Baba awaomba Watanzania wamsaidie matibabu ya mwanae

Muktasari:

  • Unaweza kumsaidia Martine kwa kumtumia fedha kupitia namba 0688 273 901 ambayo ni Airtel inayosoma jina la Pretronila Samiano.

Dar es Salaam. Mkazi wa kijiji cha Gasaboy mkoa wa Manyara, Bionise Tarmo amewaomba wasamaria wema kumchangia fedha mwanae Martine Tarimo (28) ili aweze kutibiwa.

Mwanae huyo amelazwa wodi namba 3D katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kutokana na matatizo ya figo na moyo huku familia hiyo ikiwa haina uwezo wa kumudu gharama za matibabu.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumamosi Novemba 17, 2018, Tarimo alisema walifika hospitali hapo tangu Septemba 6, 2018 na kutakiwa wafanyiwe upasuaji ambao ulishindikana kutokana na uwezo mdogo.

“Wasamaria wema walitupeleka kwenye uongozi wa JKCI, wakatuambia ni muhimu tutafute bima ya afya kwa sababu hata kama atafanyiwa upasuaji bure bado, matibabu mengine yanahitajika,” alisema Tarimo

Amesema mwanae anasumbuliwa na tatizo la figo linalosababisha tumbo kujaa maji ambayo yamekuwa yakiondolewa kwa kuvutwa.

“Zamani alilazwa kwenye hospitali ya Hydom lakini alipozidiwa tukaletwa Muhimbili, sina uwezo hata chakula kwangu ni shida sana, naomba msaada ili mwanangu aweze kutibiwa,” alisema Tarimo aliyefika ofisi za Mwananchi Tabata relini jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wasamaria wema wanaomsaidia Tarimo ambao walimsaidia kufika ofisi za Mwananchi wamekiri hali ya familia hiyo ni duni na kwamba, msaada watakaopewa unaweza kuokoa maisha ya kijana wao.

“Nililazwa na baba yangu pale Muhimbili kwa miezi kadhaa, siku zote tumekuwa tukimsaidia Mzee Tarimo na sasa tukamshauri aje Mwananchi, wasamaria wema wanaweza kumchangia,” alisema Bernad Jonas, mkazi wa Goba jijini Dar es Salam.

Katibu Tawala wa Manispaa ya Ilala, Sheila Lukuba amepitisha barua ya kuisaidia familia hiyo ipate msaada kwa ajili ya matibabu ya Martine.