Bakwata yaitaka Serikali ifafanue mashaka uwekezaji bandari

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa pamoja na viongozi wa Bakwata katika swala ya kitaifa ya Eid el Adh'haa iliyofanyika katika Msikiti wa Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco jijini Dar es Salaam. 

Muktasari:

  • Baraza la Waislamu Tanzania limeitaka Serikali kufafanua maeneo yanayotiliwa shaka kuhusu uwekezaji bandari.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuru Mruma ametoa wito kwa Serikali kupokea maoni ya wananchi kuhusu sakata la Bandari, huku akiitaka ifafanue maeneo yote yanayotiliwa shaka.

Hayo ameyasema leo Alhamis Juni 29, 2023 akihutubia Baraza la Eid El-Adh'haa lililofanyika katika Msikiti wa Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco jijini hapa.

"Pia Serikali inapaswa kutoa elimu kwa wananchi ili waendelee kuuelewa mradi huu (uwekezaji bandari)," amesema.

Mruma amesema kubainika kwa mradi huo kuliibua mjadala na taharuki kwa wananchi ambao hawakuwahi kuwa na taarifa sahihi kuhusu mradi huo.

Mruma ameitaka Serikali kupokea maoni ya wananchi na kutoa ufafanuzi kwenye maeneo yote yanayotiliwa mashaka.

Hiyo ni kauli ya kwanza kutoka Bakwata tangu uanze mjadala baada ya Serikali kusaini mkataba wa awali wa ushirikiano wa uwekezaji na uboreshaji bandari na Serikali ya Dubai kupitia kampuni ya Dubai Port World.

Hata hivyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia baraza hilo leo amesema Serikali itayafanyia kazi maoni yanayotolewa na wananchi kwa lengo la kuboresha zaidi huku akisistiza uwekezaji huo hauna lengo la kuiuza bandari kama watu wanavyosema.

“Naomba niwatoe hofu, Serikali yenu inawasikia na itayafanyia kazi. Tunawasikia wasomi, wanasiasa, wananchi wa Kawaida, lakini mjadala huu wa bandari usisababishe kutusambaratisha, sisi ni Watanzania wamoja lengo letu ni moja,”amesema.

Aidha, Majaliwa ameongeza kuwa atashirikiana na Waziri wa Uchukuzi katika utoaji wa elimu wa jambo hilo.

Sikukuu ya Eid El Adh'haa hufanyika kila mwaka na waumini wa dini ya Kiislamu wakiadhimisha Nabii Ibrahimu alipotaka kumtoa kafara mwanawe Ismail kwa amri ya Mwenyezi Mungu, lakini badala yake akaletewa Kondoo.

Kuchinjwa kwa Kondoo huyo na Nabii Ibrahim ndiko kulikofanya hadi sasa sikukuu hiyo iitwe kuwa ya kuchinja.