Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Balozi Yakubu asisitiza ushirikiano Afrika kulinda urithi wa dunia


Muktasari:

  • Tanzania imetaka ushirikiano wa Afrika katika kulinda urithi wa bara hilo.

Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Saidi Othman Yakubu, amesema nchi za Afrika zinapaswa kuendelea kushirikiana katika kulinda, kuhifadhi na kuendeleza urithi wa asili na wa utamaduni wa bara hilo.

Pia zihakikishe sauti ya Afrika inasikika kwa nguvu katika majukwaa ya kimataifa yanayojadili masuala ya urithi wa dunia.

Balozi Yakubu, ambaye pia ni mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), ameyasema hayo leo, Jumanne Juni 16, 2026 alipokuwa akiongoza mkutano wa tisa wa Nchi Wanachama wa Afrika katika Kamati ya Urithi wa Dunia ya Unesco uliofanyika jijini Dakar, Senegal.

Mkutano huo uliwakutanisha wajumbe kutoka Senegal, Angola, Kenya, Namibia, Comoro, Togo, Gambia, Uganda, Tanzania, Afrika Kusini, Malawi na Tunisia kwa lengo la kuratibu misimamo ya pamoja ya Afrika kuelekea kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia ya Unesco kitakachofanyika Busan, Jamhuri ya Korea.

Balozi Yakubu, amesema ushirikiano wa nchi za Afrika ni muhimu katika kuhakikisha maeneo ya urithi wa dunia yaliyopo barani humo yanahifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo, sambamba na kuimarisha mchango wa Afrika katika uamuzi unaofanywa ndani ya Unesco.

"Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa mengine ya Afrika katika kuendeleza ajenda za urithi wa dunia na kuhakikisha masilahi ya bara yanapewa kipaumbele katika mijadala na maamuzi yanayofanyika ndani ya Unesco.”

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mkuu wa Kundi la Afrika katika Unesco na Mwakilishi wa Kudumu wa Senegal katika Unesco, Balozi Pierre Faye na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Urithi wa Dunia wa Afrika (AWHF), Dk Albino Jopela.

Katika majadiliano yao, wajumbe walijadili hali ya uhifadhi wa maeneo mbalimbali yaliyopo katika orodha ya urithi wa dunia barani Afrika, pamoja na mikakati ya kuimarisha usimamizi wa maeneo hayo na kuondoa yale yaliyowekwa katika orodha ya maeneo yaliyo katika hatari.

Vilevile, mkutano ulijadili namna ya kuongeza uwakilishi wa maeneo ya Afrika katika orodha ya urithi wa dunia ya Unesco, hatua inayolenga kutambua na kuhifadhi maeneo yenye thamani ya kipekee ya kihistoria, kitamaduni na kiasili yaliyopo katika bara hilo.

Washiriki walibadilishana uzoefu kuhusu changamoto zinazoikabili sekta ya urithi wa dunia Afrika, ikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la shughuli za kibinadamu katika maeneo ya urithi, upungufu wa rasilimali za uhifadhi na umuhimu wa kuhusisha jamii katika juhudi za kulinda urithi huo.

Aidha, mkutano ulitathimini fursa za kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika, Unesco na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha urithi wa bara hilo unalindwa na kutumika kama nyenzo ya maendeleo endelevu, utalii, ajira na ustawi wa jamii.

Mkutano huo umefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya Mfuko wa Urithi wa Dunia wa Afrika (AWHF), taasisi iliyoanzishwa kusaidia juhudi za uhifadhi, usimamizi na maendeleo ya maeneo ya urithi wa dunia barani Afrika.