MAHOJIANO MAALUMU: Zitto aeleza mpango wa kung’atuka uongozi ACT Wazalendo

Kiongozi wa Chama cha ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza katika mahojiano maalumu na wahariri pamoja na waandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za MCL Jumanne Julai 19, 2022. Picha na Said Khamis
Muktasari:
- Baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili, Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, anatarajia kumaliza muda wake wa uongozi ndani ya chama hicho, huku akitoa mwelekeo kuwa atapisha wengine waendelee kwa mujibu wa katiba.
Dar es Salaam. Baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili, Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, anatarajia kumaliza muda wake wa uongozi ndani ya chama hicho, huku akitoa mwelekeo kuwa atapisha wengine waendelee kwa mujibu wa katiba.
Zitto, aliyeshika nafasi hiyo tangu Machi 29, 2015 na baadaye mwaka 2020 alipochaguliwa mara ya pili, amesema hana nia ya kuendelea na uongozi na kwa mujibu wa katiba lazima atii matakwa yake.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika majuzi, alisema katiba ya chama hicho haimruhusu mwanachama yeyote kuwa kiongozi zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja.
“Kwa hiyo mimi sasa hivi namalizia kipindi changu cha pili. Machi 2024 lazima kuwe na kiongozi mwingine wa chama cha ACT-Wazalendo, lazima, kwa sababu tumejiwekea huo utaratibu,” anasema.
Kwa kuwa ndiye kiongozi wa kwanza wa chama hicho, Kabwe anasema ni wajibu wake kupisha wengine na kwamba kufanya hivyo kutawafanya wanaokuja wasing’ang’anie.
“Mimi nikiheshimu katiba akaja mwingine maana yake tutakuwa tumeweka msingi kwamba yeyote atakayekuja atafuata,” anasema.
Anachokumbuka kama kiongozi
Zitto, aliyewahi kuwa mbunge kwa miaka 15, anasema mauaji ya wanachama zaidi ya 20 yaliyotokea Zanzibar ni moja ya vipindi vigumu alivyowahi kuvipitia katika uongozi wake.
Kutokana na hali hiyo, anasema idadi kubwa ya watu walitaka kuondoka nchini kwa hofu ya kukamatwa baada ya maandamano.
Alisema katika kipindi hicho balozi nne zilimtaka aondoke nchini zikihofia usalama wake.
“Kulikuwa na shinikizo kubwa, balozi kama nne hivi zilikuwa zinasema tayari haupo salama ondoka, lakini naondoka na wanachama ambao zaidi ya 20 wameuawa Pemba, una mzee kiongozi ambaye yupo Zanzibar (Maalim Seif Sharif Hamad) huwezi kumuondoa.
“Una viongozi ambao wako hospitali wakati ule mheshimiwa Jussa (Ismail) alikuwa hospitali baada ya kupigwa na polisi Zanzibar, una Nassor Mazrui hajulikani alipo, nilikataa kwa kweli nilisema lazima tukamilishe mchakato wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” anaeleza.
Lakini, alisema hicho ndicho kipindi ambacho amejifunza zaidi siasa kuliko chochote alichowahi kupitia.
Akizungumzia baadhi ya viongozi wa vyama kung’ang’ania madaraka, alisema wanapaswa kujitathmini akisisitiza ni wajibu wao kuandaa viongozi wengine watakaoshika nyadhifa hizo.
Kiongozi huyo ambaye kitaaluma ni mbobezi wa uchumi, anasema chama cha siasa kinapaswa kuhakikisha wanachama wanakuwa na haki, chaguzi zinafanyika na viongozi wanachaguliwa bila misuguano.
“Unaweza ukafa, unaweza ukakosa nguvu hiyo, ulianzisha taasisi kwa ajili yako? Wengine wakiwepo ni wajibu wako kuwaandaa ili atakayechukua aendeleze ile misingi,” anasema.
Demokrasia ya kupewa
Hata hivyo, Kabwe alibainisha kuwa kukosekana kwa demokrasia ndani ya baadhi ya vyama vya siasa, ni matokeo ya kile alichokiita demokrasia ya kupewa inayotumika nchini.
Katika maelezo yake hayo, alisema badala ya demokrasia kutokana na madai ya wananchi, kwa bahati mbaya dola iliongoza mchakato na kuitoa kulingana na inavyohitaji.
“Dola inachotazama ni chama tawala kuendelea kuwa madarakani, haijali nini kinatokea kwenye vyama vingine, sababu inaona hapatakuwa na chama kingine kitakachoingia madarakani,” anasema.
Kungekuwa na mazingira yanayowezesha vyama vingine kushika dola, alisema hata uthibiti wa dola kusimamia demokrasia ya vyama vingine ungekuwepo.
Alikosoa mazingira hayo, akisema yanahatarisha mwenendo wa nchi iwapo chama kingine kitaiongoza, kwa kuwa havitakuwa na watu wenye uwezo wa kuongoza Taifa.
“Mfumo wetu ni kwamba CCM ndiyo itakayoongoza, jambo ambalo si sahihi. Ipo siku itatoka madarakani na hatari yake tunaweza kukosa watu wenye kaliba ya kuongoza nchi kwa kuwa si jambo dogo,” anasema.
Anashauri dola kuwa na matamanio ya kuhakikisha chama chochote kitakachopata nafasi ya kuiongoza nchi kinafanya hivyo, kwa usalama na Taifa linakwenda vema.
Alisema iwapo mazingira mazuri yatawekwa, CCM itaondoa itikadi yake ya kuongoza na kufikiria ushindani katika chaguzi mbalimbali.
“Ndiyo maana tunadhania kwamba ukiwaondoa polisi, CCM hawapo kwa sababu kuna wakati CCM wenyewe hawafanyi siasa, ni kutumia wasimamizi wa uchaguzi, usalama wa taifa, polisi sasa mazingira kama hayo inawafanya wasiendeleze itikadi ya kushindana na wengine kwenye kura,” anasema.
Amsifu Samia
Katika hatua nyingine, mwanasiasa huyo alieleza kuridhishwa na hatua ya sasa ya Rais Samia, akisema ameonyesha mwelekeo katika utekelezaji wa matakwa ya wananchi.
Anasema kwa sasa kumekuwa na mwelekeo katika upatikanaji wa Katiba mpya kutokana na utashi unaoonekana kwa Rais Samia.
Imani yake kwa kiongozi huyo, alisema inatokana na kuupeleka mjadala huo katika Kamati Kuu ya CCM, hivyo mchakato kupata baraka za chama hicho, tofauti na ilivyokuwa wakati wa uongozi wa awamu ya nne chini ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
“Kikwete alisimama akasema kwa kuwa mimi ni rais wa wote natamka kwamba mchakato wa Katiba mpya uanze, ni kama aliruka bila kuagana na nyonga,” alisema.
Pamoja na nia njema ya Samia, Kabwe alisema ni vema wanasiasa wamtie nguvu mkuu huyo wa nchi kwa kuwa ndani ya CCM kuna makundi mengi yasiyopenda mabadiliko hayo.
“Kuna wale waliozoea vya kunyongwa vya kuchinja hawawezi, tunafanya hivi wakati bungeni kuna wabunge 84 waliopo huko bila kushinda, kwa vyovyote hawawezi kukubali mabadiliko ya Katiba,” anasema.