Watamani taasisi maalumu itakayoshughulikia AI Tanzania
Kituo cha Utafiti wa Maadili na AI kikizinduliwa katika chuo Kikuu cha UAUT jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuwasaidia watanzania kujengewa msingi mzuri wa AI.
Muktasari:
- Taasisi hiyo maalumu itapaswa kusimamia maendeleo, uwekezaji, matumizi ikiwemo katika kufanya tafiti na udhibiti wa AI katika kulinda maadili nchini.
Dar es Salaam. Licha ya uandaaji wa sera, miongozo na kanuni za teknolojia ya akili unde (AI) Tanzania, wataalamu katika eneo hilo wameshauri kuwepo kwa wakala au taasisi itakayoshughulikia masuala mazima ya teknolojia hiyo inayozidi kushika kasi kutokana na matumizi yake ya usaidizi.
Taasisi hiyo maalumu itapaswa kusimamia maendeleo, uwekezaji, matumizi ikiwemo katika kufanya tafiti na udhibiti wa AI katika kulinda maadili nchini, kusimamia wataalamu wa AI, kuwa mshauri kati ya kampuni na Serikali ambapo itatumika kama daraja.
Akizungumza baada ya hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Utafiti na Maadili ya AI katika wiki ya AI iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha United African University of Tanzania (UAUT), hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya tafiti ya AI Afrika (Arifa), Dk Dennis Mwighusa, alishauri akisema pia taasisi itatoa ushauri kwa Serikali kuu kuhusu ujio wa teknolojia mbalimbali mpya na athari zake.
“Kinachotakiwa ni kuwa na taasisi au wakala maalumu itakayosimamia shughuli zote za AI, mfano itaweza kutumika kusimamia taasisi zote za AI. Pia ikumbukwe ni kweli AI inakua haraka na bado ni sehemu ya teknolojia ya habari na mawasiliano,” amesema,
Akitolea mfano nchi ya Rwanda amesema tayari wanao wakala maalumu unaosimamia teknolojia hiyo, huku akisema ni hatua muhimu katika maendeleo.
Aidha, Dk Mwighusa amesema elimu kuhusu AI haipaswi kubaki kwa wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pekee bali inapaswa kuwafikia watu wa kada zote, ikiwemo afya, kilimo, sheria na biashara.
Katika hilo, Serikali inapaswa kuwekeza katika wataalamu wa ndani, mafunzo endelevu na mifumo ya maadili ili Tanzania ijenge uwezo wake wa ndani badala ya kutegemea mifumo na maarifa kutoka nje.
Pia, upo umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, vyuo vikuu na sekta binafsi ili kuharakisha matumizi salama ya AI na kupunguza pengo la utegemezi wa teknolojia.
Mchumi aliyejikita katika uchumi wa kidijitali, Francis Nyonzo, amesema kama walaji kuna utaalamu wowote wa kuangalia na kufuatilia kila AI inayokuja inatumikaje na inakiuka nini kwa Watanzania? “Hivyo kukiwa na wataalamu wa namna hiyo tutaweza kuangalia shughuli nzima za AI na hatari zake.”
Mtaalamu Mwandamizi wa Elimu, Mhandisi Henry Kulaya, amesema taasisi ya AI itachochea katika maendeleo yake kwa kuwa itakuwa mahususi kwa ajili ya teknolojia hiyo.
AI haiwezi kuchukua nafasi ya binadamu
Kulaya amesema Tanzania ipo katika kipindi muhimu cha mageuzi ya elimu na AI haiwezi kuchukua nafasi ya akili ya binadamu inayotegemea uamuzi, ubunifu, fikra pevu na maadili.
Amesema taasisi za elimu ya juu zinapaswa kubadili mwelekeo wa ufundishaji ili kuzalisha watu wenye uwezo wa kufikiri kwa kujitegemea badala ya wanaotegemea majibu ya mifumo ya kiotomatiki.
Pia, ameeleza wasiwasi kuhusu matumizi ya AI katika kazi za kitaaluma na kusema badala ya kupiga marufuku teknolojia hiyo, vyuo vinapaswa kubadili mifumo ya tathmini ili kuhimiza uchambuzi, kuuliza maswali na uelewa wa kina.
Mkurugenzi Dennis Mwighusa akizungumza kuhusu ushauri wa kuanzishwa kwa taasisi ya AI Tanzania.
Kituo kipya cha utafiti na maadili ya AI
Katika hatua nyingine kumezinduliwa kituo cha tafiti na maadili ya akili unde katika chuo cha UAUT ambacho kitasimamia maadili kama alivyobainisha Mhadhiri wa chuo hicho, Daniel Sogoja.
Katika kituo hicho Watanzania watafundishwa ujuzi wa kuandika na kupanga maelekezo (prompts) kwa usahihi ili AI itoe majibu bora, sahihi na yanayokidhi mahitaji ya mtumiaji, AI gani bora ya kutumia kuhusu eneo analofanyia kazi,
“AI inazidi kukua hivyo kituo hichi kitajihusisha na tafiti za namna ya kutumia kupata suluhisho la matatizo mbalimbali,” amesema.
Profesa Anthony Choi wa Chuo Kikuu cha Mercer kilichopo nchini Marekani amesema taarifa sasa imekuwa rasilimali muhimu ya kimkakati duniani, hivyo nchi zisizo na usimamizi madhubuti zinaweza kupoteza udhibiti wa mamlaka yao ya kidijitali.
Kwa mtazamo wake, mapinduzi ya AI hayahusu tu uwezo wa teknolojia kufanya kazi kwa akili, bali pia yanahusu udhibiti wa rasilimali na mamlaka.
Naye, Makamu Mkuu wa chuo cha UAUT, Profesa Sung Kim, amesema maendeleo ya AI lazima yaongozwe na misingi ya utu wa binadamu na haki za kijamii.
Ameonya dhidi ya matumizi ya teknolojia yanayoweza kuongeza pengo la usawa badala ya kuhamasisha ushirikishwaji wa wananchi wote.
Mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo hicho, Sally Figueiredo amesema AI inaweza kutumika kwenye kilimo kujua mazao yenye changamoto, kutumika katika elimu na afya hivyo lazima iwe na misingi ya usimamizi.