Makada 28 ACT Wazalendo wajitosa kuwania uongozi

Muktasari:
- Miongoni mwa waliojitokeza kugombea nafasi zu ongozi wa chama hicho, 11 wanawania ujumbe wa halmashauri na saba ujumbe wa kamati kuu, waliobaki ni ngome za vijana na wazee.
Dar es Salaam. Makada wa chama cha ACT-Wazalendo, wameendelea kumiminika kuchukua fomu za kusaka uongozi ndani ya chama hicho hasa nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu.
Tangu pazia la kuchukua na kurejesha fomu kufunguliwa Jumatano, Februari 14, 2024 jumla ya makada 28 kutoka Bara na Zanzibar wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali kati yao, 11 wamechukua fomu za ujumbe wa halmashauri na saba ujumbe wa kamati kuu, waliobaki ni ngome za vijana na wazee.
Mjumbe wa Kamati Maalumu ya Uchaguzi wa ACT-Wazalendo, Idrissa Kwaweta amesema hayo jana, Februari 15, 2024 alipozungumza Mwananchi Digital kuhusu mwenendo wa uchukuaji wa fomu utakaohitimishwa Februari 24.
“Hadi sasa katika nafasi ya juu ya Kiongozi wa Chama hakuna mtu aliyejitokeza, lakini kuanzia kesho wataanza kuchukua fomu, maana wameshatoa ratiba zao. Nafasi nyingine zilizochukuliwa fomu ni uenyekiti na umakamu uenyekiti,” amesema Kweweta.
Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT- Wazalendo, Isihaka Mchinjita amejitosa kuchukua fomu ya kuwania umakamu uenyekiti wa chama hicho (Bara), akianisha vipaumbele vyake vitano kikiwemo cha kupigania ujenzi wa demokrasia ya maslahi mapana kwa Taifa.
Mbali na hilo, Mchinjita amesema atahakikisha anakiimarisha chama hicho katika ngazi ya msingi, kujenga misingi imara ya kitaasisi, kuimarisha sera na mwenendo wa ACT- Wazalendo, ili kisibaki kuwa chama cha masuala, bali kisimamie kama chama kiongozi kwenye kusukuma na kushinikiza utekelezaji wa ajenda zenye maslahi kwa wananchi.
Mchinjita aliyewahi kuwa mwenyekiti wa ACT- Wazalendo mkoa wa Lindi, amechukua fomu hiyo jana katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Magomeni, Dar es Salaam akisema ataimarisha ngome za chama, ili kuzifanya ziwe nyenzo muhimu ya kuwaunganisha Watanzania kupigania ustawi wa Taifa.
Mchinjita ambaye ni msemaji wa sekta ya nishati, amesema ACT- Wazalendo kina ngome za vijana, wazee na wanawake na katiba ya chama hicho, inaeleza makamu mwenyekiti ndiyo mlezi wa ngome hizo, hivyo akishinda nafasi hiyo ataziimarisha ili ziwe imara zaidi.
“Nia yangu ni kujenga chama chenye uwezo wa kuendelea kuwa chama chenye kuibua masuala na kuonyesha suluhisho na hatimaye Watanzania wakiamini, ili kukiwezesha kuunda Serikali.
“Pia azma yangu ni kushirikiana na viongozi na wanachama wenzangu kuwa na chama kitakachoweza kuweka shinikizo madhubuti, ili kuhakikisha rasilimali za Taifa letu, mipango ya uchumi inajenga Taifa la wote kwa maslahi ya wote,” amesema Mchinjita.