Balozi akata mzizi wa fitina ujenzi bomba la mafuta

Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) nchini, Manfredo Fanti akizungumza alipokuwa akifanyiwa mahojiano na Mhariri wa Uchumi wa Gazeti la Mwananchi, Julius Mnganga (kulia) katika ofisi kuu za umoja huo jijini Dar es Salaam jana. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Wiki mbili tangu Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) litoe tamko la kupinga ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda mpaka Tanga (EACOP), Balozi wa umoja huo nchini, Manfredo Fanti amesema bunge hilo halizuii Tanzania na Uganda wala wawekezaji wake kuendelea na utekelezaji wake.


Dar es Salaam. Wiki mbili tangu Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) litoe tamko la kupinga ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda mpaka Tanga (EACOP), Balozi wa umoja huo nchini, Manfredo Fanti amesema bunge hilo halizuii Tanzania na Uganda wala wawekezaji wake kuendelea na utekelezaji wake.

Balozi Fanti ametoa ufafanuzi huo jana, alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jijini hapa kuhusu mambo kadhaa, ikiwamo mradi huo, mgogoro unaoendelea kati ya Ukraine na Russia na mustakabali wa diplomasia ya Tanzania na EU.

Alisema mamlaka ya bunge hilo ni ya kisiasa na uamuzi wake hauufungi upande wowote, kwa sababu mikataba na sera za umoja huo, husimamiwa na Baraza la Mawaziri.

“Uganda na Tanzania ziko huru kuendelea kuutekeleza mradi huu kwa sababu hizi ni nchi huru, zenye mamlaka kamili. Hata kwa wawekezaji, Total wanaweza wakaendelea na utekelezaji. Bunge la Ulaya haliingilii uhuru wa yeyote kati ya wadau hawa, ila hofu yake ni usalama wa watu watakaopitiwa na mradi huo, pamoja na uharibifu wa mazingira unaoweza kutokea. Uharibifu wa mazingira ni suala linalomgusa kila mtu duniani kwa sasa,” alisema Balozi Fanti.

Mwanadiplomasia huyo mkongwe alisema popote inapotekelezwa miradi mikubwa kama ulivyo huu, ni muhimu watu kuhoji ili kuondoa wasiwasi wowote unaoweza kujitokeza kwenye mazingira unakopita na watu watakaohamishwa.

Alisema anafahamu Serikali na kampuni ya Total, zimeandaa utaratibu wa kuwafidia wananchi watakaoathirika iwe kwa fedha taslimu au kuwajengea makazi mapya, ila uwazi zaidi unahitajika kwa wadau wa ndani na nje wanaoufuatilia.

Hata hivyo, alisema ofisi yake inafuatilia kwa karibu kuona kama kuna malalamiko kutoka asasi za kiraia, na bunge lao nalo linafanya hivyo kwa kutumia njia nyingi za kupata taarifa ilizonazo ukiacha anazopeleka yeye.

“Suala la mazingira linapewa uzito na dunia nzima. Kitu muhimu ni kuongeza uwazi ili watu wasihisi kuwa kuna kitu cha ziada kinafanyika ndani ya miradi kama hii,” alikumbusha.

Ujenzi wa mradi huo ulipewa leseni miaka miwili iliyopita baada ya Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC), kufanya tathmini ya kina kuhusu athari za kimazingira na kijamii zinazoweza kujitokeza.

Tathmini hiyo pia iliishirikisha kampuni za RSK Group, COWI Tanzania na JSB yenye makao makuu yake jijini London, Uingereza.

Alipoulizwa kwa nini Bunge la Ulaya limeipuuza ripoti hiyo bila kujali maoni ya kitaalamu yaliyotolewa na wahusika, Balozi huyo alisema ni ngumu kwake kulielezea hilo, akiamini wenye majibu sahihi ni Bunge lenyewe.

“Balozi wa Tanzania aliye Brussels (makao makuu ya EU) anaweza kusaidia kupata taarifa sahihi kuhusu hili kutoka kwa wabunge au maofisa wa Bunge. Hata hivyo sikushangazwa na uamuzi wa bunge kutoa tamko ambalo limepokelewa tofauti. Kama nilivyosema, bunge ni chombo cha kisiasa ambacho huangalia jinsi mambo yanavyokwenda katika maeneo tofauti,” alisema.

Kwa sasa, kampuni ya Total Energies yenye makao makuu yake nchini Ufaransa ambayo ndio mwekezaji mkubwa wa mradi huo, inajipanga kwenda kujieleza mbele ya EU baada ya kuitwa ikafanye hivyo hapo Oktoba 10, mwaka huu.

Uhusiano wa EU na Tanzania

Licha ya tamko la bunge hilo, Balozi Fanti alisema uhusiano wa EU, Tanzania na Uganda ni mzuri na ushirikiano umeimarika zaidi hivi karibuni, kutokana na ziara za viongozi waandamizi.

Umoja huo alisema umewekeza zaidi ya Euro 180 milioni kwenye miradi ya nishati nchini na kampuni za Ulaya zinahamasishwa kuja kuwekeza kwenye maeneo tofauti, ingawa kuna masuala ya kisiasa yanayojitokeza mara kadhaa.

“Ulaya na Afrika zinahitajiana kwa kiasi kikubwa. Tunategemeana kwa ujuzi, bidhaa na huduma. Ni muhimu kuimarisha uhusiano ulio sawa. Asiwepo anayelaliwa wala anayenufaika zaidi. Kusiwe na unyonyaji wa aina yoyote,” alisema.

Balozi huyo alitambua juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kuvutia uwekezaji kutoka nje, ikiwamo Ulaya huku akisema: “Hivi karibuni Benki ya Ulaya itarudi nchini kuendelea kutoa huduma.”

Vita Ukraine

Wakati vita vinaanza kati ya Russia na Ukraine mwishoni mwa Februari, mabalozi wa nchi za Ulaya nchini waliyaomba mataifa ya Afrika kulaani uvamizi huo, lakini kwa jinsi athari zake zilivyo kubwa kuliko uwezo wao wa kuendelea kuhimili, baadhi zinafikiria kurudisha biashara na Taifa hilo lililowekewa vikwazo na Ulaya.

Ingawa India na China zimekuwa zikishawishi kumalizwa kwa vita hivyo kidiplomasia, bado EU inaendelea kuisaidia Ukraine kwa silaha na askari.

Kuhusu mzozo huo, balozi alisema msimamo wa Umoja wa Ulaya haujabadilika, wanaendelea kulaani uvamizi wa Russia nchini Ukraine ambako mamilioni ya raia wamelazimika kuyakimbia makazi yao huku maelfu wakipoteza maisha, hasa watoto na wanawake.

“Tunaendelea kuisaidia Ukraine kutetea uhuru wake na tunatarajia amani itarejea hivi karibuni. Tumeweka vikwazo kwa baadhi ya raia na kampuni za Russia kuonyesha tunalaani. Tutakuwa tayari kusaidia upatikanaji wa amani nchini Ukraine na tupo tayari kusaidia utekelezaji wake,” alisema.

Fanti alisema wangependa kuona diplomasia inaumaliza mgogoro huo, jambo linalowezekana iwapo pande zinazokinzana ziko tayari kwa mazungumzo ya amani tofautina vita hivi, kwani upande mmoja unauvamia mwingine ambao unajitetea kutokana na uvamizi iliofanyiwa.

Alisema amani haiwezi kupatikana kwa sasa wakati upande mmoja unaendelea kuurushia makombora upande mwingine. Ila, alisema diplomasia itawezekana iwapo silaha zitawekwa chini.

“Ukraine ni taifa linalojitetea na Umoja wa Ulaya inalisaidia. Russia imevunja sheria ya kimataifa ya mkataba wa Umoja wa Mataifa ambayo kila taifa linawajibika kuifuata. Hatupendi kuona hili linatokea kwa Ukraine pekee, bali duniani kote,” alisema.

Kwa hali ilivyo, balozi huyo alisema hana uhakika ni lini EU itaacha kuisaidia Ukraine, iwapo vita hivi havitokoma. Kwa kuangalia ukubwa wa athari zake duniani, balozi alisema jamii ya kimataifa inapaswa kutuma ujumbe kwa Russia kwamba uamuzi wake umesababisha matatizo makubwa ulimwenguni kote.

Kati ya athari za moja kwa moja zilizojitokeza ni kupanda kwa bei ya bidhaa, hasa mafuta na mbolea ambazo Russia ni mzalishaji mkubwa, lakini balozi huyu alisema vikwazo vilivyowekwa ni kwa mafuta ya Russia kutoingia kwenye nchi za Ulaya na si vinginevyo.

“Vikwazo ilivyowekewa Russia havihusishi mbolea, kwani Umoja wa Ulaya unafahamu mataifa mengi yanaitegemea. Tanzania kwa mfano inaweza kufanya biashara hiyo na Russia,” alisema.

Vikwazo vilivyotolewa, alisema vinabagua kwani vimewekwa kwa baadhi ya watu binafsi, hasa watendaji waandamizi, serikali, benki, kampuni na mashirika kutokana na uvamizi ilioufanya Russia.

“Vikwazo hivi vinachanganya kidogo, unahitaji kuvisoma kwa utulivu. Tanzania na Afrika kwa ujumla inaweza kuendelea kuagiza mbolea kutoka Russia. Ninafahamu kwamba bei imepanda sana kutokana na vikwazo vilivyowekwa ila Serikali inachukua hatua za makusudi kurekebisha hali hii,” alisisitiza.