Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bado ngoma nzito KKKT Konde, maaskofu wapishana

Muktasari:

  • Baadhi ya maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wametoa maoni yao kuhusiana na kuvuliwa uaskofu kwa Askofu wa Dayosisi ya Konde, Dk Edward Mwaikali wakisema kuna jambo haliko sawa ndani ya kanisa.

  

Moshi. Baadhi ya maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wametoa maoni yao kuhusiana na kuvuliwa uaskofu kwa Askofu wa Dayosisi ya Konde, Dk Edward Mwaikali wakisema kuna jambo haliko sawa ndani ya kanisa.

Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki mkoani Tanga, Dk Stephen Munga akienda mbali na kuainisha maswali nane juu ya mkutano uliomvua uaskofu Dk Mwaikali, alisema KKKT inabomolewa na majungu, visasi na hila.

Hata hivyo, Mwananchi jana lilizungumza na Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Fredrick Shoo kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwake na kujibu kuwa punde itatolewa taarifa rasmi ya utaratibu mzima uliofanyika kutekeleza hicho kilichotokea.

“Kwa sasa sina cha kusema ila tutakuwa na taarifa rasmi juu ya zoezi lilivyofanyika hadi kufikia hapa,’’ alisema Askofu Shoo.

Mwananchi pia lilizungumza na Katibu mkuu wa zamani wa KKKT kwa miaka 16, Amani Mwenigoha ambaye alimpongeza Askofu Shoo kwa kuchukua hatua aliyoiita ni muhimu na stahiki katika mgogoro huo, akisema ni uongozi shupavu.

‘‘Mkuu wa kanisa ni mwangalizi au msimamizi mkuu wa maisha na kazi za kanisa zima nchini,” alisema Mwenigoha na kuongeza:

“Hawezi kufunga mikono akiangalia kanisa linakosa amani na Injili ya Kristo Yesu haihubiriwi katika mazingira yenye utulivu na amani.

“KKKT popote lilipo duniani na kipekee hapa Tanzania ni kanisa la kijamii katika maana ya mfumo wake wa uongozi, kwa maana ya maaskofu na wasaidizi wa maaskofu wanapatikana kwa njia ya kupigiwa kura,” alisema Mwenigoha.

Alisisitiza: “Kwa kawaida halmashauri kuu zao huchuja na kuwasilisha kwenye mikutano mikuu kwa kura ya mwisho. Kwa lugha nyepesi mamlaka ya ajira ya askofu ni mkutano mkuu wa dayosisi yake.’

“Ikitokea Wakristo kwa njia ya mkutano mkuu wa dayosisi yao wamepiga kura ya kukosa imani na askofu wao, basi askofu husika anapoteza uhalali wa kiimani au kimapokeo na kisheria na hivyo hawezi kuendelea kuongoza dayosisi hiyo. Yaani kwa kifupi hawezi kuendelea kuongoza dayosisi kwa kujificha kwenye kichochoro chochote cha katiba ya dayosisi husika au katiba ya kanisa zima.”

Askofu Mwaikali alivuliwa uaskofu katika mkutano mkuu maalumu ulioitishwa Machi 22, 2022 jijini Mbeya na Askofu Shoo kama njia ya kumaliza mgogoro uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja katika dayosisi hiyo.

Mgogoro huo umeshuhudia wachungaji 17 wa dayosisi hiyo wakitimuliwa kwa madai ya kuchochea mgogoro kwa kupotosha uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya dayosisi kutoka Tukuyu kwenda usharika wa Ruanda jijini Mbeya.

Baada ya uamuzi wa kumvua uaskofu baada ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye, mkutano huo ulimchagua Geofrey Mwakihaba kurithi mikoba yake.

Hata hivyo, Dk Mwaikali alisema mkutano huo ni batili na uamuzi wake ni batili.

“Mimi sikuhudhuria huo mkutano kwa sababu nilikuwa siutambui kwanza na hili nilishalisema tangu mwanzo. Nimesikia tu kwamba maamuzi ni hayo sijaambiwa rasmi. Wakishaniambia nitakuwa na neno la kusema,” alisema Askofu Mwaikali.

“Kimsingi, mkuu wa KKKT amewatwisha laana wana dayosisi ya Konde kwa sababu amekwepa kuwa mwenyekiti wa mkutano aliouitisha mwenyewe bila kushirikisha halmashauri kuu ya KKKT Konde. Amenawa mikono kama alivyofanya Pilato,” alisema Askofu Mwaikali.


Tamko la Halmashauri ya Konde

Hata hivyo, jana Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Konde ilisema inategemea hekima ya Mungu kumaliza mgogoro huo.

Ilisema haina imani na kiongozi mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Shoo kwenye kuhusika na utatuzi wa mgogoro huo.

Wakitoa tamko la pamoja la halmashauri kuu ya dayosisi na umoja wa vijana jana, mjumbe wa halmashauri kuu hiyo, Wilfred Chomo alisema kinachoonekana sasa, Askofu Shoo anaegemea upande mmoja katika kusuluhisha mgogoro huo.

Chomo alisema kanisa lina viongozi wengine ambao ni maaskofu wenye uwezo unaoweza kutumika kutatua mgogoro huo badala ya Dk Shoo.

Alidai uamuzi wa mwisho wa kumfukuza Askofu Mwaikali ulitolewa na Askofu Shoo, pasipo viongozi wa halmashauri kupatiwa hadidu za rejea, hivyo hawakushiriki.

“Mkutano na maamuzi yote yaliyofanyika kwenye Usharika wa Uyole tarehe 22, Machi mwaka huu, ulikuwa batili na kinyume cha katiba ya dayosisi toleo la mwaka 2006, pia ni kinyume cha katiba ya Kanisa toleo la mwaka 2015,” alidai Chomo.

Aliongeza kuwa wajumbe walioitishwa katika mkutano huo nao walikuwa batili kwa kuwa hawatambuliwi kwa mujibu wa katiba.

Katibu wa umoja wa vijana dayosisi hiyo, Mutambala Peter alisema usuluhishi uliofanywa na Dk Shoo umechochea zaidi mgogoro.

“Mgogoro huu umetugawa vipandevipande wanaKonde, tumeshtushwa na kusikitishwa na uamuzi wa ajabu uliofanyika katika mkutano batili ulioitishwa na mkuu wa kanisa katika ushirika wa Uyole,” alisema.


Maaskofu KKKT wafunguka

Askofu wa Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Ambele Mwaipopo alisema mkutano huo mkuu maalumu ulioitishwa na mkuu wa Kanisa sio sawa na kudai mkuu wa Kanisa amepoka mamlaka ya kikatiba ya Askofu Mwaikali.

“Kwa sababu nazifahamu katiba zote mbili ya Konde na ya KKKT, ni kwamba kilichotokea Konde hakiko sawasawa kwa sababu kila dayosisi ina autonomy (ni huru na zina mamlaka kamili) ya kujiendesha zenyewe,” alisema Askofu Mwaipopo.

“Katiba zao zina namna ya kumuingiza askofu na kuna vyombo vya kikatiba ambavyo hata katiba ya KKKT inavitaja. Kila dayosisi itakuwa na katiba yake, itakuwa na vyombo vyake vya maamuzi, alieleza.

Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza alisema kwa muundo wa KKKT, Askofu hajawahi kumfukuza au kumvua askofu mwingine, kwani huingia kwa mchakato na kuondoka kwa mchakato.

“Karibu mabaraza yote ya maaskofu wa kiprotestanti duniani hufuata kanuni ya the first among the equals (wa kwanza aliye sawa na wengine). Hata aliyewekwa wakfu jana ni sawa na aliowakuta,” alisisitiza Askofu Bagonza na kuongeza:

“Kwa utaratibu wa “kiundugu na kirafiki” heshima ya u-rika hufuatwa wakiwa wenyewe ndani, lakini u-rika haumpi yeyote nafasi ya ziada juu ya wengine”.

“Kilichotokea Konde ni kama hakikutokea. Historia ya kanisa haikunyooka, imejaa mabonde na milima, damu na kusalitiana. Hili litapita na kanisa litasimama. Kristo ndiye Mkuu wa Kanisa,” aliongeza kusema Askofu Bagonza.


Maswali manane ya Munga

Katika andiko lake alilolituma kwa Mwananchi jana, Munga aliuliza maswali manane kuhusiana na mkutano mkuu maalumu uliomuondoa Askofu Mwaikali, moja akihoji katiba halali ya KKKT inayotumika nyakati za sasa ni ya mwaka gani.

Pia amehoji ni vifungu vipi vya katiba ya KKKT na ya dayosisi ya Konde vimetumika kuhalalisha Mkuu wa KKKT kuitisha mkutano mkuu uliofanyika Konde badala ya askofu wa dayosisi ambaye ndiye mwenyekiti wa mikutano mikuu ya dayosisi.

Munga amehoji pia sababu za Askofu Shoo kuitisha mkutano huo bila ridhaa ya Askofu wa Dayosisi ya Konde wala ridhaa ya halmashauri kuu yake na kuhoji pia kuhusu akidi na kuhoji nani aliwateua wajumbe waliohudhuria.

Kwa mujibu wa Dk Munga, maaskofu walikwishapanga kufanya kikao chao Dodoma Machi 28 na kuhoji kwa nini Mkuu wa Kanisa hakusubiri mkutano huo na kuzungumza na maaskofu wenzake kwanza kabla ya kuchukua maamuzi.

Katika majumuisho yake, alisema kwa mtu mwenye akili za kawaida atatambua kuwa KKKT inabomolewa na majungu, visasi na ulinzi wa maslahi binafsi na kuhoji: “Iko wapi nguvu ya utume na ushuhuda wa Injili ya wokovu?”

Munga alihoji kuwa KKKT imepoteza waumini wangapi kwa ajili ya migogoro na viongozi kutumika na kutumiwa vibaya na kulitaka Kanisa kutafakari kwa maombi ili Bwana awape ujasiri maaskofu kutengeneza mambo yaliyobomoka.