Baba mbaroni akidaiwa kulala na binti yake wa miaka 11

Baba mbaroni akidaiwa kulala na binti yake wa miaka 11

Muktasari:

  • Dunia ina visa na mikasa.Ndio msemo unaoweza kuutumia kuhusiana na tukio la Ikwabe Gibogo (58) mkazi wa Kitongoji cha Chamoto wilayani hapa, kukamatwa akidaiwa kumwilingilia mtoto wake wa miaka 11.

Serengeti. Dunia ina visa na mikasa.Ndio msemo unaoweza kuutumia kuhusiana na tukio la Ikwabe Gibogo (58) mkazi wa Kitongoji cha Chamoto wilayani hapa, kukamatwa akidaiwa kumwilingilia mtoto wake wa miaka 11.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 23, mwaka huu, usiku chumbani mwake baada ya polisi kupata taarifa za vitendo vyake hivyo na kumkuta na watoto wawili akiwemo huyo wa kike na mwingine wa miaka (4), ambaye inadaiwa alizaa na binti yake mkubwa baada ya kuolewa ikabainika alipewa mimba na baba yake akalazimika kumpelekea mtoto wake na kutokomea mkoani Simiyu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Daniel Shillah akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu alikiri kuwa tukio lipo na mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi na uchunguzi unaendelea ili kubaini undani wake.

“Alikamatwa kwa tuhuma za kumwingilia mtoto wake wa miaka 11 ambaye anaishi naye hapo, uchunguzi unaendelea ukikamilika tutatoa taarifa kamili, nami naendelea kulifuatilia mara kwa mara,” alisema.

Hata hivyo, Mwananchi limethibitishiwa na chanzo cha uhakika kuwa katika uchunguzi wa kitabibu imebainika kuwa mtoto huyo ameishaingiliwa mara nyingi na mara ya mwisho ilikuwa Januari 21, siku mbili kabla ya kukamatwa kwa mtuhumiwa.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyerere, Tanu Warioba alidai siku ya tukio hakuwa kazini ila anaamini alihudumiwa na watu wengine.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa kitongoji cha Chamoto, Marwa Nyambuge, aliliambia gazeti hili kuwa wananchi walimjulisha kuhusu vitendo anavyomfanyia mtoto wake kwa kuwa kila siku usiku wanasikia kelele akilalamika kuumizwa.

“Polisi nao wakawa wamepata taarifa waliniita majira ya saa 3 usiku tukakutana stendi kisha saa 4 usiku tukaenda nikajitambulisha mimi akatoka na shuka na panga, akafungua polisi wakamwambia aache panga, akahojiwa nyumba kama ni yake akadai amepewa kuishi,” alisema na kuongeza,

“Nyumba ina vyumba zaidi ya vitatu akaulizwa anaishi na nani akasema watoto wake na wanapolala akatupeleka anatandika chini, tuliwakuta hao watoto wako uchi maana shuka wanayojifunika ndiyo aliyotoka nayo, akaulizwa anapolala akadai hapo na wanajifunika shuka moja,” alisema.

Alionyesha wanavyolala mtoto wake wa kike ndiye analala naye karibu yule mdogo anawekwa pembeni, mtoto alikiri kuwa anaingiliwa na baba yake kwa muda mrefu. Hata hivyo, mtuhumiwa baada ya kubanwa alikiri kufanya vitendo hivyo.

Alisema licha ya kuwa watoto wake wana umri wa kwenda shule hajawaandikisha akiwamo wa kiume, ambaye kwa sasa anadaiwa kufanya vibarua baada ya kutimuliwa na baba yake.

Majirani waeleza

Loyce Chacha alidai kuwa mtuhumiwa alitengana na mkewe baada ya kumfumania akiwa amelala na binti yake mkubwa. “Kitendo hicho kilimuuma na kusema wazi, lakini mwanaume alimpiga na kulazimika kwenda kwao Simiyu kwa madai hawezi kuchangia mume na mwanawe,” alisema.

Aliondoka na watoto wake wawili wa kiume na kike akiwemo huyo ambaye sasa amemgeuza kuwa mke wake. Hata hivyo, mke huyo alikaa muda mfupi akaugua na kufariki na ndipo mtuhumiwa aliwafuata watoto wake hao na kuamua kuishi nao.

“Nyumba aliyokuwa amepanga awali alifukuzwa baada ya kubaini kuna mambo yasiyo ya kawaida maana alikuwa na chumba kimoja na analala naye pamoja. Akahamia nyumba ya mtu mmoja ambayo haijaisha huko akamfukuza mtoto wa kiume ili abaki na huyo wa kike, ambaye inadaiwa alianza kumwingilia akiwa na miaka nane,” alidai jirani wa mtuhumiwa.

Mmoja wa majirani (jina limehifadhiwa) alisema: “Mtoto huyo aliwahi kusema, lakini watu hawakujali wakachukulia ni mambo ya utoto. Alisema vitendo vibaya anavyofanyiwa na baba yake usiku wanapokuwa wamelala, watu hawakufuatilia.”

Hata hivyo, alidai kuwa mtuhumiwa ambaye kazi zake ni kufanya vibarua ana tabia za ulevi na kupenda wanawake, lakini alibadilika ghafla baada ya kuleta watoto na hasa baada ya kumfukuza wa kiume ndipo wakabaini kumgeuza mwanae kuwa mke.

Kuzaa na mtoto wake

Joseph Magoiga, ambaye ni Mwenyekiti mstaafu wa kitongoji hicho aliliambia Mwananchi kuwa mtuhumiwa alianza kufanya ngono na mwanae mkubwa, ambaye pia alikuwa na umri chini ya miaka 18 na kumpa mimba na kuzaa naye mtoto.

“Binti yake huyo alichukuliwa na kijana mmoja kama mke bila kujua kama baba mkwe wake alikuwa ameishampa mimba wakaenda kuishi Lamadi, alipojifungua mtoto akawa anafanana na baba mkwe wake, alipofuatilia alibaini kuwa alikuwa kama mke wake akamwambia amrudishe kwao na ndoa ikavunjika,” alisema.

Alisema binti aliamua kumletea mtoto huyo ambaye ameishi naye kama mwanae na kama mjukuu na wote wamechukuliwa kwenda kupata hifadhi katika Kituo cha Hope for Girls and Women Tanzania kilichoko Mugumu wakati suala lake likishughulikiwa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwel amekiri kupokelewa kwa watoto hao wawili baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu chini ya usimamizi wa askari wa dawati la jinsia na watoto la Polisi Mugumu.