Babu Owino awataka vijana kuleta mabadiliko nchini
Muktasari:
- Mwanasiasa wa Kenya, Babu Owino amewataka vijana kuwania nafasi za uongozi ili kwenda kuleta mabadiliko ndani ya Tanzania, kwani vijana ni Taifa la leo.
Dar es Salaam. Mwanasiasa machachari na Mbunge wa Embakasi ya Mashariki nchini Kenya, Paul Owino maarufu 'Babu Owino' amewataka vijana wa Kitanzania kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zinazofuata.
Babu Owino ametoa wito huo leo Alhamisi Februari 29, 2024 katika mkutano mkuu wa ngome ya vijana ya ACT- Wazalendo, uliokuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo kufanya uchaguzi wa kumpata mwenyekiti na makamu wake, watakaoongoza ngome hiyo kwa miaka mitano ijayo.
Mwanasiasa huyo, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo amesema mwaka huu na mwakani kuna chaguzi zinafanyika hapa nchini, hivyo lazima vijana wajitokeze kuwania viti kwenda bungeni na kwenye mabaraza ya madiwani.
"Najua tunatoka katika familia zisizojiweza na masikini lakini ni wewe kijana utakaoibadilisha familia yako na Taifa kwa ujumla kwa kuhakikisha Serikali inaboresha huduma za jamii, kuanzia leo vijana mkitaka kitu pigania usingoje kupewa, kwa sababu hautapewa lazima usimame upiganie," amesema Babu Owino.
Babu Owino amesema Tanzania na maeneo mengine vijana hawana ajira na kwa nyakati tofauti kundi hilo limekuwa likiambiwa ndio viongozi wa kesho, lakini amewataka kuachana na msemo na kutambua wao ni Taifa la leo, kesho na keshokutwa.
"Hakikisheni nyie ni viongozi wa leo kesho na keshokutwa, lazima vijana tuamke na kujipigania na tujinasue na mnyororo wa umasikini na uongozi mbovu, jambo hilo litafanywa na viongozi kama nyinyi.
"Lazima tuwe na viongozi bora, sio bora viongozi piganieni nchi yenu, Julius Nyerere, Kwame Nkrumah na Rashid Kawawa walianza wakiwa vijana, Babu Owino bado kijana wewe unangoja nini? Kama kijana.
Kuhusu ACT- Wazalendo
Katika hatua nyingine, mwanasiasa huyo amewapongeza viongozi wa ACT - Wazalendo kwa namna wanavyokiongoza chama hicho tangu kilivyoanzishwa mwaka 2014 hadi sasa.
"ACT- Wazalendo ina mizizi katika nchi ya Tanzania, Kenya tunakitambua ndio maana nimekuja, nisingekitambua nisingekuja leo hapa, kuwepo kwangu leo hapa najisikia bashasha na furaha tele kama kibogoyo aliyefanikiwa kupata jino moja tu.
"Chama cha ACT-Wazalendo, kinazingatia hoja na masilahi ya Watanzania na vijana, ndio maana kuna baraza kivuli linalowasaidia na kuwajenga kuwa viongozi wa leo na kesho," amesema Babu Owino.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu amesema chama hicho kinawategemea vijana na hakiwezi kutekeleza malengo pasipo kushirikisha kundi hilo lenye watu wenye weledi, maarifa, shupavu, walio tayari kwa mapambano na wenye mioyo ya kujitolea kufanya kwa ujenzi wa chama na Taifa.
Ado amesema chama hicho kinawaamini wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa ngome kuanzia ngazi ya mikoa, hivyo watahakikisha wanachagua mwenyekiti bora kwa akili na maono yao.
"Tunaamini mna utashi wenu, kila mmoja anajua baya na zuri ni lipi, unyeti wa jambo hili la uchaguzi leo ndio siku ya uamuzi kama mnataka miaka mitano ijayo muwe uongozi wa ngome unaowajibika au unaolegalega.
Katibu wa ngome hiyo anayemaliza muda wake, Mwanaisha Mndeme amesema mkutano huo pamoja na mambo mengine utachagua wajumbe wa watakaokwenda moja kwa moja katika halmashauri kuu ya chama hicho.
Katika salamu zake kwa wajumbe wa mkutano mkuu huo, mwenyekiti wa ngome hiyo, Abdul Nondo amesema leo ni siku nyingine kwa wajumbe hao kufanya uamuzi wa kuchagua viongozi watakaoongoza ngome kwa mara nyingine.
Katika uchaguzi huo unatajwa kuwa na ushindani, Nondo anayetetea nafasi hiyo atachuana na Ruqayya Nassir, Petro Ndolezi na Julius Massabo waliojitokeza kuwania kiti hicho.