'Aliyemuua' mwalimu naye ajiua mahabusu
Geita. Jeshi la Polisi mkoani Geita limethibitisha kifo cha Mwalimu Samuel Subi wa Shule ya Msingi Igaka, wilayani Geita kilichotokea machi 17 kwa kujinyonga akiwa mahabusu kwa kutumia shati alilokuwa amelivaa.
Mwalimu huyo alikuwa akishikiliwa kwa tuhuma za kumuua mwalimu mwenzake, Emanuel Chacha kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali kwenye moyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema mtuhumiwa alijinyonga usiku wa kuamkia Machi 17 akiwa akiwa chooni kwa kutumia shati alilolivaa.
“Aliingia chooni na kutumia shati alilokuwa amevaa kujinyonga. Mahabusu wenzake waligundua dakika za mwisho na kumsaidia, alipelekwa hospitali ya mkoa kwa matibabu lakini alifariki dunia,” alisema kamanda Safia.
Machi 15, saa 3:45 walimu hao wakiwa darasani walikokuwa wanatoa mtihani kwa wanafunzi wa darasa la kwanza, Mwalimu Subi alichomoa kitu chenye ncha kali na kumchoma Mwalimu Chacha hivyo kumsababishia kifo.
“Huko Kata ya Isulwabutundwe mwanamume wa miaka 35 wa Shule ya Msingi Igaka aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kwenye chembe ya moyo na mwanamume mwingine mwenye miaka 35 ambaye ni mwalimu mwenzake. Walimu wote wawili walikuwa darasani wakiandaa mtihani, ndipo mtuhumiwa alitoa kisu na kumchoma mwenzake kwenye chembe cha moyo,” ilisema taarifa ya polisi kuhusu kifo hicho.
Sababu za mwalimu Subi kutenda tukio hilo inaelezwa ni yeye kuwa na ugomvi na mwalimu huyo akigombea uongozi kwenye kitengo cha elimu ya kujitegemea.
Baada ya mtuhumiwa kukamatwa, alikiri kumchoma mwenzake na kitu chenye ncha kali kutokana na walimu wa shule hiyo kumchukia na kumtenga.
Mmoja wa walimu ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema siku ya tukio mwalimu Subi aliyehamishiwa shuleni hapo wiki chache zilizopita akitokea Bukoli hakuwa na ugomvi na mwalimu aliyemchoma kisu, bali alikuwa na ugomvi na mwalimu mwingine.