Bakwata ilivyokoleza mjadala umri sahihi wa binti kuolewa

Dar es Salaam. Mjadala umeibuka upya kufuatia maoni yaliyotolewa na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) kuhusu umri wa kuolewa ikipendekeza mtoto aliyevunja ungo aruhusiwe kuolewa hata kama hajafikisha umri wa miaka 18.

Kwa maoni hayo, ni kwamba Baraza hilo halikubali marekebisho Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inayoruhusu mtoto wa kike kuolewa chini ya akiwa na umri wa miaka 15 au miaka 14 kwa kibali cha mahakama, suala ambalo limepigiwa chapuo kwa muda mrefu ndani ya nje ya mahakama.

Sheria hiyo imekuwa ikipingwa na wanaharakati wa haki za watoto na wanawake wakidai inamnyima mtoto wa kike haki ya kupata elimu na kuwa utekelezaji wa sheria hiyo unakinzana na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inayomtambua mtoto hadi umri wa 18 na tayari kuna maelekezo ya mahakama ya kutaka ibadilishwe.

Machi 22, mwaka huu akiwasilisha maoni ya Bakwata mbele ya wajumbe wa Tume ya Haki Jinai, mwanasheria wa baraza hilo, Hassan Fatiu alipendekeza mtoto mwenye umri wa miaka 11, 12 au 13 aliyeingia kwenye kipindi cha balehe aruhusiwe kuolewa kwa uhalali wa mahakama utakaozingatia vielelezo vya kimazingira.

“Mtoto wa kike ana miaka 11, 12 hajaendelea na elimu, kwa nini asiolewe? Ukimuacha huyu ni matokeo ya kupata mimba mtaani, simaanishi kila mtoto wa umri huo aruhusiwe kuolewa, ila mhakama itajiridhisha afya yake, mazingira na mengineyo.

“Sisi tumependekeza sheria ibakie kama ilivyo na hatulazimishi kila mwenye umri huo aolewe. Kwa yule atakayeoa umri huo kabla ya mahakama kuthibitisha basi ahesabike kutenda kosa,” alisema Fatiu.

Rebecca Gyumi, mwanaharakati na mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali, Msichana Initiative linalotetea haki za wasichana kupata elimu, ameonyesha kutofurahishwa na maoni hayo ya Bakwata akieleza kuwa yanarudisha nyuma jitihada ambazo zimeshafanyika kupinga ndoa za utotoni.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rebeca ameandika, “Wasichana hawalindwi dhidi ya vitendo vya ngono kwa kuwaoza. Jukumu letu la malezi na kuwapa elimu sahihi ya afya ya uzazi kama wazazi, walezi na Taifa kwa ujumla tusilihamishie kwenye kuwaoza katika umri mdogo.

“Mtoto anabaki kuwa mtoto bila kujali anakusumbua kiasi gani, awe shule au nje ya shule anabaki kuwa ni mtoto. Kuwa shule hakumfanyi mtoto awe mtoto zaidi ya yule aliyeko nje ya shule. Wote wanahitaji kufurahia utoto wao,” alisema.

Julai 8, 2016 Mahakama Kuu ilitoa hukumu katika kesi aliyofungua Rebeca ikikubali kwamba vifungu vya sheria ya ndoa vinavyoruhusu kuolewa katika umri mdogo vinapingana na Katiba ya nchi kwa kuweka umri tofauti wa kuoa au kuolewa kati ya mtoto wa kike na wa kiume.

Mahakama hiyo iliitaka Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu kujipanga kuvirekebisha ndani ya mwaka mmoja.

Rebeca katika kesi hiyo alikuwa anapinga vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya ndoa vinachoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 14 kwa kibali cha mahakama; na miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi.

Katika kuchangia mjadala huo kwenye Twitter, Luko Kennedy anasema, “Tuachane na Bakwata, turudi tu kwenye akili ya kawaida, umeshasema ni mtoto, then (halafu) aolewe. Haiingii akilini mtoto wa miaka 11, 12 bado hajapevuka kiakili na kufanya maamuzi binafsi, ndio maana hata ukifanya naye mapenzi ni kosa na huruhusiwi hata kumuajiri afanye kazi yoyote.

“Sheria ya Mtoto ya Tanzania ya mwaka 2009 inatambua mtoto kama mtu yeyote chini ya umri wa miaka 18. Hivyo, kisheria, mtoto ni yeyote ambaye hajatimiza umri wa miaka 18 nchini Tanzania. Sheria hii inalenga kulinda haki na masilahi ya watoto, ikiwa ni pamoja na haki ya elimu, afya,” alisema.

Akichangia mjadala huohuo, Emmanuel Ndomondo alisema, “kuna mtoto na mkubwa kwa kigezo cha umri; pia kuna mtoto na mkubwa kwa kigezo cha balehe. Kwetu Tanzania tunaona umri wa miaka 18 na kuendelea tunakubaliana ni mkubwa, kupevuka kimwili na upevu wa ubongo, ni umri ambao mtu anaweza kubeba dhamana ya maisha yake, si ndoa tu na maisha mengine ya kijamii.

“Hata hivyo Bakwata wapo sahihi kwa mtazamo wa pili kuwa ukishabalehe wewe ni mkubwa kimwili, kibailojia, si mtoto tena. Unaweza kubeba mimba ukishiriki mapenzi ... lakini labda niwaulize, hawaoni haja ya kuzingatia kigezo cha umri, shule?” anahoji.

Akitoa maoni yake katika hilo, Dk Norman Jonas alisema hata kiafya mtoto mwenye umri wa miaka 14 anakuwa bado hajakomaa vyema kutosha kuolewa.

“Miaka 14 hata akiugua atalazwa wodi ya watoto, kwamba mkeo kaugua unaenda kumtembelea wodi ya watoto. Ni umri ambao kuna maeneo mengi ya ubongo, hasa yanayohusiana na hisia, busara hayajakomaa,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shura ya Maimamu Sheikh Issa Ponda alisema afya haiwezi kutumika kupanga umri wa kuolewa kwa sababu inatofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

“Sheria haiwezi kutungwa kwa kuzingatia kigezo cha afya kwa kuwa inategemea mtu na mtu, ukiweka miaka 14 unataka kusema kwamba kila atakayefikisha umri huo atabalehe wakati si sahihi wengine inaweza kuwa kabla au baada. Hapa hakuna haja ya kuweka umri, ni maumbile ya mwili ndiyo yazingatiwe.

Ponda alishauri kuwa kama mtoto aliyepata ujauzito anaweza kurejea shule baada ya kujifungua basi uwekwe utaratibu utakaoruhusu watakaoolewa nao kuendelea na masomo.

Kwa upande mwingine, akizungumzia msimamo wa Kanisa Katoliki, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima alisema mapendeko yao kwa Serikali ni kuifanyia maboresho Sheria ya Ndoa katika kipengele chenye utata wa umri kwa kuwa wanapingana na ndoa za utotoni.

“Sheria iliyopo ina mapungufu, tunaamini mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 anapaswa kuwa chini ya wazazi wake akiendelea kupata elimu na malezi. Mtoto wa kike ana haki ya kupata fursa ya elimu na kukua katika misingi ya malezi chini ya uangalizi wa wazazi wake hadi atakapofikisha miaka 18, atakaporidhia yeye mwenyewe kwamba anaingia kwenye taasisi ya ndoa.


Kauli ya Serikali

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alisema baada ya mahakama kutoa hukumu ya kufanyika kwa mabadiliko ya Sheria ya Ndoa, Bunge ambalo ndilo linahusika na utungaji wa sheria liliielekeza Serikali kukusanya maoni ya wananchi na wadau mbalimbali.

Alisema kazi hiyo ya ukusanyaji wa maoni ipo katika hatua za mwisho na matarajio ya wizara yake ni kuwasilisha bungeni katika Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuanza Aprili 4.

“Wakati sheria hii inatengenezwa miaka hiyo ya 70 ilifanyika kazi kubwa ya kukusanya maoni yaliyowezeshwa utengenezwaji wake, hivyo hata tunavyoibadili tusiondoe ile formula (kanuni) iliyotumika.

Hata hivyo, Mwanasheria Jebra Kambole alisema kinachoonekana kwa sasa ni Serikali kutoheshimu uamuzi wa mahakama, jambo ambalo ni ukiukwaji wa utawala wa sheria.

“Hakuna utashi wa kisiasa wa kufanya mabadiliko na kulinda mtoto wa kike, mahakama ilishatoa uamuzi kitendo cha kwenda kukusanya maoni wakati uamuzi umeshatolewa ni kuidharau mahakama. Tayari kuna kesi mbili zimefunguliwa kupinga hiki kinachofanywa na Serikali. Iwapo Tume ya Hakijinai itakubaliana na pendekezo hilo la Bakwata tutarudi mahakamani,” alisema.