wake kwa sababu alikuwa akimtuhumu kwamba mtoto wao wa mwisho sio wake.

"Kabla ya tukio hili alikuwa na ugomvi na mke wakee akihisi kwamba mtoto wao wa mwisho sio wake. Alikuwa akimtishia kumuua, baada ya vitisho kuzidi mwanamke akaamua kuondoka," amesema Mohamed.

Amesimulia kwamba siku ya tukio la mauaji hayo, Shaaban aliwachukua watoto wake watatu, mmoja mwenye umri wa miaka tisa, mwingine sita na mdogo kabisa miaka mitatu.

Amesema alipofika kwake na watoto hao aliwapatia juisi baada ya muda kidogo wakazidiwa na mmoja wa miaka mitatu akafariki papo hapo.

Mohamed anasema baada ya kuona amefariki, mwanaume huyo alimchukua mtoto huyo hadi nyumbani kwa mama yake ambako watoto hao walikuwa wakiishi na kujaribu kubomoa karo la choo ili awatupie humo.

"Katika harakati za kubomoa karo, akasikika, kaka yake akatoka nje, akamkuta anahangaika kuvunja karo. Baada ya kumshitukiza akaamua mwenyewe kujitumbukiza," amesema Mohamed.

Baada ya kubaini kwamba alikwenda na mtoto mmoja, anasema ilibidi wafuatilie wale wengine, ndipo wakaenda kwake na kukuta wamezidiwa.

Amesema waliwachukua na kuwakimbiza hospitali lakini mmoja mwenye miaka sita naye akafariki. Mtoto mkubwa wa miaka tisa alikimbizwa Hospitali ya Amana na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Mloganzila kwa matibabu zaidi.

"Baada ya kuulizwa akasema lengo lake lilikuwa ni kuua familia yake na yeye mwenyewe ajimalize," amesimulia Mohamed.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili - Mloganzila, Neema Mwangomo alikiri kwamba waliwapokea mgonjwa huyo.

Vilevile, kamanda wa polisi wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba Shaaban anashikiliwa na jeshi la polisi.