Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bakwata yawasimamisha masheikh watatu, yupo Walid Kawambwa

Muktasari:

  • Hatua hiyo imekuja wakati taasisi za kidini zikisisitiza umuhimu wa viongozi kuzingatia maadili, uwajibikaji na misingi ya uongozi katika kutekeleza majukumu yao kwa waumini na jamii kwa ujumla.

Dar es Salaam. Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limewasimamisha kazi masheikh watatu wa mikoa baada ya kubaini kuwa mwenendo wao unakiuka misingi ya uongozi wa kibaraza.

Hatua hiyo imefikiwa leo Jumanne Julai 14, 2026 katika kikao cha dharura cha Baraza la Ulamaa kilichoongozwa na Kaimu Mufti wa Tanzania ambaye pia ni Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania, Sheikh Ali Khamis Ngeruko.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya kikao hicho, waliosimamishwa ni Sheikh Walid Alhadi Omar Kawambwa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Issa Nasor wa Mkoa wa Singida na Sheikh Hassan Kiburwa wa Mkoa wa Kigoma.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa uamuzi wa kuwasimamisha umechukuliwa kutokana na mienendo inayokwenda kinyume na misingi ya uongozi wa kibaraza.

“Kikao cha dharura cha Baraza la Ulamaa kimeazimia kumsimamisha Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na mienendo inayokiuka misingi ya kiungozi ya kibaraza,” imeeleza taarifa hiyo.

Baada ya kusimamishwa kwa Sheikh Walid, Baraza limemteua Sheikh Abbas Ramadhani Abbasi, ambaye alikuwa mjumbe wa Baraza la Masheikh Mkoa wa Dar es Salaam, kuwa kaimu Sheikh wa mkoa huo.

Kwa upande wa Mkoa wa Singida, nafasi hiyo itakaimiwa na Sheikh Issa Simba, huku Mkoa wa Kigoma ukiongozwa kwa muda na Sheikh Uwesu Kiumbe.

Bakwata haijaeleza kwa kina aina ya mienendo iliyosababisha hatua hiyo ya kinidhamu, ikisema uamuzi umezingatia misingi na taratibu za uongozi wa taasisi hiyo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Katibu Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Ulamaa, Sheikh Hassan Chizenga amesema masheikh hao wamekwenda kinyume na maadili ya uongozi wa baraza.

“Ninachoweza kusema ni kweli hawa wamesimamishwa kwa kwenda kinyume na maadili ya uongozi wa baraza, naomba niishie hapo, kwa mujibu wa dini yetu kueleza kwa undani kuhusu hili ni makosa,”

Akijibu kuhusu hatua hiyo ya kuwasimamisha itachukua muda gani Sheikh Chizenga amesema, “Tutafanya uchunguzi wa kina, hata huko kusimamishwa kwao ni kupisha uchunguzi, halafu baadaye kama itadhihiri vinginevyo basi tutaangalia nini la kufanya,”.

Juhudi za gazeti hili kumtafuta Sheikh Walid Alhady Kawambwa kupitia namba zake zote mbili za simu hazikufanikiwa. Baada ya kushindwa kumpata, gazeti hili lilizungumza na Katibu wake, Sheikh Abdallah, ambaye alisema hana taarifa rasmi kuhusu sababu za kusimamishwa kwa masheikh hao.

Sheikh Abdallah alisema yeye pia alipata taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii kama ilivyokuwa kwa watu wengine.

"Mimi pia nimeiona taarifa hiyo kwenye mitandao ya kijamii kama walivyoiona wengine. Sifahamu sababu za kusimamishwa kwa masheikh hao. Ni vyema waliotoa taarifa hiyo wakaeleza sababu za uamuzi huo," alisema Sheikh Abdallah.