Bajeti Utumishi yapaa, kilio cha ajira chatawala

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akiwasilisha maombi ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2023/2024 leo bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo.

Muktasari:

Dodoma. Bajeti ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imepanda kutoka Sh851.08 bilioni mwaka 2022/23 hadi Sh1 trilioni mwaka 2023/24, ikielezwa itawezesha vyombo vinavyosaidia kwenye maamuzi ya nchi, usalama na kuimarisha vita dhidi ya rushwa.

Bajeti ya Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, imepanda kutoka Sh741.29 bilioni mwaka 2022/23 hadi Sh860.18 bilioni, mwaka 2023/24.

Mbali na hilo, Serikali imepanga kutoa vibali vya ajira ili kujaza nafasi 43,464 zilizoidhinishwa katika ikama kwenye mwaka 2023/24.

Mwaka 2022/23, Serikali ilitoa vibali vya ajira mpya 30,000 na vibali vya ajira mbadala 7,721 kwa waajiri kutoka katika taasisi mbalimbali vilitolewa.

Akiwasilisha mapato na matumizi ya ofisi hiyo jana bungeni, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, alisema kupitisha bajeti ya ofisi hiyo ni kuchangia katika uimarishaji na uwezeshaji wake vyombo hivyo na malengo yake kwa Taifa.“Serikali itayapa kipaumbele maeneo ya usimamizi wa rasilimali watu na rasilimali fedha.

Vilevile, bajeti itaiwezesha Serikali kupandisha vyeo watumishi, ubadilishwaji wa kada au muundo wa utumishi na kulipa malimbikizo ya mishahara ya watumishi na kutoa ajira mpya,” alisema.

Simbachawene alisema kupitishwa kwa bajeti hiyo ni njia ya kuimarisha na kuchangia kukuzwa kwa maadili kwa viongozi wote na watumishi wa umma kwenye nchi, hivyo kupata tija ya rasilimali watu na rasilimali fedha kwa kuwa na matumizi yenye tija ya rasilimali hizo kwa wakati wote.

Kuhusu mchakato wa sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rishwa, Simbachawene alisema mchakato huo unaendelea na maoni kutoka kwa wadau yamekusanywa.

Alisema rasimu ya waraka wa Baraza la Mawaziri imeandaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri.

 Zaidi ya nusu wakosa ajira

Simbachawene alisema ofisi yake ilifanya usaili wa ajira za muda kwa niaba ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa nafasi za wasimamizi wa maudhui, wasimamizi wa Tehama na makarani wa sensa.

Alisema jumla ya maombi 689,935 yalipokewa na waombaji 612,023 waliitwa kwenye usaili, kati ya hao, waombaji 205,000 walifaulu na kupangiwa vituo vya kazi.

Akichangia hoja, mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi alisema kwenye kada moja ya ualimu kuna vyuo 31 vya ualimu vya Serikali katika ngazi ya stashahada ambavyo hudahili wanafunzi 400 kwa mwaka na hivyo ukichanganya na vyuo binafsi 23 jumla wanakuwa 23,000.

Alisema kwa miaka mitatu wanafunzi wa vyuo hivyo watakuwa 75,000, hivyo ukichanganya na vyuo vikuu 56,183 inafanya jumla ya wanafunzi kufikia 131,183.

Alisema ajira zilizotoka hivi karibuni katika kada za ualimu na afya ni 21,200, wastani wa kada ya ualimu wanaohitajika ni 12,000 na kuhoji wanafunzi wanaomaliza kwenye vyuo hivyo watapelekwa wapi.

“Kuna umuhimu gani wakuendelea kuzalisha walimu kama kwenye soko hatuwahitaji? Ifike mahali tupunguze utitiri wa vyuo hivi vinavyotoa elimu ya kada ya ualimu ili watoto wetu wakasome masomo ambayo watakapokwenda katika soko wataweza kuyafanyia kazi,” alisema.

Mbunge wa viti maalumu, Ester Matiko alisema hadi sasa Tanzania ina upungufu wa zaidi ya watumishi wapatao 82,000 kwenye sekta ya afya.

“Nimepitia katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 ambayo imeainisha kuwa kuongezeka kwa wafanyakazi wa sekta ya afya kutoka 82,000 hadi kufikia 100,000 mwaka 2020.

Ina maana walioongezeka ni wafanyakazi 18,000 tu,” alisema.Alisema kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Watanzania wako milioni 61, hivyo kwa uwiano bila kujali taaluma aliyonayo mtumishi wa sekta ya afya, anatakiwa kuhudumia watu 610,000.

 Alilia faragha za viongozi

Katika hatua nyingine, Mbunge wa viti maalumu (CCM), Janejelly Ntate aliishauri ofisi hiyo kuirejesha ‘Leaders Club’ iliyokuwa inalinda hadhi na faragha za viongozi mbalimbali nchini wasiadhirike wanapotaka ‘kumwagilia moyo’.

“Viongozi wetu tunasema mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi na ninyi waheshimiwa wabunge. Kwa nini inaonekana labda viongozi wa sasa hivi hawana maadili, ni kwa sababu tumewaondolea haki yao ya faragha,” alisema Ntate.

“…Hakukutoi kwenye raha zako nyingine, lakini zamani mlikuwa na faragha, mlikuwa na Leaders Club, mlikuwa mikoani mna sehemu za kukaa viongozi, ninyi wenyewe kwa wenyewe, kwa hiyo pale ukikaa hata ukiburudika na bia moja ukadondoka wanakubeba viongozi wenzako na hutalisikia mtaani.

”Alisema kutokuwa na mahali pa kukaa wakafanya faragha zao limeonekana kama hakuna maadili, lakini ukweli ni kwamba maadili ni yaleyale na watu ni walewale.

“Sasa niwaombe Leaders Club ikarudi menejimenti ya utumishi wa umma. Hapa Dodoma mjenge Leaders Club ya viongozi kwenda kupumzika baada ya saa za kazi,” alisema.

Maoni ya kamati

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Florent Kyombo alisema upo umuhimu wa wakala wa ndege za Serikali kupunguziwa majukumu, hasa ya umiliki wa ndege zilizokodishwa kwa ATCL.

Alisema hatua hiyo itawezesha uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ulete tija.

“Serikali ihamishe umiliki wa ndege zilizokodishwa kwa Kampuni ya Ndege Tanzania, kutoka kwa Wakala wa Ndege za Serikali kwenda kwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL),” alisema.