Baba anayedaiwa kuzaa na bintiye afutiwa kesi akamatwa tena

Muktasari:

  • Baba anayedaiwa kuzaa na binti yake watoto watatu amefutiwa kesi ya kuzaa na bintiye iliyokuwa ikimkabili katika Mahakama ya Wilaya ya Rufiji, Pwani lakini akatiwa mbaroni tena na kupelekwa kituo cha Polisi Ikwiriri anakoendelea kushikiliwa kabala ya hatua nyingine, huku kukiwa na taarifa za kufunguliwa upya kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani, Kibaha.

Rufiji Pwani. Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ameiondoa mahakamani kesi ya  baba anayedaiwa kuzaa na binti yake wa damu watoto watatu;  Mabula Masunga Jiumbi, mkazi wa  Kitongoji cha Mbambe, kijiji cha Mbunju-Mvuleni, Kata ya Mkongo, Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Mabula ambaye alikuwa nje kwa dhamana  baada ya kutimiza masharti siku chache baada ya kusomewa shtaka na kupelekwa mahabusu kwa kukosa wadhamini, amefutiwa kesi hiyo leo Jumatano, Novemba 8, 2023, tarehe ambayo kesi hiyo ilikuwa imepangwa kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi.

Mwendesha mashtaka wa Serikali, Inspekta Justine Sanga ameieleza mahakama hiyo kuwa DPP hana nia ya kuendelea na kesi hiyo dhidi na kufuatia taarifa hiyo, Hakimu aliyekuwa akiisimiliza Flora Mujaya ametoa amri ya kesi hiyo kuondolewa mahakamani.

Hata hivyo, mara tu baada ya kutoka nje ya mahakama, Mabula ametiwa mbaroni tena na askari Polisi aliyekuwa akimsubiri mlangoni na akapelekwa mahabusu ya mahakama hiyo kusubiri kupelekwa katika Kituo cha Polisi Ikwiriri, kwa hatua nyingine za kisheria.

Habari ambazo Mwananchi limezipata kutoka ndani ya jeshi la Polisi hilo, mtuhumiwa huyo sasa anatarajiwa kupandishwa tena kizimbani kwa kosa hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani, Kibaha.

Mabula, alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya Rufiji Oktoba 24, mwaka huu, siku chache baada ya kutiwa mbaroni na Jeshi la Polisi Rufiji, baada ya gazeti hili kuibua kashfa hiyo.

Alisomewa shtaka moja la kufanya ngono na maharimu (ndugu ambaye mtu hawezi kumuoa au kuolewa naye kwa sababu ya unasaba wao) kinyume cha kifungu cha 158 (1) (b) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu (Penal Cod- PC).

Katika maelezo ya kosa Inspekta Sanga alidai kuwa kuwa mshtakiwa huyo alifanya ngono na binti yake Mwashi Mabula Masunga, kinyume cha sheria, kuanzia mwaka 2019 mpaka 2023 na kamba kwa muda wote huo aliweza kumpa ujauzito mara tatu na kuzaa naye watoto watatu.

Mabula alikana shtaka hilo, lakini Inspekta Sanga aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa umekamilika na akaiomba mahakama waendelee na hatua inayofuata ya usikilizwaji wa awali, yaani kumsomea mshtakiwa maelezo ya muhtasari wa kesi na mahakama ikaridhia.

Akimsomea mshtakiwa muhtasari huo wa kesi, Inspekta Sanga aliieleza kuwa mshtakiwa anaitwa Mabula Masunga Jiumbi, ana umri wa miaka 45, mpagani, na mkulima mkazi wa Mkongo na kwamba alimuoa Holo Seleli Rupile na kuzaa naye  watoto 6 wavulana wanne wa wasichana wawili.

Mshtakiwa huyo alikubaliana na maelezo hayo na Inspekta Sanga akaendelea kuwa kuanzia mwaka 2019 mshtakiwa huyo alianza kufanyan tendo la ngono na binti yako aitwaye Mwashi Mabula Masungaa na kwamba alimpa ujauzito mara tatu na kumzalisha watoto watatu.

Mabula aliyapinga maelezo hayo kuwa siyo kweli.

Inspekta Sanga aliendelea kueleza kuwa baada ya taarifa kufika kituo cha Polisi Ikwiriri alikamatwa na kuhojiwa na upelelezi ukafanyika na baada ya upelelezi kukamilika ndipo akafikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya mashtaka na mshtakiwa akakubaliana na maelezo hayo kuwa ni kweli.

Baada ya maelezo hayo Inspekta Sanga aliieleza mahakama kuwa upande wa mashtaka utakuwa na mashahidi 6 na kielelezo kimoja na kwamba kwa siku hiyo tayari walikuwa na shahidi mmoja na akaomba kuendelea.

Hakimu Mujaya alikubaliana na hoja ya upande wa mashtaka kuanza usikilizwaji wa ushahidi moja kwa moja na akaelekezwa shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka.

Shahidi huyo wa kwanza wa upande wa mashtaka alikuwa ni muathirika, yaani Binti huyo anayedaiwa kuzalishwa na baba yake watoto hao watatu, Mwashi Mabula Masunga.

Shahidi huyo katika ushahidi wake, akiongozwa na Inspekta Sanga kupitia kwa mkalimani wa lugha ya Kiswahili kwenda Kisukuma na Kisukuma kwenda Kiswahili, Ditektivu Koplo Ezekiel; aliieleza mahakama hana dini na hajui umri wake ni miaka mingapi.

Hivyo kutokana na kutokuwa na doniniliyo rasmi hakupaswa kuapa badala yake ilibidi atoe uthibitisho tu kutoa ushahidi wa kweli tupu.

Alieleza kuwa anaishi na wazazi wake, baba, mama na ndugu zake, kijijini kwao, Pambe (Kitongoji) Kata ya Mkongo (kijiji cha  Mbunju- Kivuleni) akifanya kazi ya kilimo na kwamba  ameolewa lakini mumewe ambayw anamjua kwa jina moja la Maganga hajawahi kwenda kumchukua kutoka nyumbani kwao.

Alieleza kuwa ana watoto watatu aliwataja kwa majina ya Willy Mabula Masunga, Holo Mabula Masunga na Mabula Mabula Masunga.

Hata hivyo kinyume cha maelezo yake anayodaiwa kuyatoa Polisi alikana kuwa au kuwahi kuwa na mahusiano (ya kingono) na baba yake Mabula Masunga na kwamba watoto hao siyo wa baba yake.

Alipoulizwa na Inspekta Sanga kuwa kwa nini kituo cha Polisi alieleza kuwa alizaa na baba yake alieleza kuwa ni kwa sababu Polisi wote kituoni hapo walimpiga

Pia, alipoulizwa kuwa kwa nini Polisi walimpiga wakati alifika kulalamika kuwa alizaa na baba yake alijibu kuwa walikuwa wanampiga hata kabla ya kujua swali nililoulizwa na wala kosa, hivyo aliamua  kusema hivyo.

Hivyo, Inspekta Sanga alimuuliza kuwa kama Ikitokea uthibitisho wa kisayansi kuwa watoato ni wa baba yake yuko tayari kuwajibika kwa kuidanganya Mahakama, alijibu kuwa yuko tayari kushtakiwa sababu hajazaa na baba yake.

Kwa mujibu wa habari ambazo Mwananchi linazo kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Ikwiriri, hata mke wa mshtakiwa ambaye pia ndiye mama wa binti huyo anayedaiwa kuzaa na baba yake katika maelezo yake Polisi alikiri kuyafahamu mahusiano hayo na kuwalea watoto hao.