Balozi Kattanga aitaka TCRA kuwa mlezi, sio mdhibiti

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga akizungumza alipokuwa akifungua semina ya uchumi wa kidijiti kwa mamlaka za juu za maamuzi ya sera nchini, iliyofanyika Zanzibar. Semina hiyo imehudhuriwa na baadhi viongozi wakiwemo mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na viongozi kutoka taasisi mbalimbali za serikali. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga ametoa ushauri kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwa wakitaka nchi kufanikiwa na kuiikuza teknolojia katika uchumi wa kidigitali ni lazima wawe wawezeshaji badala ya kuwa mdhibiti.

  

Zanzibar.  Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga ametoa ushauri kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwa wakitaka nchi kufanikiwa na kuiikuza teknolojia katika uchumi wa kidigitali ni lazima wawe wawezeshaji badala ya kuwa mdhibiti.

Balozi Kattanga ameyasema hayo leo Machi 8, 2022 alipokuwa akifungua semina ya uchumi wa kidijiti kwa mamlaka za juu za maamuzi ya sera nchini, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Marijani Hoteli Zanzibar.

Amsema ili TCRA ifanikie, haina budi kuwa mzazi wa watumiaji na watoa huduma kwa kufanya kazi ya kukuza mahusiano yao na sekta binafsi ambao ni wadau wakubwa katika sekta ya mawasiliano.

“Hapa nataka kuiomba TCRA na Wizara tuchukue majukumu ya kuwa wawezeshaji badala ya kuwa wadhibiti, maana yake Serikali kwa uhalisia inapenda kudhibiti lakini katika haya nafikiri tuchukuwe nafasi ya kuwa mwezeshaji kama mzazi,” amesema Balozi Kattanga.

Akitoa mfano watoa huduma ya redio na televisheni hapa nchini ambazo nyingi ni za sekta binafsi, ameitaka TCRA kuzilea na kuziwezesha kutoa huduma.

“Hizi redio na televisheni nyingi sio za Serikali ni za watu binafsi kwa hiyo tuna wajibu wa kuhakikisha tunakuwa kama ni mzazi, mlezi badala ya kuwa mbabe kwa hiyo hiyo tukiiweka kando tutapata washiriki wengi kabisa watatusogelea,” amesema Balozi Kattanga.

Balozi Kattanga amesema ni muhimu mamlaka hiyo kuwa wasikivu na kufanya tasnia hiyo ikuwe kwa hiyo ni lazima kutakuwa na changamoto za watu kufanya makosa hapo ndipo wachukuwe jukumu la kufanya kazi ya malezi. 

Kuhusu umuhimu wa semina hiyo, Balozi Kattanga ameupongeza uongozi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na TCRA kwa kuandaa mafunzo hayo kwa viongozi hao kwa kuwakutanisha pamoja.

“Mmefanya jambo jema leo kwa kuwakutanisha viongozi hawa wenye maarifa, ujuzi na uelewa mbali mbali kwa lengo la kuwaongezea maarifa yao kuhusu ujenzi wa uchumi wa kidijitali,” amesema Balozi Kattanga

Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kuwa mafunzo hayo yatafanyika kwa makundi mbali mbali ili viongozi wengine waweze kupata mafunzo na kunufaika nayo kwa kuwa viongozi ndio wanaoshika usukani wa kuendesha nchi.

Nape amesema baada ya kupata mafunzo hayo anaamini wataendesha vema taasisi za Serikali ili kuendana na ukuaji wa uchumi na uchumi wa kidijitali ili wananchi na taifa lilweze kunufaika na maendeleo ya Tehama nchini kuelekea Mapinduzi ya nne ya viwanda ambapo Tanzania imeamua kujikita kujenga uchumi wa kisasa wa kidijitali kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo 2025.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Jim Yonazi amesema kuwa ana amini kuwa baada ya mafunzo hayo Serikali itabadilisha kabisa namna ya utendaji kazi kwa kuongeza matumizi ya Tehama nchini.

Semina hiyo ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wakiwemo mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na viongozi wengine kutoka taasisi mbalimbali za serikali.

Imeandikwa na

Edwin Mjwahuzi, Mwananchi