Bajeti ya kulipa deni la Taifa

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/2022, jijini Dodoma jana. Mwigulu ameliomba bunge lititishe bajeti ya wizara hiyo kiasi cha Sh12.9 trilioni. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Wakati Wizara ya Fedha na Mipango ikitenga Sh10.673 trilioni kwa ajili ya kulipa Deni la Taifa na huduma nyinginezo katika mwaka wa fedha 2021/2022, Kamati ya Bunge ya Bajeti imesema fungu la deni la Serikali linahudumia huduma nyingine ambazo hazipo kikatiba.


Dodoma. Wakati Wizara ya Fedha na Mipango ikitenga Sh10.673 trilioni kwa ajili ya kulipa Deni la Taifa na huduma nyinginezo katika mwaka wa fedha 2021/2022, Kamati ya Bunge ya Bajeti imesema fungu la deni la Serikali linahudumia huduma nyingine ambazo hazipo kikatiba.

Hayo yalielezwa Bungeni baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kuwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2021/22.

Dk Nchemba alisema wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa Sh12.961 trilioni, ambapo Sh11.935 trilioni kati ya hizo ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh1.025 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Dk Mwigulu alisema mwaka jana, wizara hiyo iliidhinishwa Sh10.477 trilioni kwa ajili ya deni la Taifa na huduma nyinginezo ambapo hadi kufikia Aprili mwaka huu zilikuwa zimelipwa Sh7.426 trilioni.

Alisema hadi kufikia Aprili mwaka huu wizara hiyo ilikuwa imelipa deni lote la Serikali lililoiva lenye thamani ya Sh6.84 trilioni.

Alisema kati ya kiasi hicho, deni la ndani ni Sh4.10 trilioni, likijumuisha riba ya Sh1.42 trilioni na mtaji Sh2.68 trilioni.

Aidha, alisema deni la nje ni Sh2.74 trilioni, ikijumuisha riba ya Sh0.63 trilioni na mtaji Sh2.11 trilioni.

Alisema tathmini ya uhimilivu wa deni ya Novemba 2020 inaonyesha viashiria vya deni la Serikali vipo ndani ya wigo unaokubalika kimataifa katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

Hata hivyo, akisoma maoni ya kamati baada ya hotuba ya Mwiguli, Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Bajeti, Omary Kigua alizitaja huduma nyinginezo kuwa pamoja na mafao kwa wastaafu wanaolipwa na hazina na mchango ya Serikali katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ambazo zinapaswa kutengwa na Deni la Serikali.

“Ni maoni ya kamati kuwa, ili kupata uhalisia wa bajeti ya kugharamia Deni la Serikali, Fungu la 22 lishughulikie tu masuala ya madeni na hizo huduma nyingine zielekezwe katika mafungu yanayofanana na majukumu husika au huduma hizo ziundiwe mafungu mapya,” alisema.

Kwa upande mwingine, akitoa maoni yake kwa gazeti hili, Mkurugenzi wa taasisi ya Utafiti wa kuondoa umasikini (Repoa), Dk Donald Mmari ameshauri kuwepo umakini katika mikopo ili kudhibiti deni la Serikali.

“Deni lazima litakuwepo, hata ukiangalia kwenye ripoti za kampuni, madeni ya muda mrefu lazima yawepo, maadamu unaendelea kufanya kazi, deni lazima liwepo, cha msingi ni kwamba lazima lilipwe, usipolipa unaingia kwenye janga la kutokukopeshwa.

“Tukope kwa matumizi sahihi na mikopo yenye riba nafuu. Hakuna nchi duniani ambayo haikopi. Maadamu uchumi una uwezo, unakopa unawekeza unajenga uwezo wa nchi kuzalisha kwa kujenga miundombinu, lakini kusema mikopo itakwisha, maana yake nchi haiishi tena,” alisema.

Washirika wa maendeleo

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu alisema kwa mwaka 2020/21, washirika wa maendeleo waliahidi kuchangia katika bajeti ya Serikali Sh2,874.37 bilioni.

Alisema kati ya kiasi hicho, Sh949.32 bilioni ni misaada na Sh1,925.04 bilioni ni mikopo nafuu.

Waziri huyo alisema hadi Aprili 2021, washirika wa maendeleo wametoa Sh1,894.96 bilioni, sawa na asilimia 70 ya makadirio ya kipindi hicho, ya kuchangia Sh2,692.0 bilioni.

Alisema kati ya kiasi hicho, misaada ya kibajeti ni Sh210.24 bilioni, sawa na asilimia 100 ya makadirio ya kipindi hicho, miradi ya maendeleo Sh1,454.72 bilioni sawa na asilimia 64 ya makadirio ya Sh2,287.98 bilioni na mifuko ya kisekta Sh230.0 bilioni sawa na asilimia 87 ya makadirio ya Sh265.69 bilioni ya kipindi hicho.

Mikopo iliyopatikana

Dk Mwigulu alisema katika mwaka 2020/21, wizara ilipanga kusimamia na kuratibu upatikanaji wa mikopo ya jumla ya Sh4,949.25 bilioni kutoka katika soko la fedha la ndani ili kuziba nakisi ya bajeti.

Akifafanua, alisema hadi Aprili 2021, wizara imefanikisha upatikanaji wa mikopo ya jumla ya Sh3,992.71 bilioni, sawa na asilimia 95.7 ya lengo la kukopa Sh4,170.01 bilioni katika kipindi hicho.

Alisema kati ya kiasi hicho, Sh2,675.63 bilioni zimegharamia mikopo ya ndani iliyoiva na Sh1,317.08 bilioni zimeelekezwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Aidha, Serikali ilipanga kukopa Sh3,035.6 bilioni kutoka vyanzo vya nje vyenye masharti ya kibiashara kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema hadi Aprili 2021, wizara imefanikisha upatikanaji wa mkopo wa Sh1,683 bilioni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Michango ya wabunge

Alipopata nafasi ya kuchangia Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee aliitaka Serikali kukubaliana na maoni ya Kamati ya Bunge ya Bajeti ya kuweka ukomo wa muda kufanya uhakiki wa madeni ya wakandarasi ili waweze kulipwa kwa wakati.

Alisema Serikali imekuwa ikijificha katika kichaka cha kufanya uhakiki katika kulipa madeni hayo, jambo ambalo linawaumiza wakandarasi na kuongeza riba kwa Serikali.

Sillo Baran (Babati Vijijini-CCM) alishauri kuongeza wigo wa ulipaji kodi na kuongeza idadi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), kuimarishwa kwa mifumo ya Tehama katika kuimarisha ukusanyaji na utoaji wa taarifa ili kuongeza upatikanaji wa kodi

Kirumbe Ngenda (Kigoma Mjini-CCM) alisema mabenki hayajawa katika mwelekeo mzuri wa kuisaidia sekta binafsi kutokana na riba kubwa ambayo imekuwa mzigo kwao na kutaka Serikali kuangalia eneo hilo.

Dk Charles Kimei (Vunjo-CCM) aliitaka Serikali kuangalia jinsi watakavyoweza kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma kwa sababu katika bajeti za wizara zote hajaona ongezeko hilo.

Mbunge wa Kisesa (CCM) Luhaga Mpina aliitaka wizara hiyo kufuatilia kama kushuka kwa makusanyo yanayosemwa na baadhi ya wizara yamesababishwa na ugonjwa wa corona kweli ama kuna sababu nyingine iliyosababisha jambo hilo.

Abbas Tarimba (Kinondoni-CCM) alimshauri Dk Mwigulu kuweka historia kwa kuwafukuza kazi wale wote walioko kwenye mnyororo uliotajwa ilivyotajwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuchota fedha wizarani kwake.