Baba amchoma mwanawe

Muktasari:
Jeshi la Polisi mkoani Songwe linamshikilia mkazi wa mtaa wa Ilembo wilayani Mbozi, Mariko Kahinga kwa tuhuma za kumuunguza mtoto wake wa miezi sita.
Songwe. Jeshi la Polisi mkoani Songwe linamshikilia mkazi wa mtaa wa Ilembo wilayani Mbozi, Mariko Kahinga kwa tuhuma za kumuunguza mtoto wake wa miezi sita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe (RPC), Janeth Magomi amesema Jeshi hilo limebaini kuwa Kahinga alimchoma mtoto huyo kwa madai kuwa sio wake huku amtuhumu mkewe kuwa alipewa mimba na mwanaume mwingine.
Kamanda Magomi amekemea kitendo hicho na kuahidi kumfikisha mtuhumiwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Awali mama wa mtoto hiyo, Patricia Mwilenga aliwaambia waandishi wa habari kuwa kabla ya tukio hilo mumewe alikuwa akitamka kauli mbaya dhidi ya mtoto akidai siyo wake.
Amesema siku ya tukio yeye alikuwa akifua nguo nje ya nyumba huku mumewe akiwa ndani na baadaye mumewe alitoka nje.
"Aliponiona aliambia amemchoma mtoto ndipo nilipoingia ndani na kumkuta mtoto akilia sana", amesema .
Amesema mtoto ameunguzwa usoni, shingoni kwenye makalio hadi mguuni.
Ofisa Muuguzi Mfawidhi msaidizi wa Hospitali ya Mkoa wa Songwe, Wilson Kasanga amekiri kumpokea mtoto huyo Januari 1, 2022 akiwa na majeraha ya kuungua na kwa sasa yupo hospitali hapo kwa matibabu zaidi.