Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mfumo wa kufuatilia wajawazito wenye uchungu

Penina Macha ambaye ni Mwanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) akizungumzia mfumo wa Mamatrack alioubuni unaoweza kufuatilia mwenendo wa mama na mtoto tangu uchungu unapoanza

Muktasari:

  • Mfumo huu, unaotumia akili bandia (AI), unalenga kuboresha huduma za afya vijijini na maeneo yenye ufinyu wa rasilimali. Tayari umefanyiwa majaribio Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Dar es Salaam. Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) imezindua ubunifu wa kidijitali unaoitwa Mamatrack, mfumo wa uchunguzi wa wakati halisi unaotumika kufuatilia maendeleo ya uchungu wa uzazi pamoja na kutathmini afya ya mjamzito na mtoto aliye tumboni.

Mfumo huo umeonyeshwa kwa mara ya kwanza katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea jijini hapa.

Mamatrack unachanganya uhandisi, teknolojia ya michoro zinazosaidiwa na akili unde (AI) ili kuchukua nafasi ya karatasi ambazo zimekuwa zikitumika kwa muda mrefu lakini mara nyingi huwa hazina ufanisi au usahihi.

Ubunifu huo unalenga kuboresha utambuzi wa mapema wa changamoto za uzazi, hasa katika maeneo yenye rasilimali haba, ambapo vifo vya mama na watoto wachanga bado ni tatizo kubwa.

Kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Malaria Tanzania (TDHS-MIS) wa mwaka 2022, vifo vya kinamama wakati wa kujifungua vilipungua kutoka 530 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 hadi 104 mwaka 2022. Mafanikio haya yanatokana na ongezeko la upatikanaji wa huduma bora za afya.

Akizungumza na Mwananchi leo, Julai 3, 2025 katika viwanja vya maonyesho, Penina Macha, mmoja wa wabunifu wa Mamatrack, ameeleza uwezo wa mfumo huo katika kubadilisha namna madaktari na wauguzi wanavyofuatilia hali ya uzazi.

“Teknolojia inabadilika kila siku, na watoa huduma za afya wanahitaji matokeo ya haraka ili kutoa matibabu kwa wakati. Hospitali nyingi bado zinatumia karatasi katika kufuatilia hali ya uzazi, jambo ambalo mara nyingine si sahihi. Mamatrack unatoa taarifa za moja kwa moja na kuonyesha wazi maendeleo ya uchungu,” amesema.

Macha ameongeza kuwa mfumo huo pia unakusanya na kuchambua taarifa za mara kwa mara kuhusu matatizo ya uzazi, jambo linalowawezesha wahudumu wa afya kubaini mwenendo na kuchukua hatua mapema kwa msaada wa AI iliyopo kwenye mfumo huo.

Mamatrack ni msaada kwa vituo vya afya vya vijijini na maeneo yenye ufinyu wa rasilimali, ambapo wafanyakazi wa afya huwa wachache.

Uwezo wake wa kufanya kazi bila mtandao na kutoa taarifa moja kwa moja hufanya ufuatiliaji wa uzazi kuwa sahihi, rahisi kufikiwa na kutekelezeka kwa haraka.

“Tupo wawili tuliobuni mfumo huu. Kwa sasa tupo kwenye mchakato wa kupata haki miliki kutoka Brela ili tuupeleka sokoni. Tayari tumefanya majaribio ya awali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,” ameongeza.

kizungumza, mmoja wa watembeleaji, Shani Msawili, amesema uwepo wa mfumo huo siku zijazo utasaidia kutambua kwa haraka matatizo wanayokutana nayo wanawake wakati wa kujifungua.

“Kwa sababu kila kitu kitakuwa kwenye mfumo, tutajua ni kitu gani kinawasumbua zaidi kinamama, kama ni shinikizo la damu, kifafa cha mimba, na hii itaweka urahisi katika kushughulikia tatizo husika,” amesema.