Baba wa mtoto anayedaiwa kuibiwa afunguka

Muktasari:
Shahidi katika kesi ya wizi wa mtoto, Emmanuel Mwanga ameiambia mahakama ya Mwanzo Vwawa mjini mkoani hapa kuwa watuhumiwa kwa kitendo hicho walikuwa na nia ovu.
Songwe. Shahidi katika kesi ya wizi wa mtoto, Emmanuel Mwanga ameiambia mahakama ya Mwanzo Vwawa mjini mkoani hapa kuwa watuhumiwa kwa kitendo hicho walikuwa na nia ovu.
Katika kesi hiyo, Rebecca Bernard (20) aliyekuwa mfanyakazi wa ndani na Joyce Sinkala (50) wanatuhumiwa kuiba mtoto.
Inadaiwa kuwa, mtoto huyo alitoroshwa Oktoba 8, 2022 na kupatikana nyumbani kwa Joyce Sinkala katika Mamlaka ya Mji wa Tunduma, usiku wa kuamkia Oktoba 9 mwaka huu baada ya mfanyakazi wa ndani kuhojiwa alipokamatwa kijijini kwao Laela Sumbawanga.
Mwanga aliiambia Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Lina Okello kwamba, mfanyakazi wake huyo alimtorosha mtoto wake Merini Emanuel (10) wakati yeye akiwa shambani.
Mzazi huyo amekanusha madai kwamba alimpeleka mtoto kwa mama yake mkubwa, kwani yeye ameishi na mtoto wake tangu akiwa na miaka miwili baada ya kuachana na mama yake na kwamba hakuwahi kumtambua mshitakiwa wa pili kuwa na mahusiano ya kindugu na mama Mzazi wa mtoto.
Amedai tukio la kutoroshwa lilitokea wakati wa likizo fupi na kwamba baada ya kumkamata mfanyakazi wa ndani, alieleza kwamba alimuacha mtoto kwa mama mkubwa wa mtoto jambo ambalo halikuwa la kweli, kwani mwanamke huyo (Joyce) hana undugu wowote na mama wa mtoto.
"Mara baada ya kumkamata mfanyakazi wa ndani ndiye aliyenisaidia kumpata Joyce Sinkala akiwa na mtoto nyumbani kwake Tunduma," amesema.
Kwa upande wake Hakimu wa Mahakama hiyo, Lina Okello ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 25 mwaka huu itakapoendelea, huku washitakiwa wakiachiwa kwa dhamana ya masharti ya kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika.