Ni vita vya Babu Duni, Othman uenyekiti ACT Wazalendo

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji, amesema haogopi kushindwa, anahitaji kampeni za kistaarabu na ni yeye pekee anayeweza kuchukua hiyo nafasi ya juu.

Dar/Unguja. Mchuano ndani ya ACT-Wazalendo umeshika kasi kati ya vigogo baada ya wawili waandamizi kujitosa kuwania nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi utakaofanyika kati ya Machi 5 na 6, mwaka huu.

Vigogo hao ni Juma Duni Haji ambaye tayari amechukua fomu kutetea nafasi hiyo na makamu wake, Othman Masoud Othman, makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye wenyeviti na makatibu wa mikoa 27 ya kichama wamemchukulia fomu.

Ingawa Othman hajapatikana kueleza kama amekubaliana na waliomchukulia fomu, ikiwa atakubali utakuwa mchuano wa aina yake kutokana na uzoefu na uzito wa wagombea wenyewe.

Mbali na mchuano huo katika nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, shughuli nyingine pevu itakuwa katika ngome ya vijana ambako hadi sasa wanne wameonyesha nia kuwania nafasi hiyo, akiwamo Abdul Nondo anayetetea kiti chake.

Mchuano mwingine unatarajiwa katika kuwani nafasi ya kiongozi wa chama hicho, itakayokuwa wazi baada ya Zitto Kabwe kumaliza muda wake wa awamu mbili kwa mujibu wa Katiba ya ACT-Wazalendo.

Miongoni mwa walioonyesha nia ni Dorothy Semu (makamu mwenyekiti bara) na Ismail Jussa ambaye ni mjumbe wa kamati kuu.


Duni achukua fomu

Baada ya mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa chama hicho, Joran Bashange kufungua pazia la mchakato huo, Babu Duni amechukua fomu katika ofisi ndogo za makao makuu ya chama hicho, yaliyopo Vuga, Mjini Unguja.

Duni alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Januari 30, mwaka 2022 akichukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad, aliyefariki dunia Februari 17, mwaka 2021.

Othman naye alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti Zanzibar mwaka 2022 akichukua nafasi ya Babu Duni.

Wawili hawa wanatarajiwa kuchuana katika uchaguzi utakaofanyika mwezi ujao katika ukumbi wa Mlimani City, kisha matokeo yake kutangazwa katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika Uwanja wa Biafra, Kinondoni.

Babu Duni ni miongoni mwa wanasiasa nguli na wakongwe waliotoka CUF baada ya mgogoro kati ya Maalim Seif na Profesa Ibrahim Lipumba uliokigawa chama hicho.

Wafuasi wengi wa Maalim Seif waliamua kumfuata alipojiunga na ACT-Wazalendo.

Duni ana nguvu na ushawishi mkubwa ndani ya ACT-Wazalendo upande wa Zanzibar.

Pia, alifanya kazi kwa miaka mingi na Maalim Seif, hivyo anachukuliwa kama mzee mwenye hekima na mrithi wa busara za Maalim Seif.

Baadhi ya wafuasi wa ACT-Wazalendo, wameona busara zake miaka miwili aliyohudumu uenyekiti, hivyo wangependa kuona akiendelea kutumikia nafasi hiyo kwa miaka mitano ijayo.

Lakini, haitakuwa kazi rahisi kwa Duni kuitetea nafasi yake kwa sababu Othman si mtu mwepesi, ni mzito ndani ya ACT-Wazalendo. Uamuzi wa kumteua kuchukua nafasi ya Maalim Seif kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kulimfanya awe na ushawishi mkubwa ndani ya chama hicho na nje pia.

Upinzani wake kwa Duni unaonekana kupata nguvu zaidi baada ya wenyeviti na makatibu wa mikoa wa ACT- Wazalendo Tanzania Bara na Zanzibar, kuamua kumchukulia fomu ya kugombea.

Hatua hiyo, inaashiria kuwa Othman ana kundi kubwa la wafuasi watakaompigia kura, lakini anabeba ndoto za kundi la vijana ambao wangetamani kumuona Duni anapumzika siasa za majukwaani na kubaki mzee au mshauri wa chama hicho.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, Kiza Mayeye amesema wameamua kumchukulia fomu Othman wakiamini endapo akishika nafasi hiyo kutakuwa na manufaa makubwa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar.

“Tunatambua ndani ya ACT-Wazalendo wapo viongozi mbalimbali wenye uwezo wa kuongoza, lakini sisi tumejiridhisha kwamba Othman ana sifa za ziada za kuwa mwenyekiti wa chama.

“Hili tumelianzisha sisi, tuna imani wajumbe wengi wa mkutano wataunga mkono mchakato kwa kumtafutia kura. Tutaenda Unguja kumkabidhi fomu yake, tutamuomba tukiamini atatukubalia ombi letu, kisha tutarudi katika maeneo yetu kufanya kazi ya kampeni ya kumwombea kura Othman,” amesema Mayeye ambaye ni mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma.


Kauli ya Duni

Duni amesema kwa miaka miwili amekuwa mwenyekiti wa chama hicho akirithi nafasi ya Maalim Seif na sasa ameamua kugombea tena kukamilisha miaka mitano akisimama mwenyewe.

Amesema ana imani yeye ni mwenye uwezo mkubwa wa kuitetea nafasi hiyo kwa sababu ya uwezo mkubwa alikuwa nao na kujifunza kwa miaka mingi siasa za Zanzibar.

“Hivi sasa Maalim Seif hayupo tena, naamini mtu pekee anayeweza kushika nafasi ya juu kwenye chama ni mimi na ndiyo maana nimeamua kugombea tena. Siogopi kushindwa, nipo tayari hata kupata kura moja, lakini nahitaji kampeni za kistaharabu zisizolenga kumchafua mgombea yeyote yule,” amesema Duni.


Wachambuzi wa siasa

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Richard Mbunda amesema baadhi ya chaguzi za ndani za vyama vya siasa zikiisha zinakuwa na mvurugano, hasa inapotokea mmoja wa mgombea kuchukuliwa fomu na kundi fulani linalomuonyesha linamuunga mkono.

“Mkijikusanya na kumchukulia mtu fomu si kosa na demokrasia ndani ya vyama kwa kumtaka kiongozi mnayemuhitaji. Lakini katika muktadha wa mmoja aliyekuwapo madarakani na kuwania nafasi hiyohiyo ni rahisi kuingia kwenye mgogoro baada ya uchaguzi kuisha.

“Sidhani kama Duni atajisikia vizuri, hii maana yake kwamba hatoshi katika ile nafasi hadi watu wameungana kumchukulia fomu makamu wake, ingawa inaonyesha demokrasia ndani ya chama, lakini huenda ikaleta mpasuko ndani ya chama hasa kwa mtu kama Duni ambaye ana ushawishi,” amesema Dk Mbunda.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Revocutus Kabobe amesema: “Natamani kuwaona wawili hawa wakichuana katika nafasi hiyo ili demokrasia iamue, tumekuwa na changamoto ya bosi wangu akichukua fomu, mimi siwezi kuchukua kushindana naye, lakini haya ni mawazo ya kutoimarisha demokrasia.

“Wote hawa wakiingia kwenye kinyang’anyiro wanachama wataamua nani anafaa kuwa mwenyekiti, Duni atabebwa na uzoefu wa muda mrefu kwenye siasa, ni mtu mwenye msimamo kwa kile anachokiamini. Wakati Othman ni mtu wa msimamo aliwahi kusimamia nafasi ya uanasheria mkuu wa Zanzibar,” amesema Dk Kabobe.

Alifafanua kuwa, ACT-Wazalendo ina wagombea wazuri ngazi ya uenyekiti, hata hivyo kitakachompunguzia kura Babu Duni huenda likawa suala la umri, lakini kitaalamu halihusiani na utendaji ila katika mchakato wa uchaguzi kuna mengi.

Mchambuzi mwingine wa siasa, Makame Ali Issa, alisema Duni ni mwanasiasa mkongwe anayejitoa kwa ajili ya chama na alishawahi kukaa jela kutokana na changamoto za kisiasa.

Hata hivyo, Issa alisema bado anaushawishi ndani ya ACT-Wazalendo katika kuwania nafasi hiyo.

“Ujio wa Othman ndani ya ACT-Wazalendo na kushika nafasi mbalimbali licha ya alipopokewa wengi hawakukubaliana naye, lakini hawa wanaompigia debe wanaangalia masilahi binafsi kutoka kwa kiongozi huyo.

“Kama mchakato wa uchaguzi utakuwa sawa, basi kutakuwa na mchuano mkali, lakini itategemea fitina itakayojengwa kwa sababu taarifa nilizonazo zinadai kuwa, baada ya Duni kushinda uenyekiti mwaka 2022, baadhi ya wanachama walisema katika uchaguzi ujao watampiga chini Babu Duni,” amesema Issa.


Ngome ya Vijana

Katika Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Nondo anatarajiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa washindani wake, Julius Masabo, Petro Ndolezi na Ruqaiya Nasir walioonyesha nia ya kuwania kiti hicho.

Kati ya watia nia hao tayari Ndolezi ameshachukua fomu, huku wengine wakitarajiwa kuchukua leo na kesho.

Katika hatua nyingine, Bashange ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo (Bara), amesema mdahalo wa watia nia ya uenyekiti wa ngome ya vijana utafanyika Februari 20, wakati ngome ya wanawake ni Februari 27 huku wa kiongozi wa chama na mwenyekiti na makamu wenyeviti Bara utakuwa Machi 4.

Bashange amesema gharama za fomu ya kuwania nafasi ya kiongozi wa chama ni Sh500,000, uenyekiti na makamu wake Sh500,000, ujumbe wa halmashauri kuu, kamati kuu na uenyeti wa ngome zote tatu ni Sh100,000.