Mabanda ya Nanenane Mbeya kujengwa kwa mfumo wa vijiji

Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye kikao cha maandalizi ya sikuu ya wakulima Nane nena ambayo yatafanyika kikanda Mkoa wa Mbeya kuanzia Agosti Mosi mpaka kilele Agosti 8, 2025 .
Muktasari:
- Hatua hiyo imetajwa ni kuimarisha ulinzi na kutekeleza agizo la Wizara ya Kilimo hususan ujenzi wa lango kuu, uzio wa maduka, huku matarajio ni kukamilika Julai 30, 2025.
Mbeya. Katika kuelekea maonyesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane), Mkoa wa Mbeya umeandaa mikakati mipya ya ujenzi wa mabanda kwa mfumo wa vijiji.
Umesema lengo ni kutaka kuboresha ulinzi na kudhibiti usambaaji usio rasmi wa watu uwanjani, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Maonyesho hayo ya kikanda yanatarajiwa kufanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale kuanzia Agosti Mosi hadi 8, mwaka huu, yakihusisha washiriki kutoka taasisi binafsi na za Serikali.
Hatua hii imechukuliwa baada ya halmashauri na taasisi za Serikali za kanda kuanza kuvunja mabanda ya zamani na kujenga miundombinu mipya kwa mfumo wa vijiji.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Julai 8, 2025 na Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mbeya, Said Madito katika kikao cha maandalizi ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane itakayofanyika kikanda mkoani Mbeya.
Madito amesema maonyesho ya mwaka huu yatakuwa tofauti kwa sababu mfumo mpya wa mabanda ya vijiji, unalenga kuongeza tija kwa kuwaweka washiriki na wageni kwa utaratibu mzuri, kulingana na halmashauri zao na kuongeza usalama ndani ya uwanja kupitia usimamizi wa Wizara ya Kilimo.
“Halmashauri zote zitakazoshiriki maonyesho zimeshabomoa mabanda ya awali na kujenga mifumo ya vijiji, lengo ni kuongeza usalama wa ndani ya uwanja,” amesema.
Kuhusu mwamko wa ushiriki, Madito amesema mwitikio ni mkubwa na maonyesho ya mwaka huu yanatarajiwa kuwa ya kipekee kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Wizara ya Kilimo.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Ujenzi wa Uwanja wa Maonyesho wa John Mwakangale kutoka Wizara ya Kilimo, Elizabeth Mziray amesema maboresho ya miundombinu yataanzia kwenye lango kuu la kuingilia, uzio na maduka ya mbele ambapo ujenzi umefikia asilimia 22.
Amesema utekelezaji unatarajiwa kukamilika ifikapo Julai 30, 2025 huku akisisitiza kuwa mkandarasi yupo eneo la mradi na kazi zinaendelea.
Aidha, mfanyabiashara na mkulima, Witness Kamwela akizungumza na Mwananchi kando ya mkutano huo, ameiomba Serikali iboreshe zaidi miundombinu ili iwe rafiki kwa makundi yote, hasa maeneo yanayouza vyakula na maliwato ili kulinda afya sambamba na usalama wa raia na mali zao.