Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Balozi Sefue: Maandamano yafanyike kwa kufuata sheria

Muktasari:

  • Kauli hiyo ya Balozi Sefue imekuja katika kipindi ambacho kumekuwa na vuguvugu la kufanyika maandamano yanayohamasishwa kupitia mitandao ya kijamii, kushinikiza mabadiliko ya Katiba na mageuzi katika mifumo ya uchaguzi.



Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue amesema maandamano ni moja ya haki muhimu za kidemokrasia na kikatiba, lakini yanapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia sheria.

Pia, ametaja jambo linalomtia wasiwasi kwa vijana wa sasa maarufu kama Gen-Z, kuwa ni tamaa ya kupata mafanikio ya haraka bila uvumilivu na maandalizi ya muda mrefu huku akiwasifu kwa uwezo wao mkubwa wa kutumia teknolojia.

Balozi Sefue ameyasema hayo wakati akizungumza na jopo la wanahabari wa Mwananchi Communications Limited (MCL), katika mahojiano maalumu yaliyofanyika katika Taasisi ya Uongozi jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo ya Balozi Sefue imekuja katika kipindi ambacho kumekuwa na vuguvugu la kufanyika maandamano yanayohamasishwa kupitia mitandao ya kijamii, kushinikiza mabadiliko ya Katiba na mageuzi katika mifumo ya uchaguzi.

Maandamano ya hivi karibuni, yalipangwa kufanyika Julai 7, 2026, hata hivyo hayakufanyika. Vyombo vya ulinzi na usalama vilisambaa mitaani kwa ajili ya kuimarisha usalama na mitaa mingi katika mikoa mbalimbali ilionekana kuwa tupu huku biashara zikifungwa.

Vuguvugu hilo ni mwendelezo wa maandamano yaliyotokea siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, yaliyotawaliwa vurugu na kusababisha vifo vya watu 518, kwa mujibu wa Tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza matukio wakati wa baada ya uchaguzi.

Vilevile, maandamano hayo yalitawaliwa na uharibifu wa miundombinu ya umma pamoja na mali za watu binafsi kama vile magari na vituo vya mafuta ambavyo vilichomwa moto na waandamanaji.


Kuhusu maandamano

Balozi Sefue ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Uongozi, amesema haki ya kuandamana ni miongoni mwa misingi muhimu ya demokrasia inayotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria za kimataifa zinazolinda uhuru wa kujieleza.

Hata hivyo, amesema haki hiyo haiwezi kutenganishwa na wajibu wa kuheshimu sheria, usalama wa watu wengine na shughuli za kijamii na kiuchumi.

Katika hoja hiyo, amesema changamoto si kuwepo kwa haki ya kuandamana, bali ni kushindwa kwa baadhi ya watu kutofautisha kati ya uhuru huo na vitendo vinavyoingia katika uhalifu.

Balozi Sefue, aliyewahi kuiwakilisha Tanzania nchini Marekani na Cuba, amesema viwango vya kimataifa vinatambua na kulinda maandamano ya amani, lakini haviruhusu vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa wengine au kuvuruga haki zao za msingi.

“Tunapaswa kutambua kuwa kuandamana ni haki ya msingi. Lakini wakati huohuo ni muhimu kujua mahali haki hiyo inapokomea na mahali uhalifu unapoanzia,” amesema.

Amefafanua kuwa maandamano yanayolazimisha wafanyabiashara kufunga shughuli zao au kuwatia hofu wananchi hayawezi kuhesabiwa kuwa sehemu ya matumizi halali ya haki za kiraia.

Kwa mfano, amesema mtu anayebeba jiwe au kitu kinachoweza kutafsiriwa kama tishio kwa wengine, huondoka katika mipaka ya maandamano ya amani yanayotambuliwa kisheria.

Mwanadiplomasia huyo aliyewahi kuwa Mwandishi wa Hotuba wa Rais wa awamu ya Pili, hayati Ali Hassan Mwinyi, amesema utaratibu wa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola kabla ya maandamano haukusudiwi kunyima watu haki zao, bali kusaidia kulinda usalama wa waandamanaji na wananchi wengine.

Akirejea uzoefu wake akiwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN), amesema Mji wa New York ni mfano mzuri wa namna maandamano yanavyoweza kufanyika kwa ustaarabu.

Amesema karibu kila siku kuna maandamano katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, hata hivyo amesema washiriki wake hufuata masharti yaliyowekwa na mamlaka husika.

Amesema waandamanaji hukubaliana na Polisi kuhusu maeneo ya kusimama, hubeba mabango na kutoa jumbe zao bila kusababisha vurugu wala kuvuruga shughuli za wengine.

“Huo ndiyo ustaarabu wa kuandamana. Watu wanatoa maoni yao kwa uhuru, lakini bila kuathiri maisha ya wengine,” amesema.

Balozi huyo ameonya dhidi ya tabia ya kuiga kila kinachotokea katika mataifa mengine bila kuzingatia mazingira na mahitaji ya ndani ya Tanzania.

Amekumbushia kauli ya Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, aliyewahi kushauri wananchi “za kuambiwa changanya na zako” akimaanisha kuchanganya ushauri wanaopewa na ya akili zao wenyewe kabla ya kufanya uamuzi.

Kwa mtazamo wake, baadhi ya nchi zimepitia machafuko makubwa yaliyoambatana na uharibifu wa mali na kupotea kwa maisha ya watu kutokana na maandamano yaliyokosa mwelekeo.

Amesema Watanzania wanapaswa kujifunza kutokana na uzoefu huo badala ya kuiga matukio yaliyosababisha madhara kwa jamii na uchumi wa nchi husika.


Gen-Z na teknolojia

Akizungumzia vijana wa Gen-Z, Balozi Sefue aliyehudumu chini ya marais wanne tofauti, amesema kundi hilo lina uwezo mkubwa wa kutumia teknolojia na mifumo ya kisasa ya mawasiliano kuliko vizazi vilivyotangulia.

Amesema uwezo huo ni rasilimali muhimu inayoweza kusaidia maendeleo ya Taifa iwapo utatumika kwa malengo sahihi na yenye manufaa.

Hata hivyo, ameonya kuwa teknolojia inaweza kuwa chanzo cha matatizo ikiwa itatumika bila uchambuzi wa kina na busara zinazostahili.

Amenukuu kauli ya Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, aliyesema kuwa “kila zama na kitabu chake”, akimaanisha kuwa kila kizazi kina mazingira yake ya kipekee ambayo ni tofauti na kingine.

Kwa mtazamo wake, viongozi na wazazi wanapaswa kujifunza kuelewa tabia na mahitaji ya vijana wa sasa badala ya kuwahukumu kwa kutumia vigezo vya zamani.

Amesema mtandao umejaa taarifa sahihi, taarifa zenye upungufu na taarifa za uongo, hivyo vijana wanapaswa kujifunza kuchambua kabla ya kuamini kila wanachokiona.

“Matumaini yangu ni kwamba watatumia teknolojia kujijenga na kujiendeleza badala ya kujiharibia maisha yao,” amesema.

Moja ya mambo yanayomtia wasiwasi zaidi ni kile alichokiita tamaa ya mafanikio ya haraka inayojitokeza kwa baadhi ya vijana wa kizazi cha sasa.

Amesema mafanikio ya kudumu yanahitaji msingi imara, uvumilivu na maandalizi ya muda mrefu badala ya kutegemea njia za mkato.

Kwa mfano, amewashauri wafanyabiashara wachanga kutoongeza shughuli zao kwa kasi kabla hawajajenga misingi thabiti ya biashara zao.

Amesema kupanuka haraka bila maandalizi ya kutosha kunaweza kusababisha hasara kubwa na hata kufilisika.

Kwa vijana wanaojenga taaluma zao, Balozi Sefue amesisitiza umuhimu wa kupanda ngazi hatua kwa hatua na kufanya uamuzi baada ya kujiridhisha kuwa msingi wao ni imara.

Kuhusu uongozi, amesema viongozi wa kisasa wanapaswa kuelewa kuwa vijana wa leo wana tabia ya kuuliza maswali na kutaka maelezo zaidi kuliko vizazi vya zamani.

Amesema hali hiyo haipaswi kuonekana kama tatizo, bali kama fursa ya kupata mawazo mapya yanayoweza kusaidia maendeleo ya taasisi na jamii.

Amesema kiongozi bora ni yule anayejenga mazingira yanayowaruhusu vijana wenye elimu na ubunifu kutoa mawazo yao bila hofu.

Akirejea maisha yake binafsi, Balozi Sefue amesema mafanikio aliyoyapata yalitokana kwa kiwango kikubwa na malezi aliyopata kutoka kwa wazazi wake.

Amesema mama yake, ambaye anatambulika kuwa mwalimu wa kwanza mwanamke Tanganyika, alimjengea mapema utamaduni wa kusoma vitabu na kujitegemea.

Ameeleza mafunzo hayo yalimsaidia kuwa na msingi mzuri hata kabla ya kuanza elimu rasmi akiwa na umri wa miaka sita.

Hata hivyo, ameeleza wasiwasi wake kuhusu mabadiliko yanayotokea katika malezi ya watoto katika jamii ya sasa.

Amesema wazazi wengi wanatumia muda mwingi katika kazi na shughuli nyingine kiasi cha kushindwa kuwa karibu na watoto wao.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya watoto wanakulia mikononi mwa wafanyakazi wa ndani, marafiki au makundi rika badala ya kupata mwongozo wa karibu kutoka kwa wazazi.

Balozi Sefue amependekeza kuimarishwa kwa mitaala ya elimu kuanzia ngazi za awali ili kujumuisha maadili, utu na misingi ya tabia njema.

Amesema hatua hiyo inaweza kusaidia kuendeleza mafunzo yanayotolewa nyumbani na kujenga kizazi chenye misingi imara ya maadili.

Kwa maoni yake, jukumu la kuwaandaa watoto kwa maisha ya baadaye haliwezi kuachwa kwa shule pekee wala kwa wazazi pekee.

Amesema familia, shule, taasisi za dini na Serikali vinapaswa kushirikiana katika kulea na kuwaandaa vijana kwa dunia inayobadilika kwa kasi.

“Uongozi ni kuangalia mbele na kuhakikisha tunakiandaa kizazi kijacho kwa dunia ya kesho, si dunia ya jana,” amesema.

Itaendelea kesho