Semu, Maharagande wajitosa kumrithi Zitto

Makamu Mwenyekiti ACT Wazalendo (Bara), Dorothy Semu akionyesha begi lenye fomu ya kugombea nafasi ya Kiongozi wa Chama hicho, baada ya kukabiziwa jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu za kuwania uongozi ndani ya ACT- Wazalendo bado liko wazi, wawili wamejitosa kumrithi Zitto Kabwe.
Dar es Salaam. Joto la uchaguzi ndani ya ACT- Wazalendo limeendelea kushika kasi baada ya wanachama wengine waandamizi kuchukua fomu kuwania nafasi ya Kiongozi wa Chama (KC) inayoongozwa na Zitto Kabwe.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Dorothy Semu na Mbarala Maharagande, Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu kwa nyakati tofauti wamechukua fomu na kueleza mikakati watakayoifanya iwapo watapewa fursa hiyo.
Semu na Maharagande wamejitosa kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi utakaofanyika Machi 5 na 6 mwaka huu, jijini Dar es Salaam kuchukua nafasi ya Zitto atayekuwa anamaliza muda wake wa uongozi wa miaka kumi ya kikatiba ya chama hicho.
Wawili hao wamechukua fomu jana makao makuu ya ACT- Wazalendo, Magomeni ikiwa ni takribani siku tano tangu vigogo wengine, Mwenyekiti wa chama, Juma Duni Haji ‘Babu Duni’ na Makamu wake Zanzibar, Othuman Masoud Othuman kujitosa kuwania nafasi moja ya mwenyekiti wa chama hicho.
Wadadisi wa kisiasa wanauangazia uchaguzi huo kuwa na mvutano mkali kutokana na aina ya wagombea wanaoendelea kujitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za chama hicho. Hasa ikitizamwa mpaka sasa waliojitokeza ni wajumbe wa kamati kuu.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Rainery Songea amesema nafasi ya kiongozi wa chama inahitaji mtu mwenye, uelewa mpana, uwezo na mzoefu mkubwa, hivyo Semu na Maharagande wana uzoefu huo kwa namna walivyohudumu nafasi mbalimbali katika siasa.
"Yeyote kati ya hawa anaweza kuibuka mshindi itategemea ushawishi na uamuzi wa wajumbe watakaowapigia kura, majina yao si makubwa ila wapo katika siasa kwa muda mrefu.
"Ingekuwa Zitto anagombea tungeweka mshindi ni fulani, lakini hawa kila mtu ana nafasi ya kuibuka mshindi, ninaamini hawa wana uwezo mzuri wa kutekeleza majukumu yao endapo mmoja wao akifanikiwa kushinda," amesema Songea.
Mchambuzi mwingine Kiama Mwaimu amesema Semu na Maharagande wote wana asilimia 50 kwa 50 ya kushinda nafasi hiyo.
"Huyu mama (Semu) ni mwana mikakati mzuri na siasa zake ni diplomasia hana tofauti na Zitto ndivyo uelekeo wa sasa uliopo wa siasa za maridhiano, lakini Maharagande yeye siasa zake za kiuharakati zaidi zingefaa wakati ule utawala wa awamu ya tano iliyongozwa na Hayati Johh Magufuli, si sasa hivi utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Mwaimu.
"Ila yote kwa yote wajumbe ndiyo watakaoamua nani awe kiongozi wa chama kwa miaka mitano maana wote bado wana nafasi ya kuibuka kidedea," amesema.
Mchuano mwingine unatarajia kujitokeza Ngome ya Vijana, Julius Massabo, Ruqaiya Nassir na Petro Ndolezi wameshajitokeza kuchukua fomu akisubiriwa Abdul Nondo ambaye ametangaza kutetea nafasi hiyo.
Ngome ya Wanawake nako hakupoi baada ya Janet Rithe na Severina Mwijage wametangaza nia ya kuwania uenyekiti wa ngome hiyo watakayoiongoza kwa miaka mitano.
Rithe anagombea kwa mara ya pili baada ya mwaka 2020 kushindwa na Rukia Kimwanga huku Mwijage ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho, ikiwa ni mara yake ya kwanza kuwania.
Vipaumbele vya Semu, Maharagande
Jana, wa kwanza kuchukua fomu alikuwa Semu aliyefika kwa maandamano akisindikizwa na wanawake na baada ya kukabidhiwa alisema akifanikiwa kushinda nafasi hiyo atahakikisha atasimamia vema sera za ACT- Wazalendo zitakazotekelezeka na kujibu changamoto za Watanzania.

Mgombea nafasi ya Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Mbarala Maharagande (kulia) akikabidhiwa begi lenye fomu ya kuwania nafasi hiyo na katibu wa kamati Maalumu ya uchaguzi wa chama hicho, Mohamed Masaga, leo Februari 18,2024. Picha na Michael Matemanga
"Lakini suala jingine kiongozi wa chama ndiye muongozaji mkuu wa viongozi wa chama hiki, hivyo nitajikita kuwajengea uwezo watendaji wetu ili kuwa viongozi bora ili ACT kiwe chama kupigiwa mfano katika kuwapika viongozi.
"Mnafahamu kwamba mwaka huu tuna uchaguzi wa Serikali za mitaa na mwakani Uchaguzi Mkuu, ninataka kuwa kiongozi wa chama atakayekipeleka chama hiki katika ushindi utakaoweka rekodi mpya ya vyama vya siasa vya ushindani nchini," amesema Semu aliyewahi kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo miaka iliyopita.
Semu ambaye pia ni Waziri Mkuu Kivuli wa ACT- Wazalendo, amesema amejipima na kuona anatosha kuwania nafasi ya kiongozi wa chama kutokana historia yake kukiongoza chama hicho wakati kinaanzishwa akihudumu kama katibu wa idara ya utafiti na mafunzo, katibu wa fedha.
"Nimechukua fomu kuwania nafasi hii kwa sababu ninaamini kwenye uongozi wa pamoja, wakati nikihudumu nafasi kaimu katibu mkuu nilifanikiwa kukivusha chama hiki katika kipindi ambacho demokrasia ilikuwa changamoto," amesema Semu huku akivunia utendaji kazi wake uliosababisha ACT - Wazalendo kupata hati safi.
Semu amesema ni wakati muafaka kwake kuwania nafasi ya kiongozi wa chama kwa sababu anatosha, anafaa katika kukivusha chama hicho kusonga mbele za katika utekelezaji wa majukumu yake.
Wakati Semu akieleza hayo, Maharagande ameahidi kuyaendeleza mazuri yaliyofanywa na Zitto, akisema ACT-Wazalendo ndiyo chama kinachonyesha njia ya kutoa hoja mbadala kwa maslahi ya Taifa.
Amesema miongoni mwa mambo atakayoyatekeleza akifanikiwa kushinda kiti hicho ni pamoja na kuimarisha sekretarieti ya ACT-Wazalendo kwa kuwa na watendaji wazuri wanaosimamiwa na viongozi wa kisiasa.
"Muundo uliopo hivi sasa nitaufanyia maboresho madogo ili kuhakikisha tunakwenda pamoja bila kumuacha mtu yeyote katika utendaji wa majukumu, nitaboresha stahiki za watendaji wote ili kufanya kazi kwa ufanisi.
"Nitasimamia uandaaji wa programu ya mafunzo kwa viongozi wetu wa ngazi zote ili kuwa wenye weledi na ufanisi wa kusimamia majukumu ya chama katika maeneo yao," amesema Maharagande ambaye ni msemaji wa katiba na sheria katika baraza kivuli la chama hicho.
Mbali na hilo, Maharagande amesema atahakikisha anasimamia uwajibikaji ndani ya ACT- Wazalendo ili kuhakikisha kila kiongozi atakayechaguliwa ili kumsaidia katibu mkuu wa chama hicho.
Amesema katika uongozi wake chama hicho, kitakuwa na watendaji wa wabunifu watakaotekeleza majukumu yao kisasa.
"Nitaimarisha mtandao wa chama kwa kuongeza idadi ya wanachama kutoka milioni 1.2 waliosajiliwa katika mfumo wa ACT Wazalendo kiganjani hadi milioni 7 ifikapo mwaka 2029," amesema
Majumuku ya KC
Miongoni mwa majukumu ya Kiongozi wa Chama (KC)ni pamoja na kusimamia viongozi wote wa chama, sera, ndiye mwenyekiti wa kikao cha mkutano mkuu wa kidemokrasia, kuteua wajumbe watano wa kamati kuu na kutoa tamko rasmi la masuala ya sera na mtazamo wa chama kwenye mambo ya kitaifa na kimataifa.