Jussa: Niko tayari kubeba majukumu ACT-Wazalendo

Mjumbe wa kamati kuu ya chama cha ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu akizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti hili wakati wa mahojiano maalumu jijini Zanzibar. Picha na ACT
Unguja. Chama cha ACT-Wazalendo kimo katika mchakato wa uchaguzi wa ndani kuanzia ngazi ya matawi, kata, majimbo, mikoa na baadaye ngazi ya Taifa utakaofanyika Machi, 2024.
Katika uchaguzi huo, kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe anamaliza muda wake. Miongoni mwa wanaotajwa kumrithi ni mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Jussa Ismail Ladhu.
Katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika hivi karibuni Unguja, Jussa amesema anatafakari suala hilo na mambo anayokusudia kufanya endapo atachaguliwa.
Pia alizungumzia siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, akibainisha nafasi ya vyama vya upinzani kushika dola.
Swali: Umekuwa ukitajwa kuwa miongoni mwa wanachama wa ACT-Wazalendo wanaotarajia kugombea nafasi ya kiongozi wa chama. Unajipimaje katika nafasi hiyo?
Jibu: Hoja ya kutafakari, imekuja kwa sababu hili ni suala zito. Unapochukua nafasi ya juu ya chama, unabeba majukumu mazito.
Nilishaonyesha hamu hiyo Februari, 2020 tulipofanya uchaguzi, nikachukua fomu nikapambana na Zitto. Nashukuru ilileta ushindani mkali, hivyo ikavunja hoja kwamba kwa nafasi hizi tunakuwa na wagombea pekee, ambayo mimi siamini.
Wakati ule kura hazikutosha, safari hii Zitto anapomaliza muhula wake, natafakari kwa kuwa najua watu wengi wametaka nichukue nafasi hiyo.
Si tu ya uongozi wa chama, hata mwaka jana tulipokuwa tukifanya uchaguzi wa mwenyekiti baada ya kifo cha Maalim Seif (Sharif Hamad), kulikuwa na vuguvugu kubwa hasa kwa vijana na la kuvutia zaidi hata kutoka Bara, wakinisukuma nichukue fomu kugombea nafasi ya mwenyekiti. Nikawaambia tumwachie Juma Duni na tulimuunga mkono.
Mwaka huu imejitokeza tena na chama kinahitaji mtu madhubuti, mwenye maono, dira na uzoefu katika uongozi; nikijipima naona ninazo sifa hizo. Niko tayari kubeba majukumu hayo.
Swali: Unatajwa kuwa mtu mwenye ujasiri wa kuongea bila kuogopa chochote, unadhani hiyo ndiyo sifa inayokubeba?
Jibu: Inawezekana ni sifa niliyonayo ikilinganishwa na wengine, lakini kiongozi wa chama ndiyo nafasi ya juu katika chama chetu kwa mujibu wa Katiba yetu.
Si tu kuwa msemaji sana, nafasi hiyo inahitaji busara na hekima; ndiyo maana ya kusema napaswa kulitafakari suala hili.
Nashukuru wenzangu wana imani nami. Huwa siwaamini watu wanaosubiri kuombwa wagombee. Mimi ni mwanafunzi wa Maalim Seif, siku zote alikuwa wazi kwamba anautaka urais wa Zanzibar.
Alikuwa akisema uongozi siku zote unakufanya uwe unacho cha kuwapa watu unaotaka kuwaongoza.
Wapo watu hata ndani ya Serikali ambao mambo yalipoharibika, wakasema mimi hata sikutaka uongozi. Sasa hiyo ndiyo natafakari. Tunahitaji mtu mwenye uwezo wa kuwa msemaji ili kukijenga chama.
Swali: Kwa muda mrefu ACT imekuwa na nguvu Zanzibar kuliko Bara, utawezaje kusawazisha hilo utakapokuwa kiongozi wa chama, unayetokea Zanzibar?
Jibu: Watu wananitambua nimejikita kwenye siasa za Zanzibar, lakini nashukuru mimi ni miongoni mwa wanasiasa wa Zanzibar tunaojitokeza katika siasa za Bara na tumekuwa tukifuatilia na kutoa maoni kwa yanayotokea kule.
Nadhani kwa uzoefu nilioupata, nimefanya kazi na watu wazito. Nimetumika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, kama mnakumbuka na ukiwa kule masuala yanayohusu Zanzibar ni yale yanayohusu Muungano, mengi nilikuwa mstari wa mbele kuwa msemaji wake.
Katika kujenga chama, kwanza nadhani tumefanya vizuri katika kipindi hiki. Wakati tumetoka Chama cha Wananchi (CUF) na kujiunga ACT-Wazalendo, ilikuwa ikihusishwa na Mkoa wa Kigoma na maeneo machache, lakini leo tunaona kinajijenga.
Kimsingi, kwa sasa ni miongoni mwa vyama vitatu vikubwa vya siasa Tanzania, wakati kuna vyama vikongwe vilivyopo.
Leo ACT-Wazalendo (Bara) ukitazama, Kigoma bado imeshikilia maeneo ambayo zamani yalikuwa ni ya CUF, Mkoa wa Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara tumejiimarisha vya kutosha.
Hata mikoa ambayo hatukuwa na nguvu, kwa mfano Ruvuma, mikoa ya Kanda ya Ziwa, kule upande wa Magharibi tumejiimarisha.
Swali: Mnatumia mbinu gani kujijenga kiasi hicho?
Jibu: Moja tunalofanya ni kupanga safu za chama, kujenga muundo wa chama katika ngazi za matawi, kata, majimbo na mikoa. Tumefanya hivyo kuhakikisha hatuwi na uongozi unaoning’inia juu tu katika majimbo na mikoa, ila wenye misingi madhubuti katika matawi.
Kingine ni chama kujiimarisha kirasilimali kwa sababu shughuli za siasa zina gharama kubwa.
Katika kujiimarisha ni lazima uwe na rasilimali za ofisi, kufanya mikutano, kukagua utendaji wa chama kila mara na ikifika mahali watendaji wa chama tuwasaidie kuendesha shughuli za chama.
Nikiwa mjumbe wa kamati kuu, nashiriki vikao vya mikakati, naamini si miaka mingi ijayo ACT itakuwa na nguvu kubwa ya ushawishi Tanzania; kwa hiyo tuliposema The Future is Purple (yajayo ni zambarau) si tu kauli ya kujifurahisha, lakini ni kuhakikisha kiwe tegemeo kwa Zanzibar na Tanganyika.
Swali: Pamoja na kujijenga huko, mnalaumiwa mnaelekeza mashambulizi kwa wapinzani wenzenu, kuliko hata CCM?
Jibu: Si kweli. Hakuna wakati wowote ACT ikashambulia chama kingine, isipokuwa ni mapambano ya vijana huko mitandaoni. Ukweli ni kuwa, mara nyingi chama kimekuwa kikijibu mashambulizi tu.
Kwa muda mrefu, tumeshuhudia vijana wa (anataja chama) wakifanya kila mbinu kuipaka tope ACT-Wazalendo na kumchafua kiongozi wa chama, Zitto Kabwe.
Kuna watu maalumu wamewekwa, ukiposti kitu chochote wao wanakuja kushambulia ACT, wataandika maneno ya kuudhi ili uache hoja uliyokusudia uwajibu.
Lakini siwalaumu kwa sababu ni mchezo wa siasa, lakini ukiamua kuwachezea wenzako, halafu mchezo huo ukachezewa usilalamike.
Swali: Kuna madai nguvu yenu Zanzibar imeanza kushuka na hata katika matokeo ya uchaguzi mdogo wa Mtambwe (Pemba) hivi karibuni, kura za CCM zimeongezeka. Unasemaje?
Jibu: Kimsingi, tangu uchaguzi wa mwanzo kabisa wa mwaka 1995 kulikuwa na majimbo 21 Pemba na 29 Unguja, CCM haikupata hata jimbo moja Pemba, wakati huo chama kina miaka mitatu tu tangu kuanzishwa mwaka 1992.
Mwaka 2000 kulifanyika vurugu katika uchaguzi Pemba.
Tumefanya uchaguzi mwingine ambao unaweza kusema ulikuwa na afadhali wa mwaka 2005 hawakupata hata jimbo moja, 2010 hawakupata hata jimbo moja, 2015 ambao ulifutwa, hawakupata hata jimbo moja Pemba. 2020 hatuwezi kuutumia kuupimia kwa sababu tunaulalamikia.
CCM haiongezi nguvu, bali inazidi kupunguza. Naamini katika uchaguzi wa 2025 itapoteza zaidi kwa sababu mgombea wao amepoteza umaarufu.
Swali: Unasema amepoteza umaarufu, lakini tunaona kumekuwa na mabadiliko hasa katika ujenzi wa miundombinu.
Jibu: Kama ni kujenga majengo, nchi hii haijapata kuwa na wakati haijengwi. Kama kuna Rais aliyepata umaarufu kwa kujenga barabara basi ni Amani Karume, kwa sababu alipoingia alikuta barabara zimechakaa, akajenga kuunganisha maeneo.
Kwa mfano, zamani ukitoka Kaskazini kwenda Kusini ilikulazimu upitie hapa mjini, lakini sasa kuna barabara inayopita Wilaya ya Kati inayounganisha Kaskazini na Kusini.
Barabara za Pemba ambazo mpaka leo ukipita bado ni nzuri, zilijengwa na Wamarekani kupitia Mfuko wa Millennium Challenge Cooperation (MCC), zilisainiwa na Rais Karume na kuanza kujengwa wakati wake.
Swali: Lakini naye amejenga miundombinu?
Jibu: Unazungumzia ujenzi wa hospitali? Huduma za afya si majengo tu. Ni huduma ambazo mwananchi akizitaka anazipata.
Leo tunaona huduma za afya wamepewa sekta binafsi, ni takribani mwaka mzima, hakuna maboresho. Wanatumia majengo ya Serikali, vifaa vya Serikali, wanakusanya faida.
Ukienda katika elimu, anasema kajenga majengo. Wakati wa Rais mstaafu Dk Mohamed Shein, kulijengwa shule chungu nzima za ghorofa kutoka mkopo wa Benki ya Dunia.
Unazungumzia skuli za ghorofa, Wazanzibari si limbukeni wa skuli za ghorofa, hapa eneo la Mji Mkongwe, nimesoma skuli za ghorofa tangu msingi hadi sekondari.
Dunia nzima inataka huduma bora. Ukienda Uingereza katika kila uchaguzi mjadala mkubwa ni huduma za afya za Taifa (NHS), hata kwenye Bunge la Uingereza, mjadala mkubwa unaokula muda ni NHS, hawazungumzi majengo.
Jisifu kwamba kiwango cha elimu kimepanda Zanzibar, tuonyeshe sisi kwamba katika mitihani ya Taifa, skuli za Zanzibar zimepanda ziko juu, lakini leo katika skuli 10 zinazoongoza Tanzania nzima, umepata kuona hata moja kutoka Zanzibar?
Katika afya, sisi kama kisiwa tunapaswa kujilinganisha na Seychelles, Mauritius, au Cape Verde. Leo katika kipimo cha uchumi nchi zinazoongoza Afrika, zinazoongoza ni visiwa hivyo vitatu. Kipi kinaikwaza Zanzibar? Ni kwa sababu imekosa uongozi bora.
Unazungumzia ukarabati wa Uwanja wa Amani, si jambo kubwa. Uwanja ule ulipojengwa na Rais Abeid Karume, ulikuwa ndiyo unaongoza Afrika Mashariki. Televisheni ya kwanza ya rangi Kusini mwa Jangwa la Sahara ilikuwa Zanzibar wakati wa Mzee Karume. Yote hayo hayakuwa hoja.
Swali: Mngetarajia kupata nini katika utawala wa Rais Mwinyi?
Jibu: Moja kati ya masuala makubwa ni suala la Muungano, haki za Zanzibar katika Muungano, mambo ambayo Zanzibar imenyimwa katika Muungano. Wapo viongozi hata ndani ya Serikali walisimama na kutetea hilo. Kama huzungumzi hilo Wazanzibari hawawezi kukuelewa.
Swali: Kila unapofika uchaguzi mnalalamikia Tume ya Uchaguzi na mifumo, mwaka 2025 mmejipangaje?
Jibu: Kwanza katika nchi za Afrika tunajiandaa katika kila hali. Sisi tulipoamua kuingia katika SUK (Serikali ya Umoja wa Kitaifa), Maalim Seif aliweka masharti, yakiwamo namna ya kufanyika mfumo wa uendeshaji wa uchaguzi na taasisi nyinginezo.
Baada ya kuja Othman Masoud katika nafasi hiyo, naye akayafanyia kazi na kupeleka mapendekezo ya hatua ya kipi kifanyike.
Sasa hapo katikati kimeundwa kikosi kazi cha Zanzibar na baada ya kuweka shinikizo kumeundwa kamati ya CCM na ACT-Wazalendo yenye wajumbe watano kila upande na bahati nzuri mimi ni mmoja wa wajumbe wa chama chetu.
Lengo letu ni kuhakikisha kunafanyika mageuzi ili yale maeneo yanayolalamikiwa yarekebishwe kabla ya uchaguzi wa 2025.
Swali: Katika mikakati mnayoifanya, mnaamini itafanikiwa?
Jibu: Kila jambo lina wakati wake. Mimi ni muumini kwamba, katika dunia hii hakuna jambo lisilo na mwisho. Katika dunia hii kuna mambo ambayo watu hawakuyafikiria lakini yametokea. Kuna wakati fulani hakuna mtu aliyeamini ukomunisti utaporomoka katika kambi ya Mashariki, lakini ilifika mahali ukaporomoka ulipoanguka ukuta wa Berlin.
Hata Umoja wa Soviet (USSR) uliokuwa ukidhibiti mataifa madogo Ulaya Mashariki, hakuna aliyeamini kama utaanguka na zile nchi zitakuwa huru. Leo hii Estonia, Lithuania, Latvia, Georgia, nchi za Kazakhstan, Uzbekhstan, Kyrgyzstan, zote zilikuwa chini ya Soviet, lakini zimepata uhuru.
CCM si chama pekee cha ukombozi Afrika; tuliona Zambia UNIP ilishindwa, Malawi MCP imeshindwa. Naamini itafika wakati, ni suala la muda, hakuna chama kitakachotawala milele.